Matukio : Uchimbaji wa Mchanga kwenye Mito Dar Wapigwa Marufuku - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


21 Apr 2018

Matukio : Uchimbaji wa Mchanga kwenye Mito Dar Wapigwa Marufuku


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe Selemani Jafo (Mb) amepiga marufuku uchimbaji wa mchanga unaoendelea katika mito mbalimbali Jijini Dar es Salaam.



Mhe. Jafo ametoa katazo hilo wakati wa ziara yake ya kuangalia athari zilizotokana na mafuriko katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala leo 20 Aprili 2018. Akiwa katika kata ya Gongolamboto eneo la Ulongoni A na Ulongoni B, amejionea jinsi ambavyo mafuriko yaliyotokana na wingi wa mvua zilizonyesha yalivyoharibu madaraja na kuacha athari kubwa kwa wananchi.




“Nimejionea mwenyewe jinsi ambavyo mvua hizi zimeleta athari kubwa hapa na kusababisha mawasiliano kukatika baina yenu nyinyi na wenzenu wa upande wa pili. Lakini niwaambie kuwa kwa sehemu kubwa baadhi ya wananchi wanachangia uharibifu wa maeneo haya kutokana na uchimbaji wa mchanga unaoendelea na kusababisha uharibufu katika kingo za mito pamoja na miundombinu hii iliyojengwa,” alieleza Mhe. Jafo




Waziri ameeleza kuwa miundombinu inajengwa kwa gharama kubwa na Serikali lakini wapo watu ambao wanaiharibu kwa makusudi kutokana na uchimbaji wa mchanga, hivyo akaeleza kuwa Serikali haitavumilia swala hilo.“Hatuwezi kuzizuia mvua zisinyeshe lakini hatuwezi kuvumilia kuwaacha watu wanaoharibu miundombinu na kingo za mto kwa kuchimba mchanga. Hivyo kuanzia leo napiga marufuku uchimbaji wa mchanga katika maeneo yote ya mito ya Dar es Salaam,” ameagiza Waziri Jafo.




Amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sofia Mjema aliyeambatana naye katika ziara hiyo kusimamia agizo hilo pamoja Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla wake, na kuwakamata wale wote watakaokaidi agizo hilo.Aidha Mhe. Jafo ameeleza kuwa Serikali inajitahidi kurejesha mawasiliano katika maeneo hayo yaliyoathirika kwa kujenga madaraja ya muda wakati wakisubiri ukarabati mkubwa kufanyika.




Ameeleza kuwa amewasiliana na waziri wa Ulinzi Mhe. Hussein Mwinyi ili Jeshi la Ulinzi lisaidie katika kutengeneza madaraja hayo. “Waziri wa Ulinzi ameniahidi kuwa anatuma wataalamu wa Jeshi kufanya tathmini ya uharifu ili kutengeneza madaraja hayo ya muda,” amesema Jafo.Awali, katika ziara hiyo Mhe. Jafo ametembelea Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi “DART” katika kituo cha Jangwani na kuangalia athari zilizoltokana na mafuriko.




Akiwa katika kituo hicho cha Jangwani amepongeza uongozi wa UDART kwa kuzingatia agizo lake alilolitoa awali la kuyahamisha mabasi katika kituo hicho na kuyalaza Kimara pamoja na Gerezani hivyo kufanikiwa kuokoa mabasi hayo.“Mmeniambia kuwa yale mabasi niliyoyaona hapa wakati wa mafuriko ni yale ambayo yalikuwa hayatembei kabisa na hata hivyo mmetoa vifaa amabavyo vingeharibika katika mabasi hayo na mengine yote mliyatoa hapa. Nawapongeza kwa hilo,” ameeleza Jafo.




Mhe.Jafo amesema kuwa mafuriko hutoke duniani kote marekani, china na kwingineko na hatuwezi kuyazuia, lakini ni akasema kuwa ni lazima wadau na wananchi wote wazingatie tahadhari zinazotolewa ikiwa ni pamoja na kuhama mabondeni ili kupunguza athari.Pia ameeleza kuwa Serikali inampango mkubwa wa kuutengeneza Mto Msimbazi kupitia Mradi wa DMDP, ambapo takribani dola za kimarekani 20 milioni zimetengwa ili kupata suluhisho la kudumu. Alieleza kuwa kazi hiyo inatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2018 mara baada ya kumalizika kwa usanifu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo akiwa na viongozi wengine akiwemo Mkuu wa wilaya ya Ilala Sophia Mjema wakionyeshana maeneo ya daraja yalivyo haribika na mafuriko.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo akiwa na viongozi wengine katika ukaguzi wa athari za mvua.

Maeneo yaliyoharibiwa na Mvua

Maeneo yaliyoharibiwa na mvua

Maeneo yaliyoharibiwa na mvua

Maeneo yaliyoharibiwa na mvua


Athari za mafuriko

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad