Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. PICHA/Maktaba |
Kiteto. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameagiza
wote waliovamia eneo la Hifadhi ya Jamii ya Emborey ya Murtangos,
kuondoka ili kuheshimu uamuzi wa mahakama ya rufani na akaagiza
waliohusika na mauaji ya watu 15 kusakwa.
Waziri Mkuu pia, ameagiza vijiji saba vinavyounda
hifadhi hiyo, kuunda kamati za kutafuta maridhiano, ambazo
zitashirikisha wakulima, wafugaji na wazee wa jadi ili kuhakikisha
hakutokei mapigano tena.
Tamko hilo la Pinda, limekuja siku chache, baada
ya kauli ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye amekuwa akiwatetea
wakulima waliovamia hifadhi hiyo, kushauri kuchukuliwa hatua, Mkuu wa
Wilaya hiyo, Martha Umbulla na watendaji wengine kwa kushindwa kudhibiti
mapigano.
Akizungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa
Serikali wa Mkoa wa Manyara na Dodoma, Pinda alisema, haiwezekani watu
kuvamia ardhi kama haina mwenyewe.
“Nimepita kwenye soko la mahindi Kibaigwa karibu
wote wanaeleza kulima Kiteto, sasa hakuna ambaye anazuia watu kutoka
eneo moja kwenda lingine kulima lakini lazima sheria zifuatwe,”alisema
Pinda.
Pinda alisema hakuna ardhi ambayo haina mwenyewe
na kimsingi mwenyewe mkubwa ni rais na kutoka kwake ndipo kuna ardhi ya
vijiji, hifadhi, misitu ama ardhi ya jumla.
Hata hivyo, wakazi wa Kiteto walionekana kupandwa
na munkari na kumweleza Pinda, kwamba viongozi wa wilaya na mkoa
hawawezi kuwasaka na kuwakamata wauaji.
Pinda, alijibu kelele hizo na kusema kuwa,
wataangalia jinsi ya kuboresha utaratibu huo na kwamba iwapo wataona
kuna haja ya kufanya hivyo, kuna majeshi mengine nchini ambayo yanaweza
kuifanya kazi hiyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo,
alisema mauaji yaliyotokea hivi karibuni yalitokana na wakulima
kutoridhika na kauli yake aliyoitoa katika mkutano wa Januari 9, mwaka
huu ya kuwataka kuondoka katika hifadhi hiyo kama utekelezaji wa hukumu
ya Mahakama ya Rufani.
Alisema baadhi ya wakulima waliopata nafasi ya
kuuliza maswali kwenye mkutano huo walisema hawataondoka kwa namna
yoyote katika hifadhi hiyo.
Wakati huohuo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kimemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwasimamisha kazi, Mkuu
wa Wilaya ya Kiteto pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri, wilayani humo.
Kama hiyo haitoshi, Chadema kimemtaka Pinda
kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi viongozi hao kwa madai ya
kushindwa kutatua mgogoro wa wakulima na wafugaji ambao umedumu kwa
miaka mingi . Chanzo: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment