Na MWANDISHI WETU.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ametoa pongezi kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) baada ya
kuelezwa mafanikio mbalimbali ambayo NSSF imeyapata katika kipindi cha
miaka mitatu ya uongozi wake.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 13
Julai, 2024 wakati alipotembelea banda la NSSF kwenye kilele cha Wiki ya
Wazazi iliyofanyika Mjini Mpanda Mkoani Katavi. NSSF imeshiriki katika
kutoa elimu ya hifadhi ya jamii katika maadhimisho hayo kwani Jumuiya ya
Wazazi ni mojawapo ya wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (
NSSF).
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw.
Masha Mshomba, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, Bi. Lulu Mengele
amesema NSSF inamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa namna alivyofungua
nchi, ambapo wafanyakazi kwenye sekta binafsi wakiwemo wale wa viwandani
wameongezeka na kuiwezesha NSSF kupata wanachama wapya.
“Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunakupongeza kwa kazi kubwa unayoifanya,
umefungua fursa mbalimbali ambapo wakati unaingia madarakani mwaka 2021
thamani ya NSSF ilikuwa ni Shilingi Trilioni 4.8 lakini sasa imepanda
kwa juhudi kubwa ambazo umefanya tumefikia Trilioni 8.5,” amesema Bi.
Mengele.
Amesema NSSF inaendelea kuboresha mifumo yake ya TEHAMA
ambapo hivi sasa mwajiri anaweza kumwandikisha na kuwachangia
wafanyakazi wake kulekule walipo na pia mwanachama anaweza kuangalia
taarifa zake mbalimbali bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF
na kwa hatua hiyo imerahisisha huduma kwa wanachama.
Akizungumzia
ushiriki wa NSSF katika Kilele cha Wiki ya Wazazi, Bi. Lulu alimueleza
Mhe. Rais Dkt. Samia kuwa NSSF imeshiriki Maonesho yaliyoandaliwa na
Jumuiya ya Wazazi kwa kuwa wafanyakazi wa Jumuiya ya Wazazi ni wanachama
wa NSSF kama zilivyo Jumuiya nyingine za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bi.
Lulu amesema wametumia maonesho hayo kutoa elimu ya hifadhi ya jamii
kwa wanachama waliotembelea kwenye Banda hilo, matumizi ya mifumo kwa
waajiriwa na waajiri ambapo wakiwa popote wanaweza wakapata taarifa zao
za michango na kuwasilisha michango bila kulazimika kutembelea ofisi za
NSSF.
Amesema NSSF inaendelea kufanya vizuri kwa kuweka kipaumbele cha kuwarahishia huduma wanachama wake.
No comments:
Post a Comment