JUMUIYA YA MADOLA : WABUNGE KUTOKA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA MADOLA (CPA) WALALAMIKA KUFANYWA "ATM" NA WANANCHI - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Wednesday, 28 May 2014

JUMUIYA YA MADOLA : WABUNGE KUTOKA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA MADOLA (CPA) WALALAMIKA KUFANYWA "ATM" NA WANANCHI


Wabunge kutoka nchi kadhaa barani Afrika na nje ya bara hilo wamelalamikia uelewa mdogo miongoni mwa wananchi wa kawaida kuhusiana na majukumu ya wabunge na kuwafanya wananchi hao wawaone wabunge wao kama chanzo kikubwa cha fedha. 
 Malalamiko hayo yalitolewa jana na wabunge kadhaa wanahudhuria semina ya 25 ya Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola, inayofanyika jijini Dar es Salaam. Mjadala kuhusu suala hilo uliibuliwa na Mbunge wa Rungwe Mashariki, Prof David Mwakyusa (CCM), wakati akichangia mada kwenye semina hiyo. 
 Mbunge huyo ambaye ni mongoni mwa wabunge kadhaa wanaoliwakilisha Bunge la Tanzania kwenye semina hiyo, alisema kuwa wananchi wengi hawaelewi maana hasa na wajibu wa mwakilishi wao kwenye chombo cha kutunga sheria.
 “Watu wengi wanamuona Mbunge kama mtu mwenye fedha nyingi sana ambaye anapaswa kuwatatulia matatizo yao mbalimbali kama vile kulipa ada kwa ajili ya mtoto, kulipia gharama za matibabu au kumalizia ujenzi wa nyumba,” alisema na kuongeza:
 “Matokeo yake, kila Mbunge unapoonekana kwenye jimbo lako wananchi wanaona kama Benki ya Dunia ndogo imekuja na hivyo wanajipanga wakisubiri kupata chochote kutoka kwako.” 
 Ingawa Prof Mwakyusa alitoa hoja hiyo akidhani kuwa ni tatizo hilo linawakabili wabunge wa Tanzania tu, wakati wa mjadala huo ilibainika kuwa tatizo hilo limeenea barani Afrika na nje ya bara hilo, hasa katika nchi zinazoendelea. 
 Mwasilishaji wa mada iliyozua mjadala huo, Dk Benjamin Bewa-Nyong Kunbour, ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa Serikali katika Bunge la Ghana na Waziri wa Masuala la Bunge, alibainisha kuwa tatizo hilo lipo pia nchini kwao. 
 “Kama huku wananchi wanamuona mbunge kama Benki ya Dunia ndogo, kule kwetu mambo ni magumu zaidi kwa sababu wananchi wanamuona mbunge kama Benki ya Dunia kubwa sana,” alisema Dk Kunbour na kuwaacha watu wengi na mshangao.
 Alibainisha kuwa ni kweli wananchi wengi hawana uelewa mkubwa kuhusiana na majukumu ya mbunge na matumizi ya fedha yamekuwa ni moja ya viungo kati ya mbunge na wananchi waliomchagua. 
 Akitoa uzeofu wa Ghana katika suala hilo, Dr Kunbour alibainisha kuwa iwapo mbunge anakuwa bahili na kushindwa kuwapatia wananchi wake fedha, uwezekano wa kuchaguliwa tena katika uchaguzi unaofuatia unakuwa ni mdogo sana. 
 “Wapo wabunge ambao wanashinda kwenye majimbo yao wakishughulikia kero zinazowakabili wananchi lakini kwa sababu hawatoi fedha wananchi hawawaoni kama wana maana kwao. 
Kuna wabunge wengine hawaendi kabisa katika majimbo yao lakini kwa sababu wanatoa fedha na kuhakikisha zinawafikia wananchi, wanapendwa sana na wananchi wao,” alisema. 
 Alisema hilo ni jambo linaloshangaza sana kwa sababu huko Ulaya matumizi ya fedha kutoka kwenye mfuko binafsi wa Mbunge kwa ajili ya kuwaridhisha wananchi linachukuliwa kuwa ni rushwa wakati barani Afrika suala hilo linaonekana kuwa ni ukarimu.
   Mjumbe kutoka Tanzania Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na wabunge wengine kutoka nchi washiriki wakifuatilia mada kwa makini
   Katibu Mkuu wa CPA Dkt. William shijja akifafanua jambo wakati Mnadhimu Mkuu wa Serikali katika Bunge la Ghana ambaye pia ni Waziri anayeshughulikiwa maswala ya Bunge Dkt. Benjamini Bewa- Nyang Kunbour akiwasilisha mada yake kuhusu Mahusiano  ya Mbunge na chama chake wakati wa siku ya pili ya semina ya 25 ya Chama cha Mabunge wanachama wa jumuiya ya Madola CPA
 Mbunge kutoka News Zealand Asenati Lole- Taylor akichangia uzoefu wan chi yake baada ya kuwasilishwa mada kuhusu Mahusiano  ya Mbunge na chama chake na Mnadhimu Mkuu wa Serikali katika Bunge la Ghana Dkt. Benjamini Bewa- Nyang Kunbour
 Mbunge kutoka Tanzania Mhe. Prof. David Mwakyusa akiuliza swali kupata uzoefu wa namna Wabunge wa nchi nyingine wanavyoshirikiana na wananchi wao majimboni
    Mhe. Elijah Muohima kutoka Zambia akiuliza swali wakati wa Semina
 Wabunge wakifuatilia mada
 Wabunge wakisikiliza kwa makini mada kutoka kwa Mhe. Dkt. Benjamini Bewa- Nyang Kunbour, Mnadhimu Mkuu katika Bunge la Ghana
 Wabunge wakifuatilia mada
Ujumbe wa Tanzania katika semina ya 25 ya Chama cha Mabunge wanachama wa jumuiya ya Madola CPA ukiwa katika mazungumzo  na Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilila baada ya mapumziko 
Picha na Owen Mwandumbya

No comments:

Post a Comment