Elimu : Jamii yatakiwa kutowaficha Watoto wenye ulemavu - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Tuesday, 6 October 2026

Elimu : Jamii yatakiwa kutowaficha Watoto wenye ulemavu

 



Na Mwandishi wetu, Arusha 



JAMII imetakiwa kutowaficha watoto wenye ulemavu ndani ya nyumba, badala yake wawapeleke shule ili wapate elimu na fursa ya kutimiza ndoto zao na baadaye kulitumikia taifa.


Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tengeru, Padre John Assey, wakati wa maafali ya 19 ya Tengeru Boys pamoja na maafali ya sita ya Shule ya Holy Ghost Viziwi Tengeru.


Padre Assey alisema watoto wenye ulemavu wana haki ya kupata elimu, kwa kuwa elimu itawasaidia kujenga maisha yao na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.


Alisema watoto wenye ulemavu wanapopewa elimu, hujengewa uwezo wa kujitegemea na baadaye wanaweza kurejea katika jamii na kulitumikia taifa kwa kutumia elimu na ujuzi walioupata.


Alifafanua kuwa asilimia kubwa ya watoto wenye ulemavu wana ndoto kubwa zinazohitaji kujengwa na kuendelezwa, hivyo jamii inapaswa kuwapa nafasi na mazingira yatakayowawezesha kuzifikia.


Padre Assey alisema wao kwa kushirikiana na Shirika la Roho Mtakatifu wameweza kuweka alama kubwa katika kuwapatia elimu watoto wenye ulemavu, hususan wenye ulemavu wa kusikia, ambapo wamekuwa wakipata elimu ya sekondari na kufanya vizuri.


Aliongeza kuwa katika maafali hayo, zaidi ya vijana 10 wenye ulemavu wameweza kuhitimu elimu ya kidato cha nne, huku wanafunzi zaidi ya 100 wasiokuwa na ulemavu wakihitimu.


Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Gaudensi Mtui, alisema wameendelea kuwalea wanafunzi katika misingi mizuri ya maadili ili waweze kuwa vijana wenye nidhamu na manufaa kwa jamii.


Mtui aliwataka wazazi kuendelea kuwaunga mkono watoto wao katika masomo, pamoja na kuhakikisha kuwa watoto wote, hasa wenye ulemavu, wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu.


Alisema ushirikiano wa wazazi, walimu na jamii ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata elimu na malezi bora yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao

No comments:

Post a Comment