Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi,
akimfariji mmoja kati ya abiria waliokua katika Jahazi la Sun Rise, Juma Ali
Jaku , iliyopata ajali na kuzama kati ya Tanga na Mkokotoni karibu na Mkondo
wa Nungwi, ikiwa imebeba jumla ya abiria 32 kati ya hao 21 wameokolewa na 11
kati yao hadi sasa hawajapatikana. Kushoto kwa Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha
Suleiman Iddi na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Pemba Juma Khamis.
Nahodha na abiria mmoja ambao ni miongoni mwa watu 21 walionusurika kufa kati ya 32
waliokuwa wakisafiri na Jahazi lililopata ajali na kuzama liitwalo Sun Rise
likitokea Mkoani Tanga kuja Mkokotoni Unguja, wakiwa katika wodi ya Hospitali
ya Wilaya ya Kaskazini A iliyopo Kivunge, Zanzibar wakiendelea kupatiwa matibabu.
Jumla ya abiria 21 wameokolewa katika ajali hiyo na
kupelekwa Kivunge kwa ajili ya kupatiwa huduma ya matibabu ambapo hadi sasa
abiria saba watoto wakiwa watatu na watu wazima wane bado hawajapatikana kutokana na ajali hiyo.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pamoja na Viongozi wa Juu wa Ofisi
yake ambayo ndio inayoratibu masuala ya maafa walifika Hospitali ya Kivunge kuwapa
pole majeruhi hao waliobakiwa wakipatiwa huduma za Matibabu.
Nahodha wa Jahazi hiyo Bwana Abdulla Saleh akiwa pamoja na
Majeruhi mwenzake Bwana Ali Juma Jaku alimueleza Balozi Seif kwamba ajali hiyo
ilitokea kutokana na kuchafuka mara Moja hali ya Bahari.
Nahodha Abdulla alisema chombo chao chenye uwezo wa kubeba
abiria 50 kiliondoka bandarini Tanga salama Majira ya Saa nane za Usiku na walianza kupata mitihani na kuzama mara
baada ya kuchafuka kwa bahari majira ya saa 11 za alfajiri.
Akiwapa pole majeruhi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Maafa Zanzibar Balozi Seif
alisema juhudi alizoonyesha Nahodha huyo katika kusaidia uokozi huo zinastahiki
kupongeza na Jamii yote.
Balozi Seif
aliwaombea majeruhi hao kupoa haraka na kuungana na familia zao na kuutaka
Uongozi wa Hospitali ya Kivunge kuendelea kuwachunguza Mareruhi hao kutokana na
juhudi kubwa waliyoifanya ya kusaidia harakati za uokozi wa wenzao uliopelekea
kupoteza nguvu nyingi.
Jahazi hilo la Sun Rise lililokuwa likitokea Tanga kuja
Mkokotoni mbali ya kuchukuwa abiria pia lilibeba sanduku nne za maziwa pamoja
na Polo zipatazo 30 za Mkaa.
Othmna Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar
31/1/2013.
Source: Asili Yetu Tanzania
No comments:
Post a Comment