CHAN 2024 : Dar Kuzizima Ufunguzi wa CHAN24 - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Saturday, 19 July 2025

demo-image

CHAN 2024 : Dar Kuzizima Ufunguzi wa CHAN24

 

WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2022.17.01

WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2022.17.02%20(1)

Na Rahel Pallangyo

ARDHI ya Tanzania kwenye mji wenye pilikapilika, Dar es Salaam Agosti 2, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa utashuhudiwa ufunguzi wa fainali ya mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN 2024).

Dar es Salaam si tu kinara wa watu wake kujitafutia kipato, bali pia kuna mashabiki walevi wa soka ambao mioyo yao imejaa mapenzi ya dhati na hujitoa kwenda viwanjani kushuhudia wachezaji wao wakisakata kabumbu.

Tanzania inaamka, inajiandaa si kwa mchezo tu bali kwa ibada ya soka wakipiga kelele kila bao linapofungwa au kulia timu yao inapofungwa.

Chan ambayo itakafanyika Kenya, Uganda na Tanzania na kutoa mechi za kusisimua safari hii si viatu vya wachezaji pekee vitakavyotimua vumbi bali kuna mioyo ya mashabiki itakayokuwa inadunda kwa kasi wakishuihudia Taifa Stars ikifungua dimba na Burkina Fasso, Agosti 2 mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Hii ni mara ya tatu Tanzania kushiriki mashindano hayo baada ya kufanya hivyo mwaka 2009 na 2020 lakini ilitolewa katika hatua ya makundi. 

Awali fainali hizi zilikuwa zichezwe Februari Mosi hadi 28, mwaka huu lakini Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kusogeza mbele kutokana na ushauri wa wataalamu wa ufundi na miundombinu ambao baadhi yao wapo katika nchi za Kenya, Tanzania na Uganda, kushauri kuwa muda zaidi unatakiwa kuhakikisha miundombinu na vifaa viko katika viwango vinavyohitajika ili kuandaa michuano yenye mafanikio.

Chan imeshachezwa mara ya saba, itachezwa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu Rwanda wawe wenyeji 2016 na mataifa 19 yamepangwa katika makundi manne.

Fainali itachezwa Kenya ambao ndio wenyeji katika Kundi A na wamepangwa na washindi mara mbili Morocco na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na Angola na Zambia, katika kundi lililojaa mabingwa na timu bora.

Tanzania watakuwa wenyeji wa Kundi B na watamenyana na Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Uwanja wa New Amaan Complex Unguja utakuwa mwenyeji wa Kundi D ambalo lina bingwa mtetezi Senegal, Congo, Sudan na Nigeria.

Uganda ndio wenyeji katika Kundi C wakiwa na timu za Niger, Guinea, Afrika Kusini na Algeria.

Morocco na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kila moja imebeba kombe hilo mara mbili kabla, pamoja na Tunisia, Libya na mabingwa watetezi Senegal.

Mashindano hayo yanajumuisha wachezaji pekee wanaocheza ligi za nyumbani na ni jukwaa la kuonesha ubora wa vipaji vya nyumbani. Ni dhana ya kipekee kwa Afrika.

Makundi ya michuano ya Chan Kundi A: Kenya, Morocco, Angola, DRC, Zambia

Kundi B: Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati

Kundi C: Uganda, Niger, Guinea, Afrika Kusini na Algeria.

Kundi D: Senegal, Congo, Sudan, Nigeria

Kauli ya serikali

Serikali ya Tanzania imesema ipo tayari kwa asilimia 100 kwa ajili ya fainali Chan 2024.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ ndiye aliyetoa kauli hiyo baada ya kufanya ukaguzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao utatumika kwa mashindano na viwanja vya mazoezi Dar es Salaam jana.

“Kimsingi kwa asilimia 100 tupo tayari kwa ajili ya mashindano; kwenye upande wa miundombinu, ukienda Benjamin Mkapa, Gymkhana, Shule ya Sheria na pale Meja Jenerali Isamuhyo mtaona, naamini sisi Tanzania tutakuwa bora kwenye miundombinu ukilinganisha na nchi nyingine," alisema.


Kadhalika alisema, “Timu yetu kuweka kambi nchini Misri lengo ni kuwatenga wachezaji na kelele pamoja na kuwapa nafasi kuwasikiliza vizuri makocha lakini pia, fursa kwa ajili ya mechi nzuri za kirafiki na timu itakaa kule kwa siku kumi pekee baada ya hapo itarejea kujiandaa”.


Mchango wa Rais Samia 

Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa na mchango mkubwa katika michezo nchini huku ‘Goli la Mama’ likiongeza hamasa.

Kuanzia aanze kutoa pesa kwa kila goli linalofungwa kwenye mechi za kimataifa za timu za taifa na klabu wachezaji wameonesha juhudi kubwa na kurejesha imani kwa Watanzania.

Karia na bahati zake

Katika kipindi cha uongozi wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Wallace Karia ni mara ya tatu Taifa Stars ikifuzu Afcon na kuwa kiongozi mwenye mafanikio katika uongozi wake.

Kwa mwaka 2025 timu za Taifa zilizofuzu fainali za Afrika ni Taifa Stars katika fainali za Morocco, Twiga Stars ambayo imefuzu Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) yanayofanyika Morocco pia, Ngorongoro Heroes (U20) nayo imefuzu Afcon, U15 ya wanaume ni mabingwa watetezi wa mashindano ya shule Afrika.

Ukiachana na hizi pia katika kipindi cha Serengeti Girls ilifuzu fainali za Kombe la Dunia 2022 na kufika robo fainali, timu ya soka la ufukwe imefuzu fainali za mataifa ya Afrika mara tatu.

No comments:

Post a Comment

Tuwasiliane

Name

Email *

Message *

Contact Form

Name

Email *

Message *