Nishati: TANESCO Yazindua Rasmi Mfumo wa Ni - KONEKT, Iringa. - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Wednesday, 15 June 2022

Nishati: TANESCO Yazindua Rasmi Mfumo wa Ni - KONEKT, Iringa.

Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga akiongea na wadau wa umeme pamoja na wafanyakazi wa shirika la TANESCO mkoa wa Iringa wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Nikonekt

Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga akishuhudia namna gani ambavyo mfumo wa Nikonekt unavyofanya kazi wakati wa uzinduzi wa mfumo wa Nikonekt mkoa wa Iringa.

 

 Na Fredy Mgunda,Iringa.

 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Iringa limezindua rasmi Mfumo rahisi wa maombi ya huduma ya Umeme kwa njia ya Mtandao ‘Kidigitali’ maarufu NI- KONEKT huku likiwaomba wananchi kuchangamkia fursa hiyo ambayo inamrahisishia mteja kupata huduma za umeme bila kufika katika ofisi za TANESCO.

 

Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi za TANESCO Mkoa wa Iringa na kuhudhuriwa pia na wateja wa TANESCO waliofika kupata huduma za umeme.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Ni – Konekt, Meneja wa TANESCO nyanda za juu kusini Mhandisi Satco Nombo alisema Mfumo wa Ni- Konekt unamuwezesha mteja kutuma na kufuatilia maombi ya umeme kwa njia ya kidigitali, kutoa taarifa za dharura, kufanya maombi yasiyo ya umeme kutoa malalamiko pamoja na kufanya maulizo mbalimbali.

 

“Kupitia mfumo huu wateja wetu watapata huduma ya umeme kwa urahisi na haraka huko waliko wakiwa wanaendelea na shughuli zao, kila kitu kitafanyika kwa njia ya digitali. Huduma hii inarahisisha sana kwa wafanyabiashara wanaohitaji huduma zetu. Pia itapunguza manung’uniko mbalimbali na mianya ya rushwa na vishoka..Ukiomba maombi SMS itakuja, hatua tutakazokuwa tunazifanya SMS itakuja kwa hiyo utakuwa unajua kila hatua inayoendelea”,alisema.

 

Mhandisi Nombo amesema ili mteja/mwombaji aweze kupata huduma ya maombi ya umeme kupitia mfumo wa Ni- konekt anapaswa kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA) huku akieleza kuwa Mfumo huo unatumia njia kuu tatu kufanya kazi yaani maombi kupitia Kiswaswadu (USSD Code), Tovuti (Web portal) na Programu tumishi (Nikonekt Mobile App).

 

 

Ameeleza kuwa mteja anaweza kutumia mfumo wa Nikonekt kwa kutumia njia ya Tovuti (Web portal) ya www.tanesco.co.tz ambapo mteja anaweza kutumia simu janja, komputa au kifaa kingine chenye uweo wa Intaneti.

 

 

“Njia zinazotumika kupata mfumo wa Ni- konekt ni pamoja na kutumia namba maalumu za USSD Code (Kiswaswadu) kwa kupiga namba *152*00# kwa watumiaji wa simu za kawaida. Bonyeza *152*00#, nenda namba 4 (Nishati) kisha nenda tena namba 4 (TANESCO) baada ya hapo nenda namba 1 (Maombi ya umeme) baada ya hapo utaulizwa unahitaji kwa matumizi ya nyumbani/biashara/taasisi…Kila hatua unayofanya utakuwa unapatiwa Ujumbe (SMS) kwenye simu yako”,amesema Mhandisi Mangara.

 

 

Amesema njia nyingine ya kutumia mfumo wa Ni- konekt ni kupitia Ni-konekt Mobile App ambapo mteja anaweza kupakua Programu ya Ni- konekt kwenye simu yenye uwezo wa Intaneti ambapo App ya Ni-Konekt inapatikana kwa watumiaji wote wa simu janja (Smartphone). Kwa watumiaji wa Android, Aplikesheni ya Nikonekt inapatikana kwenye Play store na App store kwa watumiaji wa Iphone.

 

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga alisema kuwa analipongeza shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kwa kazi nzuri wanayoifanya kutoa huduma ya umeme kwa wananchi.

 

Sendiga alisema kuwa uwepo wa umeme unasaidia kuchochea maendeleo kwa wananchi kwa kurahisisha shughuli mbalimbali ambazo mara nyingi zinahitaji nishati hiyo.

 

Alisema kuwa kuanzia mfumo wa Nikonekt utasaidia wananchi kupata huduma kwa haraka bila kutapeliwa na vishoka ambao awali walikuwa wanawatapeli wateja wa TANESCO.

 

Sendiga alisema kuwa mfumo huo mpya unaendana na mabadiliko ya teknolojia ya sasa hivyo wateja ambao wanahitaji kuunganishiwa umeme wanaweza kutuma maombi wakiwa nyumbani na kuokoa muda wa kwenda kwenye ofisi za shirika hilo.

 

Alimalizia kwa kusema kuwa mfumo huo unapunguza gharama za wananchi kutoka eneo moja kwenda ofisi za tanesco kwa ajili kuunganishwa umeme.

 

Nao baadhi ya wananchi wameipongeza TANESCO kuanzisha mfumo wa Ni – Konekt ambao amesema utawapunguzia wananchi muda na gharama za kufuata huduma za umeme katika ofisi za TANESCO

 

 

No comments:

Post a Comment