Waziri Mkuu mstaafu na mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa akizungumza katika tafrija aliyoiandaa kwa wananchi wake na wageni mbalimbali ya kuukaribisha mwaka mpya 2014,iliyofanyika nyumbani kwake Ngarashi Monduli.Pembeni yake ni mkewe mama Regina Lowassa.
Monduli. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
ametangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake,
ambayo amesema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji
safi na maendeleo ya uhakika.
Akizungumza katika ibada ya shukrani na kuupokea
mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT),Usharika ya Monduli Mjini, Lowassa bila ya kutaja safari hiyo ni
ipi, aliwashukuru watu wote kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambao
walimsindikiza katika ibada hiyo.
Lowassa alisema anaamini watu hao waliofika, wana uhakika wa ushindi katika safari hiyo kwa kumtegemea Mungu.
“Nimefarijika sana leo kuwaona hapa marafiki zangu
wengi. Ninapowatazama hadi machozi yananitoka na kwa uwezo wa Mungu
tutashinda kwani nyote mnajua nia na ndoto yangu,’’ alisema Lowassa na
kupokelewa na sauti za shangwe kanisani.
Licha ya kutoweka bayana, Lowassa amekuwa akitajwa
kuwa ni mmoja wa wanasiasa wanaowania kumrithi Rais Jakaya Kikwete
baada ya kumaliza kipindi chake cha uongozi mwakani.
Azungumzia Katiba Mpya.
Akizungumzia Katiba Mpya, ambayo mchakato wake
sasa unaelekea katika Bunge Maalumu, licha ya kuipongeza Tume ya
Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba
alisema ana wasiwasi juu ya muundo wa Serikali Tatu.
“Nina wasiwasi na huu muundo, ni vyema viongozi wa
dini, kuliombea taifa tupate Katiba bora kwani maoni ya watu asilimia
40 ambao hawakutaka muundo wa Serikali Tatu lazima yatazamwe,” alisema
Lowassa.
Ibada katika Kanisa hilo, ambayo iliendana na
harambee ya kuchangia hosteli na zaidi ya Sh89 milioni kupatikana,
iliongozwa na Kaimu Askofu wa KKKT, Usharika wa Kaskazini Kati, Solomon
Masango.
Katika mahubiri yake, Kaimu Askofu Masango
alimtakia kila la heri Lowassa katika safari yake hiyo akisema
anamtambua kuwa ni kiongozi bora.
Hafla ya nyumbani
Akizungumza katika hafla aliyoandaa baadaye nyumbani kwake, Lowassa alirudia kauli yake ya kuanza safari.
Waliohudhuria halfa hiyo ni pamoja na wabunge wengi wakiwa wa
CCM, wenyeviti wa CCM, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM,
Mgana Msindai kutoka Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa UVCCM,
Manka Dilu kutoka Mkoa wa Mara na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Wanawake wa
CCM, Diana Chilolo pia kutoka Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa CCM Mkoa
wa Manyara, Lucas ole Mukusi ambaye ndiye katibu wa wenyeviti wote wa
CCM.
Wengine waliohudhuria ni wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya CCM (Nec), mikoa mbalimbali ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na
viongozi wa dini mbalimbali. Pia alikuwapo aliyekuwa mgombea urais wa
Kenya katika uchaguzi uliopita, Profesa James ole Kiapi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Lowassa alisema
ndoto ya elimu bure, ajira kwa vijana, kuondoa umaskini zitafanikiwa
baada ya kuanza safari yake hiyo hapo jana.
Alisema wakati ukifika wa kutangaza rasmi nia
hiyo, ataeleza mengi na akawataka wanaomuunga mkono wasiwe na shaka...
“WanaCCM msiwe na shaka, tutavuka kwa nguvu zetu... wingi wenu huu
unanipa faraja kuwa katika safari yetu na kwa kumtegemea Mungu
tutashinda.”
Lowassa aliwataka waungane na kaulimbiu yake,
‘Tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na tutashinda pamoja’ na baada
ya kusema maneno hayo, alipokewa kwa sauti za CCM... CCM... CCM.
Waalikwa wazungumza
Akizungumza katika hafla hiyo, Msindai ambaye
aliwaongoza wenzake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja na
Onesmo Nangole wa Mkoa wa Arusha alisema wanamuunga mkono, Lowassa
katika safari yake hiyo.
Alisema anamfahamu Lowassa kwa muda mrefu na
kumwelezea kwamba ni kiongozi bora mwenye uamuzi na kwamba haoni sababu
ya kutokumuunga mkono.
Mgeja alisema anawashangaa watu wachache ambao wameanza tabia ya kulazimisha watu kuwachagulia marafiki na kuwachafua wengine.
Alisema hakuna ambaye hafahamu kuwa Lowassa ndiye
tumaini la Watanzania akisema jina lake linatajwa kila kona kwa kuwa ana
uwezo na sababu za kuwa kiongozi wa Taifa.
Mgeja alionya kuwa kuna kundi la watu linalodhani
kuwa CCM ni mali ya viongozi kitu ambacho alisema si sahihi, bali ni
mali ya wanachama ambao alisema ndiyo wenye uamuzi.
Nangole alisema Lowassa ni kiongozi msikivu na makini ambaye ni tegemeo la Watanzania katika kuwaunganisha kuwa kitu kimoja.
Wakizungumza katika hafla hiyo, viongozi hao wa CCM, walisema wanamuunga mkono Lowassa kutokana na uwezo mkubwa alionao.
Manko kwa upande wake alisema UVCCM ina imani
kubwa na Lowassa kwani ni mmoja wa makada wa CCM wenye historia ndefu
katika chama hicho.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chemba Kondoa (CCM),
Juma Nkamia alisema Lowassa sasa ni sawa na Simba na kusema wanaomchukia
walie tu kwani ni kiongozi bora.
Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein Bashe
aliwataka wananchi wa Monduli kutunza heshima ya Lowassa na kwamba kazi
nyingine watafanya wao.
Alisema safari ya Lowassa ndiyo, imeanza
inawezekana na kwamba alipoanguka mwaka 2008, ilikuwa ni mipango ya
Mungu kuwezesha safari hiyo. “Lowassa ana sifa zote za uongozi...
tunachokiomba kwenu ni ushirikiano tu.”
No comments:
Post a Comment