OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAFUNGUA OFISI 23 KATIKA MIKOA MBALIMBALI NCHINI - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


27 Sept 2013

OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAFUNGUA OFISI 23 KATIKA MIKOA MBALIMBALI NCHINI

 Afisa Habari, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Asiatu Msuya (kushoto) akieleza kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu ufunguaji wa ofisi 23 katika mikoa mbalimbali nchini ili kutekeleza  Mpango wa kutenganisha Upelelezi na uendeshaji wa  Mashtaka, wakati wa mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Wakili wa serikali Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Frederick Manyanda.
 Wakili wa serikali Mkuu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Frederick Manyanda (kulia) akieleza kwa waandishi wa (hawapo pichani) mkakati wa kuhakikisha kuwa huduma ya usimamizi na utoaji wa haki inawafikia wananchi wote kwa karibu kwa kufungua ofisi zaidi Mikoani, Katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam,katikati ni Afisa Habari toka ofisi hiyo Bi. Asiatu Msuya na Kulia kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Bi. Georgina MisamaPicha na Hassan Silayo-MAELEZO
---
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
Utangulizi
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanikiwa kufungua Ofisi 23 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro (Moshi), Arusha, Mwanza, Kagera (Bukoba) Mara (Musoma), Shinyanga, Tabora, Singida, Iringa, Mbeya, Mtwara, Lindi, Dodoma, Rukwa (Sumbawanga),Ruvuma (Songea), Njombe, Manyara,Morogoro,Kigoma,Geita  na Pwani. Aidha jumla ya Ofisi mbili (2) za zimefunguliwa katika Wilaya za Temeke na Monduli. Kwa mwaka wa fedha 2012/2013 pekee jumla ya Ofisi tano (5) zimefunguliwa katika mikoa ya Pwani, Kigoma, Morogoro, Manyara, Njombe na Geita ikiwemo pia Ofisi mbili za Wilaya. 

Lengo
Lengo kuanzishwa na kuimarishwa kwa Ofisi hizi za Mikoa na Wilaya ni kuhakikisha kuwa huduma ya usimamizi na utoaji wa haki inawafikia wananchi wote kwa karibu zaidi. Baadhi ya huduma zinazotolewa ni pamoja na kuendesha Mashtaka mahakamani, kushughulikia malalamiko na kero za wananchi kuhusiana na kesi za jinai na madai zinazowakabili, kutembelea mahabusu na kuratibu upelelezi wa kazi za upelelezi wa makosa ya jinai zinazofanywa na vyombo pelelezi/chunguzi ikiwemo Polisi, Magereza, Uhamiaji,TAKUKURU. 

Utekelezaji wa Mpango wa kutenganisha Upelelezi na Mashtaka nchini
Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kutekeleza mpango huu wa Utenganishwaji wa Upelelezi na Mashtaka kwa mujibu wa Sheria ambapo mfumo wa Sheria ambao uliwezesha kutungwa kwa Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, 2005 na Sheria ya Usimamizi wa Uendeshaji Mashtaka nchini, 2008 umeboreshwa; pamoja na kuanzishwa kwa Jukwaa la Ki-taifa la Haki-Jinai (National Criminal Justice Forum) Desemba 2009 linaloviunganisha pamoja vyombo vyote vinavyosimamia utolewaji wa Haki-Jinai nchini; 

Serikali pia imeboresha  Muundo wa Divisheni ya Mashtaka kwa kuweka Sehemu (Section) mahsusi inayosimamia utekelezaji wa mchakato wa utenganishaji wa kazi za upelelezi na Mashtaka na uratibu wa kazi za ki-pelelezi; pamoja na kuanzishwa kwa huduma ya Mashtaka ya moja kwa moja ambako Mawakili wa Serikali wanaendesha kesi;  Hii imepelekea idadi ya kesi zinazofunguliwa Mahakamani ambako Mawakili wa Serikali wanaendesha Mashtaka kupungua ikilinganishwa na kipindi cha nyuma; 
Kuongezeka kwa ubora wa huduma zitolewazo na kupungua kwa kesi za kubambikizwa.

Utekelezaji wa Programu ya Utenganishwaji wa Mashtaka na Upelelezi (Civilianization) imetoa msukumo mkubwa kwa Ofisi kuingia uanachama na makubaliano ya mashirikiano na vyama vinavyohusiana na kazi za Uendeshaji Mashtaka duniani, kama vile-IAP, HOPAC, APA, EAAP, na ARINSA; Serikali itaendelea kupanua wigo wa uendeshaji wa Mashtaka kwa kuanzisha na kuimarisha Ofisi katika Wilaya zote nchini pamoja na Mikoa miwili iliyobaki ya Katavi na Simiyu. 

Tunapenda kuwakumbusha Wadau wetu wote na Wananchi kwa ujumla kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa za uhalifu au jinai yoyote katika jamii kwa vyombo husika kupitia utaratibu unaofaa; na kutoa ushahidi Mahakamani pale unapohitajika kwa kuwa hizi  ni nguzo muhimu katika uendeshaji wa kesi mbalimbali. Aidha tunatoa wito kwa umma, wadau wetu na wananchi wote kwa ujumla pamoja na vyombo vya habari nchini kufuatilia mtiririko, hoja zinazowalishwa Mahakamani na uamuzi uliotolewa na Mahakama katika kesi mbalimbali zinazoendelea kuwa na taarifa sahihi ya kuhusu kesi hizo.

Imetolewa Na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ijumaa, Septemba 27, 2013

Kwa mawasiliano zaidi
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
SLP 9050
KIVUKONI FRONT
DAR ES SALAAM
SIMU: +255 22 21181778
NUKUSHI: +255 22 2113236
BARUA PEPE: info@agctz.go.tz 
TOVUTI:  www.agctz.go.tz

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad