Biashara : Benki ya NBC Yatoa Elimu ya Fedha kwa Wanafunzi, Walimu Shule ya Sekondari Pugu - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

27 Aug 2024

Biashara : Benki ya NBC Yatoa Elimu ya Fedha kwa Wanafunzi, Walimu Shule ya Sekondari Pugu

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa elimu ya fedha na umuhimu wa uwekaji akiba kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Pugu iliyopo Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.


Hatua hiyo inalenga kutoa fursa kwa wanafunzi hao kujifunza masuala ya kifedha ili kuwajengea utamaduni wa kujiwekea akiba, kubuni mawazo ya biashara sambamba na kutambua namna ya kutumia taasisi za kifedha ikiwemo benki hiyo ili kujinufaisha kiuchumi.

Semina fupi kuhusu mafunzo hayo ilifanyika mwishoni mwa wiki shuleni hapo ikiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki vigezo (Compliance) NBC Bi Sarah Laiser, alieambatana na viongozi wengine waandamizi wa benki hiyo akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya NBC, Bi Salama Mussa, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Mahesabu wa benki ya NBC Bw Fulgence Shiraji pamoja na maofisa wengine waandamizi. Wenyeji waliongozwa na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Boniface Orenda, baadhi ya walimu pamoja na wanafunzi.

Akizungumzia hatua hiyo Bi Laiser alisema ni muhimu kwa kuwa inalenga kuwajengea ufahamu na ujuzi wa kifedha vijana hao wakiwemo wale wanaotarajia kuhitimu elimu ya sekondari na kujiunga elimu ya juu na wale watakaojiri.

“Elimu ya fedha kwa wanafunzi ni muhimu kwa sababu inawawezesha kuelewa mapema jinsi ya kutunza na kuendesha fedha zao, kubuni na kufuata bajeti, na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.’’

“Zaidi, uwepo wetu hapa leo unalenga kuwasaidia wanafunzi hawa kutambua umuhimu wa akiba, uwekezaji, na matumizi sahihi ya mikopo. Tunaamini hawa ndio wajasiriamali, wawekezaji na maofisa wa kesho hivyo ni vema kuanza kuwaandaa mapema ili pia waweze kujua namna ya kutumia taasisi za fedha katika kujikwamua.’’

Wakiwa shuleni hapo maofisa wa benki hiyo walipata wasaa wa kutoa mafunzo na kuwasilisha mada mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, ujasiriamali pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi hao wakiwemo wale wenye mahitaji maalum kujibu na kujadili hoja mbalimbali kuhusu mada hizo.

“Pia tumepata fursa ya kutambulisha huduma zetu mahususi kwa wanafunzi na walimu zikiwemo akaunti za Mwanafunzi na akaunti ya Mwalimu zilizobuniwa kulingana na mahitaji ya makundi hayo. Pia tumetoa zawadi mbalimbali ikiwemo jezi za vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya NBC Premier League, mipira na zawadi binafsi zilikabidhiwa kwa uongozi wa shule pamoja na wanafunzi mbalimbali. ‘’ aliongeza.

Zaidi, maafisa hao, walishiriki zoezi la upandaji miti ya matunda na vivuli kwenye viunga vya shule hiyo ili kuacha kumbukumbu pamoja na kuunga mkono jitihada za shule hiyo pamoja na serikali katika utunzaji wa mazingira.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Orenda, pamoja na kuishukuru Benki ya NBC kwa hatua hiyo, alisema elimu hiyo itawasaidia wanafunzi hususani wale wanaotarajia kuhitimu kuwa na elimu ya kujiwekea akiba, kujijenga kijasiriamali hata pale watakaposhindwa kuendelea na elimu ya juu zaidi.

“Kimsingi ujio wa NBC shuleni hapa umekuwa na tija kubwa si tu kwa wanafunzi bali pia walimu kwa kuwa huduma zao zinatulenga pia walimu. Elimu hii imewanufaisha jumla ya wanafunzi 930 wanaosoma hapa ambapo 139 kati yao ni wenye mahitaji maalum. Tunashukuru mafunzo yamekuwa shirikishi kwa wanafunzi wa aina zote wakiwemo wenye mahitaji maalum na wote wameweza kujibu maswali kwa ufasaha na wamepata zawadi,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Mwalimu Orenda, umuhimu wa elimu ya fedha kwa wanafunzi hao unaokana zaidi pindi wanapohitimu elimu yao ambapo baadhi yao hujiingiza kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo biashara na hata wanaondelea na elimu ya juu, bado elimu ya fedha imekuwa ikiwasaidia katika kufanya maamuzi yanayohusu fedha wanazozipata ikiwemo mikopo ya elimu ya juu na pesa wanazotumiwa na wazazi pamoja na walezi wao wakiwa vyuoni.

Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki Vigezo (Compliance) wa Benki ya NBC Bi Sarah Laiser, (aliesimama) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Pugu ya jijini Dar es Salaam walioshiriki semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba iliyoendeshwa na benki hiyo shuleni hapo mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki Vigezo (Compliance) Benki ya NBC Bi Sarah Laiser, (kulia) na Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Mahesabu wa benki ya NBC Bw Fulgence Shiraji (kushoto) wakikabidhi mipira ya miguu kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Pugu, Mwalimu Boniface Orenda (Katikati) ikiwa ni moja ya zawadi zilizotolewa na benki hiyo kwa uongozi na wanafunzi wa shule hiyo wakati semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba iliyoendeshwa na benki hiyo shuleni hapo mwishoni mwa wiki.



Mkurugenzi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Mahesabu wa benki ya NBC Bw Fulgence Shiraji (wa pili kushoto) akipokea zawadi ya mchoro wa mkono wa nembo ya benki hiyo kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Pugu (wa pili kulia) wakati maofisa hao walipotembelea shule hiyo kwa ajili ya semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba iliyoendeshwa na benki hiyo shuleni hapo mwishoni mwa wiki. Wengine ni pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya NBC, Bi Salama Mussa (kushoto)


Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki Vigezo (Compliance) Benki ya NBC Bi Sarah Laiser, (aliepiga magoti) akipanda moja ya mti wa matunda kwenye viunga vya Shule ya Sekondari ya Wavulana Pugu iliyopo Manispaa Ilala jijini Dar es Salaam ikiwa ni kumbukumbu ya ziara ya maofisa hao shuleni hapo kwa ajili ya semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba kwa wanafunzi. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa Shule hiyo Boniface Orenda (alievaa suti) na maofisa wengine wa benki hiyo.



Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Pugu, Mwalimu Boniface Orenda (alievaa suti) akizungumza na maofisa waandamizi wa benki ya NBC wakati maofisa hao walipotembelea shule hiyo kwa ajili ya semina fupi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha na akiba iliyoendeshwa na benki hiyo shuleni hapo mwishoni mwa wiki.















Wakiwa shuleni hapo maofisa wa benki hiyo walipata wasaa wa kutoa mafunzo na kuwasilisha mada mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, ujasiriamali pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi hao wakiwemo wale wenye mahitaji maalum kujibu na kujadili hoja mbalimbali kuhusu mada hizo. 

No comments:

Post a Comment


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633