Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema pamoja na kuwa na faida nyingi na uhuru mkubwa katika matumizi ya mtandao, basi hakuna budi kuhakikisha uhuru huo unatumika vizuri ili kihakikisha jamii inabaki salama.
Waziri Nape ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Vyombo vya Habari mara baada ya kufungua Jukwaa la Uhuru wa Mtandao Barani Africa 2023 (FIFAfrica23) katika Hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam, Septemba 28, 2023.
“Sisi kama Nchi ni waumini wa uhuru wa mtandaoni na tumeweka kwenye Katiba yetu na tumeweka kwenye Sheria zetu lakini pamoja na kuwa na uhuru huo ni muhimu sana kuendelea kulinda tamaduni zetu, kuendelea kulinda watoto wetu, kuendelea kulilinda Bara letu la Afrika.” Amesema Waziri Nape
“Tuna utamaduni wetu kama Watanzania, tuna utamadunia wetu kama Bara la Afrika, pamoja na kutuunganisha na Dunia, pamoja na kuwa na uhuru mitandaoni, hatunabudi kuhakikisha uhuru huo unatumika vizuri ili kufanya jamii yetu inakuwa salama”. Amesema Waziri Nape
“Tumeona madhara yaliyotokea kwenye Nchi nyingi Duniani walipojiunganisha kwenye Mtandao wakapatwa na madhara kwenye amani yao, madhara kwenye tamaduni zao, sisi tungetamani bara la Afrika libaki salama. Tusiondoke kwenye mtandao na kila mtu ajiunge lakini tubaki salama.” Amesema Waziri Nape
Katika hatua nyingine Waziri Nape amesema kuwa kama Serikali ingetamani chaguzi zijazo zifanyike kwa njia ya mtandaoni pamoja na huduma mbalimbali zitolewe kwa jamii kwa njia ya Mtandao.
Jukwaa hilo lenye washiriki mbalimbali kutoka Barani Afrika litafanyika kwa muda wa Siku mbili na lina matarajio makubwa ya kutoka na njia mbalimbali za namna bora ya matumizi ya mtandao kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment