Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu Huria (OUT), kinaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka huu ambapo maadhimisho hayo kilele chake kitafanyika kwenye Mahafali ya 43 ya Chuo Novemba mwaka huu, Mkoani Kigoma.
Maadhimisho hayo yamekwenda na kauli mbiu isemayo, 'Miaka 30 ya kufungua fursa endelevu za elimu kwa njia ya masafa huria,'.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho hayo leo Julai 18, 2024 Jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa OUT, Prof. Elifas Bisanda amesema kauli mbiu hiyo inaendana na malengo makuu ya kuanzishwa chuo hicho na kuonyesha mchango wa Chuo katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
"Maadhimisho haya yatatumika kama jukwaa la kutathmini kiwango cha mafanikio ambayo Chuo kimeyafikia, kuuwezesha umma kutambua shughuli na mchango wa Chuo katika ujenzi na maendeleo ya Taifa."amesema.
Aidha Prof. Bisanda amesema katika kilele hicho, vituo vya Mikoa, Kurugenzi, Idara na wadau mbalimbali watashiriki kikamilifu katika kuandaa maonesho, mihadhara ya wazi na shughuli mbalimbali za maadhimisho.
"Licha ya mambo mengine katika siku hiyo, kutakuwa na wiki ya huduma ya Msaada wa Kisheria ambapo Wanasheria watatoa msaada wa kisheria, ushauri na elimu kwa wananchi," amesema Prof. Bisanda.
Pamoja na hayo amesema pia wataandaa makala ya miaka 30 ya chuo hicho itakayohusisha viongozi na watu mbalimbali ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Chuo hicho.
No comments:
Post a Comment