Matukio : NIDA kuzindua Usajili wa Vitambulisho vya Taifa Kigoma, Rukwa na Katavi - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


8 Mar 2018

Matukio : NIDA kuzindua Usajili wa Vitambulisho vya Taifa Kigoma, Rukwa na Katavi


Kaimu Ofisa Uhusiano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Rose Joseph akielezea mikakati ya kuzindua usajili wa vitambulisho Kigoma, Rukwa na Katavi sambamba na ndani ya mgodi wa Tanzanite.


MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) inatarajia kuzindua usajili na utoaji wa vitambulisho hivyo katika mikoa mitatu ya Katavi, Kigoma na Rukwa.


Pia NIDA kwa kushirikiana na Wizara ya Madini , imeanza kuwasajili watu wote watakaoishi, kufanya kazi au biashara ndani ya eneo lililozungushiwa ukuta lenye madini ya TANZANITE huko Mererani mkoani Arusha.


Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, leo, Kaimu Ofisa Uhusiano wa NIDA, Rose Joseph, alisema mpaka sasa mamlaka hiyo imaendelea na usajili na utoaji vitambulisho vya uraia katika mikoa 20.


“Hivi karibuni tutafanya uzinduzi katika mikoa mitatu iliyobaki ambayo ni Kigoma, Rukwa na Katavi . Wananchi katika mikoa hii watakuwa na muda wa miezi mitatu wa kujisajili, na hivyo tutakuwa tumeifikia nchi nzima,”alisema Rose.Ofisa huyo alisema pia NIDA taangu Novemba mwaka uliopita ilianza usajili wa mkupuo katika mikoa mbalimbali na muda ulikuwa ukiongezwa kadri ilivyokuwa uinaruhusu.


“Tayari baadhi ya mikoa imemaliza kazi ya kusajili kwa mkupuo ikiwemo mikoa ya Mara na Iringa,”.alieleza Rose.Alisema katika kazi hiyo ya usajili NIDA kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji wanapeleka maofisa hadi ngazi ya kata na vijiji, ili kuhakikisha kazi hiyo inakwenda kwa mchujo sahihi na wale wote wanaosajiliwa wawe na sifa na vigezo kuwa raia wa Tanzania. “Tunasajili vitambulisho vya aina tatu ambavyo ni vya uraia, mkimbizi na mgeni na kumekuwa na ufanisi mkubwa,”alifafanua ofisa uhusiano huyo.


Alisema, pia NIDA kwa kushirikiana na Wizara ya Madini, imeanza usajili na kutoa vitambulisho kwa wafanyabiashara, wakazi na watu wote watakao kuwa wakiendesha shughuli zao ndani ya ukuta wa madini ya TANZANITE huko Mererani.“Kila mtu atasajiliwa na kupewa kitambulisho cha taifa. Hakuta kuwa na ruhusa ya mtu kuingia na kufanya shughuli yoyote ndani ya ukuta huo bila kuwa na kitambulisho hiki,”alibainisha Rose.


Alisema lengo ni kuona kuna kuwa na utaratibu maalumu wa kulitumia eneo hilo pamoja na kuwatambua wachimbaji wote wadogo na wakubwa na wafanyabishara wa madini katika eneo hilo.“Lengo ni kutambua watu wanaonufaika na shughuli zozote katika eneo hilo la madini. Tunataka kuona vijana wa Tanzania ndiyo wanufaika wakubwa , hivyo kutoa vitambulisho kutadhibiti wageni kuvamia eneo hilo,”alisema Rose.


Pamoja na hayo, Rose libainisha kuwa NIDA, kwa kushirikiana na wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA) kwa sasa wanaendelea na usajili na kuwapa vitambulisho vya uraia watu wote waliofungua makampuni kupitia wakala huo.“Utaratibu uliopo hivi sasa ni kwamba mtu yoyote ambaye hana kitambulisho taifa hawezi kupata usajili wa kampuni BRELA. Ni marufuku na wale ambao tayari walifungua wanatakiwa kufika BRELA kuchukua vitambulisho hivyo katika madawati yetu,”alifafanua ofisa huyo.


Aliongeza; “Changamoto kubwa tuliyonayo watanzania tunapenda njia za mkato, lakini katika kazi hii ni lazima tuwe wakweli , kwani kuwa na kitambulisho cha taifa kunakupa hadhi ya utanzania,”Alisema watu wengi wanataka kusajili kampuni kwa haraka hivyo kupita nijia za mkato kisha kukwama katika hatua za mwisho.


“Zoezi lingine ambalo NIDA tunalitekeleza ni la kuwasiliji wananchi wanaotaka Paspoti na hati za kusafiria za kielektroniki.Kwa sasa hupati hati hizo bila kuwa na kitambulisho cha taifa,”alisema Rose.Alisema kuna huduma za haraka zinazowawezesha wananchi wasio na vitambulisho hivyo wanaohitaji hati za kusafiria.


“Pia tunaendelea na usajili wa wanachama wa mifuko yote ya hifadhi ya jamii Tanzania ambapo kwa kushirikiana na Mamlaka Udhibitiwa Mifuko hiyo (SSRA), kusajili wanachama wote wa mifuko hiyo ambao hawana vitambulisho,’ alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad