Na Hamza Temba, Arusha
..............................................................
Wadau wa Utalii Jijini Arusha wamempongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kwa kukubali kuyafanyia kazi mapendekezo yao ya kuwaingiza wajasiriamali wadogo katika utoaji wa huduma za kusafirisha watalii nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo wakati akichangia mapendekezo ya viwango vipya vya leseni za biashara ya utalii zilizowasilishwa kwao na Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Jijini humo.
Chambulo alisema kwa muda mrefu sasa kanuni zinazotumika zinamtaka mfanyabiashara ya usafirishaji watalii awe na magari matatu kwa kiwango cha chini ikiwa ni pamoja na kulipia ada ya leseni ya Dola za Kimarekani 2,000 sawa na wafanyabiashara wengine matajiri jambo ambalo limekuwa likiwabagua wafanyabiashara wadogo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akizungumza na wadau wa utalii Jijini Arusha jana ambapo Wizara yake iliwasilisha mapendekezo ya viwango vipya vya leseni za biashara ya utalii na tozo ya ada za malazi katika viwango vya ubora wa nyota. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Aloyce Nzuki.
“Tunakupongeza sana Mhe. Waziri kwa kutupa angalao hilo moja, tuliomba mwenye kagari kamoja nae aruhusiwe na apewe leseni walau ya dola 200 ili afanye biashara kidogo kidogo mwishowe atanunua gari tano na kuendelea, tunataka sisi Watanzania wote tufaidike na rasilimali zetu,” alisema Chambulo.
Awali akiwasilisha mapendekezo ya viwango hivyo vipya vya leseni ya biashara ya utalii, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Deogratias Mdamu alisema kwa upande wa watanzania ambao ni wajasiriamali wadogo wenye gari moja hadi magari matatu watatakiwa kulipa ada ya leseni ya dola za Kimarekani 200.
Kwa upande wa wafanyabiashara wenye magari kuanzia manne hadi kumi alisema imependekezwa walipe Dola za Kimarekani 2,000, wenye magari 11 hadi 50 Dola za Kimarekani 3,000, magari 51 hadi 100 Dola za Kimarekani 10,000 na magari 100 na kuendelea Dola za Kimarekani 15,000.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa utalii Jijini Arusha jana ambapo Wizara yake iliwasilisha mapendekezo ya viwango vipya vya leseni za biashara ya utalii na tozo ya ada za malazi katika viwango vya ubora wa nyota. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Aloyce Nzuki na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Deogratias Mdamu (kushoto).
Kwa upande wa wafanyabiashara ambao sio Watanzania wenye magari 10 hadi 30 imependekezwa walipe Dola za Kimarekani 10,000, magari 31 hadi 100 Dola za Kimarekani 15,000 na magari 101 na kuendelea Dola za Kimarekani 20,000.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alisema lengo la kuwasilishwa kwa mapendekezo hayo ya viwango hivyo vipya vya leseni ya biashara ya utalii kwa wadau ni kuweka ushirikishwaji na makubaliano ya pamoja ya kutekeleza kanuni hizo.
Alisema sehemu kubwa ya mapendekezo hayo imezingatia maombi na maoni ya wadau hao ambayo yaliwasilishwa kwake awali. “Kilio chenu nimekisikia mimi mwenye mamlaka ya kufanya mabadiliko, lengo kubwa la mapendekezo haya ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo wenye gari moja waweze kuingia kwenye biashara hii ya utalii pamoja na kuongeza mapato ya Serikali na jamii kwa ujumla,” alisema Dk. Kigwangalla.
Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo akichangia mapendekezo ya viwango vipya vya leseni za biashara ya utalii zilizowasilishwa kwao na Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii katika mkutano huo.
Katika hatua nyingine amewaagiza watalaamu ndani ya Wizara yake kuhakikisha wanakamilisha kanuni hizo mpya ndani ya mwa mwaka huu ili utekelezaji wake uanze mapema mwakani, 2018.
Akizungumzia wafanyabiashara wanaofanya biashara ya kuwasafirisha watalii nyuma ya pazia bila kulipia leseni, alisema Wizara yake inaandaa mfumo maalumu wa kielektroniki utakaowezesha ukaguzi wa magari kwenye mageti ya kuingilia hifadhini ili kudhibiti vitendo hivyo.
Aidha, ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara hao na kuwataka kufanya biashara hiyo kwa weledi na kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwemo kulipa ada ya leseni husika kwa mujibu wa sheria.
Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo wakiwa kwenye mkutano huo.
Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo wakiwa kwenye mkutano huo.
Baadhi ya wadau wa Utalii walioshiriki mkutano huo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) akitambulishwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Aloyce Nzuki (kushoto) kwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini yaChama cha Waongoza Watalii Tanzania (TATO), Merywn Nunes muda mfupi baada ya kikao na wadau wa utalii Jijini Arusha jana ambapo Wizara yake iliwasilisha mapendekezo ya viwango vipya vya leseni za biashara ya utalii na tozo ya ada za malazi katika viwango vya ubora wa nyota.
No comments:
Post a Comment