HakiElimu Yasisitiza Serikali na Wananchi kuchukua hatua dhidi ya Elimu ya Tanzania - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 7 February 2013

HakiElimu Yasisitiza Serikali na Wananchi kuchukua hatua dhidi ya Elimu ya Tanzania

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (kulia)akizungumza kwenye mkutano huo na wanahabari.
Mkuu wa Kitengo cha Habari cha HakiElimu, Nyanda Shuli (Wa kwanza kulia) akizungumza
Mkutano wa HakiElimu na wahariri na waandishi wa habari.
Mmoja wa waandishi wa habari waandamizi kutoka Channel ten, Henry Mabung’o (wa pili kushoto) akichangia mada katika mkutano huo.

Na Joachim Mushi

IMEELEZWA kuwa hali ya elimu nchini kwa sasa si shwari hivyo ni wakati muafaka kwa wananchi na Serikali kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na hali hiyo. Changamoto hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo anuai vya habari kuzungumzia mustakabali wa elimu nchini. 

Alisema shule zetu zinapaswa kutoa elimu inayomwezesha mwanafunzi kujitambua na kumpa maarifa yatakayomsaidia kumudu mazingira yake jambo ambalo halifanyiki kwa sasa kutoka na sera hafifu. “Wakati tukijaribu kutafakari changamoto hizi katika sekta ya elimu ni muhimu tukajiuliza tumefikaje hapa tulipo?,” alisema.

“Matatizo ya mfumo mbovu wa elimu yamechangia kwa kiasi kikubwa na kutokuwa na dira ya elimu, ambayo inatolewa na sera kwa takribani miaka mitano sasa Serikali imekuwa ikiahidi kukamilisha na kupitia sera ya elimu ya mafunzo ya mwaka 1995. Watanzania wamekosa dira ya elimu waitakayo kwa sababu Serikali imeshindwa kukamilisha uandaaji wa sera mpya ya elimu,” alisema. 
 
Alisema Serikali imekuwa ikiandaa sera tangu mwaka 2007, lakini kwa sababu zisizojulikana imekuwa ikisuasua katika ukamilishaji sera hiyo mwaka hadi mwaka. “Sera ilianza kuandaliwa tangu mwaka 2007, Serikali kwa sababu zisizo julikana imebaki ikipiga danadana kila mwaka. Ni dhahiri kwamba kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini inahitajika sera mpya itakayotupa dira sahihi ya sura ya elimu tunayoitaka, pia kuandaa kutoelekeza mipango sahihi kuboresha mfumo wa elimu hapa nchini,” alisema Bi. Missokia.
 
Alisema kikwazo kingine ni migogoro sugu katika sekta ya elimu inachangia kudorora kwa elimu ya msingi na sekondari, kwani kwa kipindi kirefu sasa sekta ya elimu imegubikwa na migogoro mingi ikiwemo madeni ya walimu ambayo mgogoro wake umedumu kwa zaidi ya miaka minane.
Akizungumzia mvutano ulioibuka bungeni juu ya uwepo wa mitaala ya elimu ama kutokuwepo, Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa HakiElimu, Godfrey Bonivetura alisema taasisi hiyo haijawahi kuona mtaala wowote wa elimu licha ya wao kuomba mara kadhaa.

“Kwa mantiki hiyo sisi tunaamini mtaala haupo na kinachofanyika sasa walimu hutumia muktasari wa masomo kufundishia…mwaka jana tulifanya utafiti mmoja ambapo tulizungumza hadi na walimu nao walikuwa wakidai hata wao hawajawahi kuona mtaala,” alisema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Habari cha HakiElimu, Nyanda Shuli aliitaka Serikali kuwa wazi juu ya suala hilo na kama kweli inayo mitaala iiweke katika tovuti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili wananchi na wadau mbalimbali wa elimu waweze kuuona. “Ukiwauliza watendaji wa Serikali juu ya suala la mtaala wanasema upo ukiuomba uuone utapigwa danadana hadi unakata tamaa…,” alisema Nyanda.

Aidha aliiomba Serikali kuacha kuingiza siasa katika kushughulikia masuala ya elimu kwani hali hiyo ndiyo iliyoifikisha elimu yetu hivi sasa. Hivi karibuni ulizuka mjadala bungeni kuhusu kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mitalaa, sera na mihutasari ya elimu, hoja binafsi ambayo iliibuliwa na Mbunge wa Kuteuliwa NCCR-Mageuzi, James Mbatia akilitaka bunge kuunda Kamati kuchunguza suala hilo.

No comments:

Post a Comment