Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akimtambulisha Mhe. Amina Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati wa pamoja Mkutano na Waandishi hao kuhusu pongezi za Serikali ya Kenya kwa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliyoitoa hivi karibuni kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika hotuba hiyo Mhe. Rais Kikwete alieleza msimamo wa Tanzania wa kutojitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). |
Waandishi kutoka Vyombo mbalimbali vya habari wakimsikiliza Mhe. Membe (hayupo pichani) |
Mhe. Mohammed akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari huku Mhe. Membe akisikiliza. |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. John haule (wa pili kulia) akimsikiliza Mhe. Mohammed (hayupo pichani) alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu pongezi za Serikali ya Kenya kwa Tanzania. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa,Balozi Celestine Mushy (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Vincent Kibwana (wa pili kushoto) na Mjumbe kutoka Kenya. |
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Dora Msechu (katikati), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Bw. Robert Kahendaguza (kushoto), Mjumbe kutoka Kenya na Bw. Mkumbwa Ally (mwenye koti jeusi), Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wakati wa Mkutano kati ya Mhe. Membe na Mhe. Mohammed na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) |
Mhe. Membe akiagana na Mhe. Mohammed mara baada ya kukutana na Waandishi wa Habari. |
Waandishi wa Habari kazini. |
-----------------------------------------------------------------
KENYA YAIPONGEZA TANZANIA KWA MSIMAMO WAKE KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
Serikali
ya Kenya imetoa pongezi nyingi na shukrani kwa hotuba iliyotolewa hivi
karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete kuhusu nafasi ya Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC).
Katika
hotuba yake kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
aliyoitoa tarehe 7 Novemba, 2013 mjini Dodoma, Mhe. Rais Kikwete alisema
kuwa Tanzania haina nia wala mpango wa kujitoa katika Jumuiya hiyo
pamoja na kwamba baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ikiwemo Kenya
wamekuwa wakifanya vikao pasipo kuishirikisha Tanzania.
Pongezi
za Kenya ambayo ni nchi ya kwanza kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kuipongeza Tanzania, ziliwasilishwa nchini na Waziri wa Mambo ya Nje wa
nchi hiyo, Mhe. Bibi Amina Mohammed ambaye aliwasili nchini tarehe 08
Novemba, 2013 kama Mjumbe Maalum wa Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri
ya Kenya.
Katika
mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari Mhe.Mohammed ambaye
alisindikizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa
Tanzania, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) alisema kuwa, Serikali ya Kenya
imeridhika na hotuba iliyotolewa na Mhe. Rais Kikwete na wameisoma kwa
makini na kuielewa kikamilifu na wanashukuru sana kwa hotuba hiyo kwani
ni faraja kubwa kwao kuwa Tanzania bado ni mwananchama hai wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
“Kenya
imefurahi na kuridhika na hotuba ya Mhe. Rais Kikwete kwani Tanzania na
Kenya zimetoka mbali pamoja. Pia ni waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, hivyo Kenya inaamini kuwa, tutaendelea kujenga Jumuiya hii
kwa pamoja na kuendelea kuwa majirani wazuri ili kukuza uchumi kwa
pamoja na kuwaletea maendeleo wananchi wa nchi zetu”, alisema Mhe.
Mohammed.
Mhe.
Mohammed aliongeza kuwa anawashukuru Watanzania kwa kumuunga mkono Mhe.
Rais Kikwete kwa hotuba yake na hiyo inaonyesha umoja uliopo hapa
nchini. “Tunawashukuru sana Watanzania kwa kumuunga mkono Rais Kikwete
na hii inadhihirisha umoja na mshikamano uliopo baina ya Watanzania na
Serikali yao,”aliongeza Bibi Mohammed.
Akizungumzia
vikao vinavyoendelea kati ya nchi tatu za Kenya, Uganda na Rwanda, Mhe.
Mohammed alifafanua kuwa, Tanzania haijatengwa na haiwezi kutengwa na
kwamba masuala yote yanayojadiliwa katika vikao hivyo hayako nje ya
Mkataba na Itifaki za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, Mhe. Mohammed alitumia pia fursa hiyo kuishukuru Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiunga
mkono nchi yake katika kesi inayowakabili Rais na Makamu wa Rais wan
chi hiyo huko Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC). Alieleza
kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazounga mkono kesi hiyo
iahirishwe hadi mwishoni mwa mwaka 2014 ili kutoa nafasi kwa Viongozi
hao kuwatumikia wananchi waliowachagua.
“Tunaishukuru sana Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiunga mkono Kenya katika suala linalowakabili viongozi wetu la kushitakiwa
ICC. Tumaamini kabisa kuwa hatuwezi kumaliza kesi hiyo wala kupata
kibali (deferral) cha kesi hiyo kusogezwa mbele bila kuungwa mkono na
nchi kama Tanzania” alisisitiza Mhe. Mohammed.
Awali
akimkaribisha Bibi Mohammed kuzungumza na Waandishi wa Habari, Mhe.
Membe alisema kuwa Serikali ya Tanzania imefurahishwa sana na ziara ya
Ujumbe huo mzito kutoka Kenya na Tanzania inazipokea kwa mikono miwili
pongezi hizo za Kenya kwa Rais Kikwete na kwa Watanzania kwa ujumla.
Kuhusu
suala la viongozi wa Kenya kupelekwa ICC, Mhe. Membe alisema kuwa,
Tanzania bado inaunga mkono maamuzi yaliyofikiwa na Nchi Wanachama wa
Umoja wa Afrika (AU) ya kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuahirisha kesi
hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuwapa nafasi Viongozi hao
kukamilisha baadhi ya mambo waliyojipangia kuyatekeleza kwa nchi yao.
“Tunashukuru
Mwendesha Mashitaka wa ICC ametoa tamko la dharura kwa kesi dhidi ya
Rais Kenyatta kuanza kusikilizwa tarehe 5 Februari, 2014 badala ya
tarehe 12 Desemba, 2013. Hata hivyo bado tunaiomba Jumuiya ya Kimataifa
kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusogeza mbele kesi hiyo
kwa mwaka mmoja hadi mwishoni mwa mwaka 2014 ili kutoa nafasi kwa
Viongozi hawa kuitumikia nchi yao kikamilifu kwani tunaamini katika
kipindi hicho Serikali ya Kenya itakamilisha mengi” alisisitiza Mhe. Membe.
Mhe.
Membe aliongeza kuwa, kulingana na kauli ya Mhe. Mohammed alipozungumza
nae, migogoro ya Kenya iliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007
imetatuliwa kwa asilimia 75, ambapo baadhi ya
wahusika wamepatiwa ardhi, watuhumiwa wamepelekwa mahakamani na baadhi
yao wamepewa fidia kutokana na madhara mbalimbali waliyoyapata.
“Tanzania ipo pamoja na Kenya na ipo kuhakikisha Serikali hiyo
inatawalika kwa kuwapa nafasi viongozi waliochaguliwa na wananchi
kuongoza”, alisema Mhe. Membe.
Mkutano
wa pamoja na Waandishi wa Habari kati ya Mhe. Membe na Mhe. Mohammed
ulifanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro jijini Dar es
Salaam na kuhudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John Haule na Maafisa Waandamizi kutoka
Serikali zote mbili.
No comments:
Post a Comment