Kundi la wafanyakazi kutoka China waliotekwa nyara nchini Sudan, wameachiliwa huru na kusafirishwa hadi Kenya, maafisa kutoka nchi hizo mbili wanasema.
Wachina hao wanaofanya kazi za ujenzi waliachiliwa kwa kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu siku ya Jumanne, siku 11 baada ya kutekwa.
Walikuwa wakishikiliwa katika mpaka wenye mzozo wa Sudan katika jimbo la Kordofan ya Kusini.
Hali njema
Ndege ya shirika la Msalaba Mwekundu iliwasafirisha watu hao hadi jijini Nairobi, ambapo walipelekwa katika ubalozi wa Uchina, Sudan imesema.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Sudan al-Obeid Morawah ameiambia BBC kuwa kwa ufahamu wake Wachina 29 wamesafiri na ndege hiyo na wote walikuwa katika hali njema kiafya.
Ndege ya Msalaba Mwekundu ilisafiri kutoka kwenye uwanja mdogo wa ndege uliopo mji wa Kauda, Kordofan Kusini, alisema.
Wafanyakazi hao wa ujenzi wa barabara walitekwa nyara baada ya waasi kutoka kundi la SPLM-N kuvamia kambi yao Januari 28.
Uhusiano
Watu wengine 18 walikimbia katika shambulio hilo, ambapo 17 walipatikana wakiwa salama. Mtu mmoja aliuawa katika shambulio hilo, ambapo mwili wake ulipelekwa katika ubalozi wa Uchina mjini Khartoum.
Kundi la SPLM-N ambalo lilikuwa likipambana kwa kushirikiana na watawala wa sasa wa Sudan Kusini iliyo huru - limekuwa likipambana na majeshi ya serikali Kordofan Kusini kwa zaidi ya miezi sita.
Waandishi wa habari wanasema Uchina ndio mshirika mkuu wa serikali ya Sudan lakini tukio la utekaji nyara, ikiwa ni mara ya tatu kwa Wachina kutekwa tangu mwaka 2004, limeteteresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Tuhuma
Uchina inanunua mafuta mengi yanayozalishwa Sudan, na Sudan Kusini na ndio inayopeleka silaha kwa wingi zaidi Sudan.
Uchina inajaribu kusuluhisha mzozo mkali wa mafuta kati ya Sudan na Sudan Kusini. Sudan Kusini ndio inazalisha mafuta lakini mafuta hayo hulazimika kusafirishwa kupitia mabomba hadi Sudan kwa ajili ya kuuzwa nje.
Viongozi wapya wa Sudan Kusini wanakanusha tuhuma za Sudan kuwa wanaunga mkono kundi la SPLM-N.
No comments:
Post a Comment