TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI KATIKA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO 2013/14 - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Wednesday, 9 October 2013

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI KATIKA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO 2013/14

Mchumi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Bw. Andrea Aloyce(Kushoto) akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Mpango wa serikali wa kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kufikia asilimia 20 ya Pato la Taifa ifikapo June 2014 kutoka asilimia 18 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Ofisi hiyo Bi. Joyce Mkinga
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Bi. Joyce Mkinga(Kushoto) akieleza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wa mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2013/2014,wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo jijini Dar es Salaam.Kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari(MAELEZO) Bi. Fatma Salum.
Mtafiti Mkuu na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Bw. Leonard Mboera(kulia) akieleza kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu Mifumo mbalimbali ya utoaji taarifa za Tafiti zinazofanywa na Taasisi hiyo,wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Afisa Hbari wa Idara ya Habari(MAELEZO) Bw. Frank Mvungi.  
.....................................<<<<<<<<<<>>>>>>>>>...........................................
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS, TUME YA MIPANGO

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
USHIRIKI WA SEKTA BINAFSI KATIKA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO 2013/14

Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2013/14 ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16).
Mpango huu umeandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, ambavyo ni miundombinu, kilimo, viwanda, maendeleo ya rasilimali watu na uendelezaji wa huduma za utalii, biashara na fedha.

Mpango huu umejikita katika maeneo ya kipaumbele ya kimkakati ili kuleta matokeo ya haraka ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mwaka 2013/14 imegawanyika katika maeneo mawili;

i) Miradi ya kitaifa ya kimkakati ambayo ina matokeo ya haraka ya ukuaji uchumi, inayochochea maendeleo ya maeneo mengine na inayovutia uwekezaji wa sekta binafsi. (miundombinu, kilimo, viwanda, rasilimali watu na huduma za utalii, biashara na fedha)

ii) Miradi mingine muhimu kwa ukuaji uchumi; iliyo na matokeo ya haraka ya ukuaji uchumi na kijamii na kupunguza umaskini, yenye uhusiano wa moja kwa moja na sekta za ukuaji haraka wa uchumi na kufungulia fursa za ajira na uwekezaji.

Katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2013/14, Serikali kwa kutambua umuhimu na mchango wa sekta binafsi katika kuleta maendeleo ya kiuchumi katika jamii kupitia uwekezaji, imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kuvutia sekta binafsi kushiriki katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Katika Mpango huu Serikali imedhamiria kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kufikia asilimia 20.0 ya Pato la Taifa ifikapo Juni 2014 kutoka asilimia 18.0 mwaka 2012 ili kuwezesha sekta binafsi kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na kushiriki shughuli nyingine za kimaendeleo.

Hatua mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hatua hizo ni pamoja na uwepo wa Sera ya Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) na kukamilisha mwongozo wa kutekeleza Sera, Sheria na Kanuni za ubia baina ya Sekta ya Umma na sekta binafsi - PPP.

Mafanikio yaliyopatikana katika kuvutia sekta binafsi kuchangia katika ukuaji wa uchumi na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2012/13 ni pamoja na kusajiliwa miradi ya viwanda 186 ambapo kati ya hiyo miradi 157 ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) na 29 imesajiliwa na Mamlaka ya EPZ.

Katika eneo Maalum la Uwekezaji la Mabibo (BWM SEZ) jumla ya wawekezaji waliopewa leseni hadi kufikia Mei, 2013 ni Kampuni 18, kati ya hizo kampuni tano zimeanza uzalishaji ambazo ni Despec Africa Ltd (mwekezaji kutoka Dubai), DZ Card (T) Ltd. (Sweden/Thailand), Smart Export (T) Ltd. (Tanzania), Quality Pulse Ltd (India) na The Great Export (T) Ltd. (Tanzania). Aidha, kampuni saba zimeanza kufunga mashine kwa ajili ya kuanza uzalishaji katika mwaka 2013/14 na Kampuni sita zipo katika hatua za ujenzi.

Serikali iliendelea kuhamasisha uanzishaji wa viwanda katika maeneo mbalimbali nchini hususan Kanda ya Kusini ili kutumia rasilimali ya gesi asilia. Viwanda hivyo ni pamoja na Dangote Cement Co. Ltd kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni 3 za saruji kwa mwaka na kuajiri jumla ya wafanyakazi 5,000. Vifaa vya awali vya ujenzi wa kiwanda hicho vimewasili Mtwara. Aidha, kukamilika na kuanza uazalishaji kwa viwanda vya saruji vilivyopo mkoa wa Lindi ambavyo ni Lee Construction Materials Company Limited kilichopo Kilwa Masoko na kuanza kwa ujenzi wa kiwanda cha MEIS Cement Company kilichopo Lindi mjini.

Miradi mingine ya viwanda vya saruji ambayo ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi ni pamoja na Dar es Salaam Cement Company - Mbagala; Lake Cement Company, Dar es Salaam; Fortune Cement Company-Vikindu-Mkuranga; Athi River Cement Company - Tanga; Rhino Cement Company, Mkuranga- Pwani na Kisarawe Cement Company kilichopo Kisarawe mkoa wa Pwani.

Kwa upande wa miundombinu makampuni mbalimbali yameshirikiana na Serikali katika kuendeleza miundombinu hususan kwenye reli, bandari na nishati. Hali kadhalika, katika eneo la utoaji wa huduma sekta binafsi imechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza biashara, sekta ya fedha, utalii - ujenzi wa mahoteli, elimu – ujenzi wa shule na vyuo, afya-ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati.

Vile vile, sekta binafsi itachangia katika maendeleo ya kilimo kwa kujenga na kuendeleza miundombinu ikiwemo maghala ya kuhifadhia chakula na viwanda vya mbolea. Kampuni ya MARA LTD imeanza ujenzi wa ghala la kuhifadhia mbolea lenye uwezo wa kuhifadhi tani 45,000 kwa mara moja pembeni mwa bandari ya Dar es Salaam ambapo ujenzi wake unatarajia kukamilika Desemba 2013.

Kwa mwaka wa fedha 2013/14 Serikali imekadiria kutumia jumla ya shilingi trilioni 5.2 sawa na asilimia 31.09 ya bajeti yote kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kwa pamoja tutajenga nchi yetu!

Imetolewa na
Joyce Mkinga
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
09 Oktoba 2013

No comments:

Post a Comment