NA TIGANYA VINCENT
19 MACHI 2018
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo imeamua kumsimamisha Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Kitete Dkt. Nassoro Kaponta ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa na wananchi dhidi ya Hospitali hiyo.
Maazimio hayo yalitolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri mara baada ya kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa Kitete.
Alisema Dkt Kaponta anasimamisha sio kama yeye katenda kosa bali ni katika uwajibikaji ili kupitisha Kamati Maalumu ya Kuchunguza Kitaalamu (Therapeautic Committee) kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa na wananchi kuhusu mwenendo wa wa Watumishi wa Hospitali hiyo ambaye yeye alikuwa akiisimamia.
Mwanri alitaja baadhi ya tuhuma ni pamoja na lugha chafu kutoka kwa baadhi ya Wauuguzi wanazitoa kwa wakimama wajawazito wanapokwenda kupatiwa huduma ya kujifungua, wagonjwa kudaiwa rushwa na baadhi ya wafanyakazi na vifo wa wakinamama vinavyotokana na uzembe.
Alisema pamoja na Kamati hiyo kuchunguza mambo ya Kitaaluma pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) Mkoani Tabora imepewa jukumu la kuchunguza tuhuma zinazotolewa na wananchi wanaoenda kutibiwa pale za rushwa na lugha chafu.
“Ndugu zangu nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi Ofisini kwangu kuhusu Hospitali yetu ya Mkoa kuhusu lugha chafu ambazo nyingine ziwezi kuzisema hapa, rushwa , uchafu na vifo… hivyo tumekaa mimi na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wafanyakazi wa Hospitali ya Rufaa ya Kitete na tumeamua kumweka pembeni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ili kupisha uchunguzi” alisema Mkuu huyo wa Mkoa
Mwanri alisema wakati kazi hiyo ikiendelea Dkt. Kevin Nyakimori atakaimu Uganga Mfawidhi katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora Kitete hadi majibu ya uchunguzi yatakapotelewa na Wizara ya Afya kutoa maamuzi kufuatia taarifa itakayotolewa.Aidha aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Mamlaka husika pindi wanapobaini kutotendewa haki katika eneo lolote wanapoenda kupata huduma ya tiba.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema hatasita kumchukulia hatua Mtumishi yoyote wa kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali atakayewatoza malipo Wajawazito, Watoto waliochini ya miaka mitano na wazee ambao imeagizwa wapate matibabu bila malipo.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Gunini Kamba alisema baadhi ya malalamiko ambayo yalifikishwa katika Ofisi yake ni pamoja na kifo cha Mfanyakazi wa Hazina ndogo Tabora baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na utumbo kujikunja na kile kilichomhusu Mama Mjamzito aliyekuwa na upungufu wa Damu.
No comments:
Post a Comment