Na Mwandishi Wetu,KAGERA
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,George Simbachawene amehimiza ushirikiano kati ya watumishi wa serikali waliopo katika Kituo cha Forodha cha Pamoja cha Mutukula kilichopo wilayani Misenyi mkoani Kagera ambapo ni mpaka kati ya nchi ya Tanzania na Uganda huku akiwaasa kutilia mkazo masuala ya usalama na ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya nchi ambapo uhitaji wa usalama na mapato ni muhimu ili nchi iweze kukua kiuchumi.
Ametoa rai hiyo wakati wa ziara ya ukaguzi wa shughuli mbalimbali za kiforodha katika kituo hicho akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Kagera ambapo awali alipowasili mkoani humo alipata ripoti ya hali ya ulinzi na usalama kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Hajjat Fatma Mwassa,ripoti iliyoonyesha kuwepo kwa sintofahamu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ikiwemo wingi wa vipenyo vinavyotumiwa na wahamiaji haramu na watu wanaoweza kuingia nchini kwa nia ovu ya kuvuruga amani iliyopo.
‘Kwanza ni usalama wa nchi yetu, kwahiyo kila mmoja aliyepo huku jambo namba moja ni usalama wa nchi yetu, lakini la pili ni ukusanyaji wa mapato,ili nchi iweze kuendelea inahitaji fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo imeahidiwa kwa wananchi na hiyo fedha ya kuendeleza miradi hiyo inapatikana kwenye maeneo ya ukusanyaji, moja kati ya maeneo muhimu ni mipakani, mpaka huu wa mutukula kati ya Tanzania na Uganda ni sehemu ambayo tunaamini makusanyo yakifanyika vizuri yatasaidia kutunisha mfuko wa serikali ili kuweza kufanikisha miradi inayohudumia wananchi zikiwemo huduma za afya,miundombinu kama Barabara,shule na kilimo.’ Alisema Simbachawene
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Mtukula, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Sarah Ngonyani amesema wanaendelea na huduma za kiuhamiaji ikiwemo kulinda mpaka huo sambamba na kukamata wahamiaji haramu wanaoingia nchini kupitia vipenyo mbalimbali vilivyopo katika vijiji vya Kanyigo na Minziro huku Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Edmund Lubinza akiweka wazi mapato wanayoingiza ambapo kwa mwezi wameingiza takribani bilioni 9 kwa mwezi.
‘Kuanzia Januari hadi Novemba,2025 jumla ya wageni 44,486 waliingia nchini na wageni 24,730 walitoka hali iliyopelekea ukusanyaji wad ola 158,680 kupitia malipo ya viza lakini pia tumekua tukitoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya uhamiaji haramu na mheshimiwa sisi uhamiaji kama unavyojua tuna kampeni maalumu ya ‘MJUE JIRANI YAKO’ ambayo tumekua tukiendelea nayo tukishirikiana na wananchi kutambua au kubaini wahamiaji haramu’ alisema Sarah
‘Katika kipindi cha Julai mpaka Novemba kituo kiliwekewa lengo la kukusanya bilioni 29 lakini kilifanikiwa kukusanya bilioni 27 ikiwa ni ufanisi wa asilimia 95% huku mafanikio hayo yakiwa yametokana na ushirikiano wa taasisi zilizopo hapa Kituoni Mutukula.’ Alisema Edmund.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA),Edmund Lubinza(kulia),wakati wa ziara katika ofisi za Kituo cha Forodha cha Pamoja cha Mutukula kilichopo wilayani Misenyi,mkoani Kagera ambapo ni mpaka kati ya Tanzania na Uganda.Kulia ni Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Mtukula,Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji,Sarah Ngonyani.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akikagua jinsi mfumo wa ukaguzi wa magari unavyofanya kazi katika Kituo cha Forodha cha Pamoja cha Mutukula kilichopo wilayani Misenyi,mkoani Kagera ambapo ni mpaka kati ya Tanzania na Uganda.Kulia ni Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Edmund Lubinza.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Edmund Lubinza (kulia), akitoa maelezo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene wakati wa ziara katika Ofisi za Kituo cha Forodha cha Pamoja cha Mutukula kilichopo wilayani Misenyi, mkoani Kagera ambapo ni mpaka kati ya Tanzania na Uganda.Watatu kulia ni Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Mtukula, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Sarah Ngonyani.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akipita katika mtambo wa ukaguzi wa magari uliopo katika Kituo cha Forodha cha Pamoja cha Mutukula kilichopo wilayani Misenyi,mkoani Kagera ambapo ni mpaka kati ya Tanzania na Uganda.Kushoto ni Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Mtukula,Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji,Sarah Ngonyani na kulia ni Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Edmund Lubinza. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Edmund Lubinza akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene wakati wa ziara katika Ofisi za Kituo cha Forodha cha Pamoja cha Mutukula kilichopo wilayani Misenyi, mkoani Kagera ambapo ni mpaka kati ya Tanzania na Uganda. Wapili kushoto ni Mfawidhi wa Kituo cha Uhamiaji Mtukula, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Sarah Ngonyani.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment