Elizabeth Michael "LULU" |
Dar es Salaam. Mwigizaji maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael Kimemeta, amekiri mahakamani kuwa na uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa mwigizaji mwenzake, Steven Kanumba na pia kuwa ugomvi na Kanumba siku ya tukio la kifo cha mwigizaji huyo, lakini akakana mashtaka ya kumuua bila kukusudia.
Lulu ambaye yuko nje
kwa dhamana anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, akidaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, kinyume cha Kifungu cha 195 cha
Kanuni za Adhabu (PC), April 7, 2012, nyumbani kwa marehemu Kanumba, Sinza
Vatican.
Jana Lulu alipandishwa
kizimbani mahakamani hapo na kujibu mashtaka hayo kwa mara ya kwanza tangu
alipofunguliwa kesi hiyo, ambapo alikana kumuua Kanumba bila kukusudia.Kesi
hiyo namba 125 ya mwaka 2012 inasikilizwa na Jaji Rose Teemba.
Kukubali kuwa na uhusiano
wa kimapenzi na Kanumba, ni miongoni mwa mambo manane ambayo mshtakiwa huyo
aliyakiri mahakamani hapo jana, kama mambo yasiyobishaniwa katika kesi hiyo.
Mambo mengine ambayo
Lulu aliyakiri mahakamani hapo yaliyoko katika maelezo ya kesi hiyo ni pamoja
na jina na anuani yake, kwenda nyumbani kwa Kanumba usiku wa tukio hilo, kuwa
na ugomvi na Kanumba pia Kanumba kumzuia kutoka nje ya chumba alipojaribu
kutoka ili akimbie.
Mengine ni kufanikiwa
kutoka nje ya chumba cha Marehemu Kanumba, kumweleza mdogo wa Kanumba (Seth
Bosco) kuwa Kanumba ameanguka, kukamatwa kwake na polisi eneo la Bamaga, saa 11
Alfajiri ya usiku wa tukio hilo na kwamba kweli anashtakiwa kwa kosa la kumuua
Kanumba bila kukusudia.
Kama jana Lulu
angekiri mashtaka hayo baada ya kusomewa, basi mahakama ingemtia hatiani na
kumhukumu adhabu ambayo ingeona inafaa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, baada ya
kukana mashtaka hayo, sasa kesi hiyo itaingia katika hatua nyingine ya
usikilizwaji kamili (trial), ambapo upande wa mashtaka utalazmika kuwaita
mashahidi wake mahakamani ili kuthibitisha kuwa Lulu alimuua Kanumba bila
kukusudia.
Pia Lulu atalazimika
kujitetea yeye binafsi na pia kuwaita mahakamani mashahidi wa kumtetea na kisha
mahakama itaandaa na kutoa hukumu yake.
Wakili wa Serikali,
Mbogo aliiarifu mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, upande wa
mashtaka utakuwa na mashahidi wanne ambao ni pamoja na Seth Bosco, Daktari
binafsi aliyekuwa akimhudumia Kanumba, Dk Paplas Kageiya, Ester Zephania na
Askari D/Sgt Ernatus wa Kituo cha Polisi Oysterbay.
Pia Wakili Mbogo
aliwasilisha mahakamani vielelezo viwili vitakayotumika kama sehemu ya ushahidi
katika kesi hiyo ambayo ni taarifa ya kitabibu ya uchunguzi wa chanzo cha kifo
cha Kanumba na ramani ya eneo la tukio.
Lulu kwa upande wake, mawakili wake Peter Kibatala na Fulgence Massawe waliiarifu Mahakama kuwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kwenye utetezi watakuwa na mashahidi watano na vielelezo viwili. Hata hivyo hawakutaja majina ya mashahidi hao.Chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment