Matukio : Moto Ulivyoteketeza Bweni la Wasichana Sekondari Korogwe - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


6 Mar 2018

Matukio : Moto Ulivyoteketeza Bweni la Wasichana Sekondari Korogwe


Na Yusuph Mussa, Korogwe


BWENI la Mapinduzi la wanafunzi wa kidato cha pili na nne katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe limeteketea kwa moto, huku mali zote za wanafunzi ikiwemo fedha zimeungua.


Moto huo ulioanza 3.15 usiku jana Machi 4, 2018, uliwakuta wanafunzi 43 wa bweni hilo wote wakiwa darasani (prepo), hivyo mali zao zote kuanzia vitanda 19 vya kulala wanafunzi wawili wawili na vitanda vitano vya kulala mtu mmoja vimeteketea kwa moto.


Akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela, Katibu Tawala wa Wilaya ya Korogwe Rehema Bwasi, alisema mali nyingine zilizoteketea ni magodoro 43, ambapo kati yao 26 ni ya shule na 17 ya wanafunzi. Pia vyandarua 43, shuka 86, blanketi 43, masanduku ya bati 43, mabegi 43 na fedha taslimu za wanafunzi mmoja mmoja sh. 336,500.


"Vitu vingine vilivyoungua ni pamoja na nguo za wanafunzi, miswaki, sabuni, vikombe, sahani pamoja na vitabu vya wanafunzi na vya shule. Ila tathmini inaendelea ili kuweza kujua hasara iliyotokana na moto huo" alisema.


Bwasi alisema kutokana na kadhia hiyo, baadhi ya wanafunzi walipata mshtuko, huku wengine wakiwa na magonjwa mbalimbali kama pumu na kifua, hivyo wanafunzi 41 walipelekwa Hospitali ya Wilaya na saba Zahanati ya Majengo.


"Baada ya muda, afya za wanafunzi 38 ziliimarika na waliruhusiwa kurudi shuleni. Mpaka saa mbili asubuhi ya leo Machi 5, 2018 wanafunzi 10 walikuwa bado wapo hospitali wakiendelea na matibabu, kati yao tisa wapo Hospitali ya Magunga na mmoja Zahanati ya Majengo" alisena Bwasi.


Mkuu wa Mko,a Shigela, alisema kwa haraka sana Serikali itatoa bati 400, godoro 150 na milioni sita kwa ajili ya kununua shuka na vitu vingine vidogo vidogo ili kuweza kurudi kwenye hali ya kawaida. Shigela amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Mary Chatanda na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, kwani waliweza kushirikiana na wananchi kuzima moto huo.


Naye Chatanda amelia na umeme akisema huenda ndiyo chanzo cha kuteketea bweni hilo, kwani umeme kwa sasa hivi ni changamoto kwa Wilaya ya Korogwe, unaweza kuwaka dakika moja na dakika nyingine ukazima.


Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Korogwe Inspekta Said Akilimali alisema wamechelewa kuzima moto huo kutokana na changamoto za maji na miundombinu ya kuyafikia mabweni.


"Moto huu ulioanza saa 3.15 tulijitahidi kufika mapema, lakini tumeshindwa kuzima moto kwa wakati kutokana na miundombinu ya barabara ya kuingia kwenye mabweni. Pia tulikosa ushirikiano na Idara ya Maji, hivyo badala ya maji tuchukue mjini, tukaenda Mtonga.


" Na chanzo cha moto huo huenda ni umeme, kwani muda huo umeme ulikuwa mdogo, halafu ukarudi ukiwa mwingi" alisema Akilmali. Meneja wa Mamlaka ya Maji Mji wa Korogwe (KUWSA) Sifaeli Masawa alisema hawakukataa kuwapa maji taasisi ya zimamoto, bali hawakwenda kwa utaratibu unaoeleweka kwenye eneo la maji.


"Wao hawakuwaeleza watu sahihi ili waweze kupata maji. Wamekwenda ofisi zetu za maji na kukuta walinzi ambao waliwakatalia kuingia, lakini kama wangewasiliana na mimi, ningetoa ruksa ya wao kuingia na kuchukua maji" alisema Masawa.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela(mwenye shati jeupe) akiangalia athari zilizosababishwa na moto ulioteketeza bweni katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Wilaya ya Korogwe. moto huo ulizuka usiku wa kuamkia leo, juu pichani akiwa ndani ya Bweni hilo linaloitwa Mapinduzi lililoteketea kwa moto. Kulia ni Mkuu wa Shule hiyo Anisia Mauka. (Picha zote na Yusuph Mussa)

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela Machi 5, 2018 alifika Wilaya ya Korogwe kuangalia athari za moto Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe. Pichani akimfariji mmoja wa wanafunzi waliopata mkasa wa kuunguliwa na bweni la shule hiyo. Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela leo Machi 5, 2018 alifika Wilaya ya Korogwe kuangalia athari za moto Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe. Pichani akimfariji mmoja wa wanafunzi waliopata mkasa wa kuunguliwa na bweni la shule hiyo. Kulia kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said.

Bweni la Mapinduzi la Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe ambalo limeteketea kabisa kwa moto jana usiku Machi 4, 2018. Bweni hilo walikuwa wanalala wanafunzi 43 wa kidato cha pili na nne.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad