Afisa
kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Bw. Frank Muhina akiwa
kazini kunukuu mambo mbalimbali kutoka kwa Afisa wa Wizara ya Mambo ya
Nje ya Uturuki.
Na Ally Kondo, Uturuki
WATURUKI WAHIMIZWA KUWEKEZA TANZANIA
Waturuki
wenye mitaji wamehimizwa kuja Tanzania kuchangamkia fursa lukuki za
uwekezaji zinazopatikana nchini. Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) wakati
wa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Uturuki tarehe 08 na 09 Mei,
2014.
Katika
ziara hiyo, Waziri Membe aliweza kuonana na kufanya mazungumzo na
Viongozi wa Kitaifa wa Serikali ya Uturuki akiwemo Waziri Mkuu, Mhe.
Recep Tayyip Erdogan; Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Emrullah Isler; Waziri wa
Mambo ya Nje, Mhe. Ahmet Dovutoglu na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Lutfi
Elgan.
Aidha,
Mhe. Waziri na mwenyeji wake, Mhe. Dovutoglu walifanya mkutano wa
pamoja na waandishi habari pamoja na kushiriki chakula cha mchana na
wafanyabiashara wakubwa wa Uturuki.
Mhe.
Waziri alieleza kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji ambazo
hazijatumiwa ipasavyo, hivyo ni muda muafaka kwa Waturuki kuwekeza
mitaji yao nchini Tanzania kwa faida ya pande zote.
Baadhi ya maeneo ambayo yatakuwa na faida kubwa endapo yatapata wawekezaji ni pamoja na sekta ya usafiri wa anga. Hivyo, Mhe.
Waziri alilihamasisha Shirika la Ndege la Uturuki kuangalia uwezekano
wa kuingia ubia na Shirika la Ndege la Tanzania. “Endapo Shirika la
Ndege la Tanzania litapata mwekezaji, likawa na ndege za kutosha na kwa
sababu Tanzania imezunguukwa na nchi nyingi, wasafiri wengi wa nchi
hizo, watatumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere kuunganisha safari zao kwenda nchi za Ulaya”. Mhe. Membe
alisikika akiwambia Viongozi wa Uturuki pamoja na wafanyabiashara
wakubwa
Waziri
Membe pia aliwahahakishia wawekezaji wa Uturuki watakaokuwa na dhamira
ya kuwekeza nchini, kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Ukanda Maalum wa
Uwekezaji (EPZA) itatoa eneo maalum ili wawekezaji hao waweze kujenga
viwanda vya uzalishaji. Alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika viwanda
vya nguo, mbolea, gesi, zana za kilimo, miundombinu ya umwagiliaji,
umwagiliaji wa matone pamoja
na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, nyama na maziwa. Alisema
endapo sekta hizo zitafanyiwa kazi ipasavyo basi ukuaji wa uchumi
utaenda sambamba na ustawi wa maisha ya watu wa kawaida, kwa sababu
sekta hizo zitaongeza ajira kwa maelfu ya vijana wa Tanzania.
Aliendelea
kueleza kuwa ili ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki uendelee
kuimarika, Serikali itatimiza ahadi yake ya kufungua Ubalozi nchini
Uturuki katika mwaka wa Fedha 2014/2015.
Kwa
upande wao, Viongozi wa Uturuki walimuhakikishia Mhe. Membe kuwa
watawahamasisha wafanyabiashara wa Uturuki kuja kuwekeza Tanzania.
Walisema kazi hiyo kwao ni nyepesi na wanahakika itapokelewa vizuri na
jumuiya ya wafanyabiashara kwa sababu Tanzania mbali na kuwa na fursa
nyingi, pia ina utulivu wa kisiasa ambao ni kigezo muhimu katika uwekezaji.
Katika
hatua nyingine, Mhe. Membe aliishukuru Serikali ya Uturuki kwa kitendo
chake cha kukubali wanamichezo 10 wa Tanzania kuweka kambi ya mafunzo
kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika
Scotland mwezi wa Julai, 2014.
Sanjari
na shukrani hizo, alimshukuru pia Balozi wa Uturuki nchini Tanzania na
Mke wake kwa jitihada zao za kunusuru maisha ya watu wenye ualbino.
Alisema uamuzi wao wa kujenga kijiji ambacho kitakuwa na uwezo wa
kuchukuwa watu wenye ualbino 500 kwa ajili ya kuwapa elimu na stadi
nyingine za maisha ni mfano wa kuigwa na jamii ya wasamalia wema.
Vile vile, Mhe. Waziri aliishukuru Uturuki kwa kulisaidia Shirika la Utangazaji la Taifa Tanzania (TBC) kwa kulipa vifaa na teknolojia ya kisasa. Alisema kabla ya msaada huo, TBC ilikuwa inafanya kazi katika mazingira magumu
|
No comments:
Post a Comment