Matukio : Vijana Waaswa Kulinda na Kudumisha Muungano - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Monday, 23 April 2018

Matukio : Vijana Waaswa Kulinda na Kudumisha Muungano



Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma

Vijana Nchini wametakiwa kulinda na kudumisha Muungano kwa Vitendo kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho ikiwa ni sehemu ya kuonesha uzalendo.

Akizungumza wakati wa Kongamano lililofanyika mkoani Dodoma kuhusu Muungano lililowashirikisha wanafunzi zaidi ya 300 wa vyuo vya elimu ya juu mkoani Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba amesema kuwa vijana wanalo jukumu kubwa katika kulinda Muungano na kuudumisha.

“Vijana tunawategemea muwe watetezi na walinzi wa Muungano wetu kwa kuwa huu ni urithi wa Taifa tunawajibika kuulinda na kuudumisha kwa faida ya kizazi hiki na kijacho” Alisisitiza Makamba. Akifafanua Makamba amesema kuwa vijna wanaowajibu wakuonesha uzalendo wao kwa kudumisha Muungano ambao unalitambulisha taifa nje ya mipaka yetu.

Mambo mengine yanayolitambulisha Taifa letu ni Lugha, Mipaka yetu, Historia, Utamaduni wa kisiasa na kijamii.“ Waasisi wa Taifa letu walikuwa na dhamira njema ndio maana waliasisi Muungano wetu na kuweka mipaka mipya ya Taifa letu tofauti na ile ya wakoloni hivyo hili ni jambo la kujivunia” Alisisitiza Mhe. Makamba.

Aliongeza kuwa vijana wanapaswa kuwapuuza wale wote wanaobeza Muungano kwa kuwa hawalitakii mema taifa letu.Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe na Waziri (mstaafu) wa baraza la kwanza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Kwanza mara baada ya Uhuru Balozi Job Lusinde akizungumza katika mahojiano maalum mjini Dodoma amewaasa vijana kudumisha Muungano kwa kujifunza historia ya Muungano ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuuenzi.

“Vijana wajitahidi wawe waadilifu kwa kulinda uhuru wetu, umoja wetu na muungano wetu kwa faida ya kizazi hiki na kijacho” Alisisitiza Balozi Lusinde.

Akifafanua Balozi Lusinde amesema vijana wanapaswa kuepuka vitendo vya wizi na ufisadi ili kuchochea maendeleo.Mada zilizotolewa katika Kongamano hilo ni pamoja na Historia na faida za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mtazamo wa Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa.

Kongamano kuhusu Muungano limefanyika Mkoani Dodoma ikiwa ni siku chache kabla ya maadhimisho ya siku ya Muungano yanayotarajiwa kufanyika Aprili 26, 2018 mjini Dodoma, Kongamano hilo limewahusisha wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma, Mipango, CBE, St. John, Chuo cha Madini na Chuo cha Maendeleo Vijijini Hombolo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba

No comments:

Post a Comment