Kenya, Tanzania, Rwanda zasonga mbele - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Wednesday, 16 November 2011

Kenya, Tanzania, Rwanda zasonga mbele

Stars
Harambee Stars imetoa kipigo

Kenya imefuzu kuingia katika ngazi ya makundi ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014 kwa kuizaba Ushelisheli 4-0 siku ya Jumanne.
Harambee Stars inasonga mbele kwa kupata mabao 7-0 ya jumla baada ya kupata ushindi wa 3-0 katika mchezo wa kwanza kwenye uwanja wa Nyayo jijini Nairobi.

Magoli ya Harambee Stars yamefungwa na Brian Mandela, Dennis Oliech, Titus Mulama na Victor Wanyama. Kenya sasa itapambana na Nigeria, Malawi na Namibia au Djibouti katika kundi F la kufuzu.
Stars
Taifa Stars imesonga mbele licha ya kuchapwa kwao
Tanzania nayo ilisonga mbele licha ya kufungwa wakiwa nyumbani 1-0 na Chad kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam siku ya Jumanne.
Taifa Stars walitarajiwa kupata ushindi mzito kutokana na kushinda 2-1 katika mchezo wa kwanza mjini N'Djamena siku ya Ijumaa.
Lakini Chad waliwashangaza Stars dakika tatu baada ya mapumziko wakati Muhamat Ahmat Labo alipowanyamazisha mashabiki wa Tanzania.
Hata hivyo Tanzania imeweza kusonga mbele kutokana na kanuni ya mabao ya ugenini kwa kuwa timu hizo zilikuwa na matokeo ya jumla ya 2-2.
Taifa Stars sasa ina mlima mkubwa wa kupanda katika ngazi ya makundi kwani inakabiliwa na Ivory Coast, Morocco na Gambia.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) iliendelea kutoa kisago kwa kuichapa Swaziland 5-1 mjini Kinshasa siku ya Jumanne na kujihakikishia nafasi katika ngazi ya makundi.
Mabao mawili kutoka kwa Mputu Mabi na mawili kutoka kwa Alain Kaluyituka na moja kutoka kwa Ilunga Diba yalizamisha jahazi la Swaziland. Wanasonga mbele kwa jumla ya magoli 8-2, baada ya kushinda 3-1 katika mchezo wa awali.
DRC itapambana na Cameroon, Libya na Togo katika kundi I la kufuzu.
Togo ilithibitisha nafasi yake katika kundi lao siku ya Jumanne baada ya kuifunga Guinea Bissau 1-0 mjini Lome.
Togo wanasonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1. Emmanuel Adebayor alicheza mechi yake ya kwanza katika kipindi cha miaka miwili baada ya kubadili uamuzi wake wa kutoichezea timu yake ya taifa.
Lesotho nayo ilifika katika ngazi ya makundi ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014 licha ya kupoteza mchezo wake dhidi ya Intamba Murugamba ya Burundi 2-1 mjini Bujumbura.
Lesotho wanasonga mbele kwa kanuni ya magoli ya ugenini, baada ya kushinda mchezo wa awali 1-0 siku ya Ijumaa.
Mamba hao wa Lesotho sasa watapambana na Ghana, Zambia na Sudan katika kundi D la kufuzu.
Rwanda nayo ilitinga katika ngazi za makundi chini ya kocha mpya Milutin Sredojevic baada ya kuizaba Eritrea 3-1 kwenye mchezo wa pili uliochezwa kwenye uwanja wa Amahoro mjini Kigali.
Rwanda inaingia katika ngazi ya makundi kwa jumla ya magoli 4-2 baada ya kutoka sare na Eritrea mjini Asmara siku ya Ijumaa.
Sredojevic ambaye aliongoza Rwanda katika mchezo wake wa pili kufuatia kutimuliwa kwa kocha Sellas Tetteh, alizawadiwa magoli hayo na Olivier Karekezi, Jean Claude Iranzi na Labama Kamana.
Goli la Abraham Tedros katika dakika ya 90 halikuweza kusaidia lolote kwa Eritrea.
Equatorial Guinea nayo ilisonga mbele katika mazingira kama hayo, baada ya kupoteza mchezo wake 2-1 dhidi ya Madagascar mjini Antananarivo.
Wenyeji hao wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2012 wamefuzu kwa kupata jumla ya mabao 3-2, kutokana na kushinda mchezo wa awali 2-0 siku ya Ijumaa.
Equatorial Guinea sasa itaungana na Tunisia, Cape Verde na Sierra Leone katika kundi B.
Kwa jumla Afrika itaandaa mechi 152 za kufuzu, ili kusaka timu tano ambazo zitacheza Kombe la Dunia 2014.
Timu hizo tano zitaiwakilisha Afrika katika fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa nchini Brazil kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1950.

No comments:

Post a Comment