Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mbulu
Watanzania wametakiwa kuenzi mila na desturi ambazo ni chanya wazitunze na kuzitumia ili kujenga jamii yenye maadili mema nchini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura alipotembelea Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) Haydom wilaya Mbulu mkoani Manyara ambapo amejionea utajiri wa kiutamaduni wenye fursa za utalii wa kiutamaduni.
“Nimetembelea nyumba za asili zilizopo hapa katika kituo hiki nimefurahishwa sana na utajiri wa kiutamaduni uliopo hapa, wazee walizingatia maadili katika kuwalea watoto wao kulingana na mila na desturi zao, ni vema tuenzi utamaduni wetu, huo ni msingi wa maadili mema ya jamii” alisema Naibu Waziri Wambura
Akitolea mfano wa maadili mema yanayopaswa kurithishwa aliyojionea katika kituo cha 4CCP na namna ambavyo watoto waliheshimu nyumba za wazazi wao, Naibu Waziri Wambura amesema kuwa kwa mujibu wa mila na desturi za Kitanzani suala la ulevi na utumiaji wa tumbaku kwa vijana ilikuwa ni mwiko hadi kijana afikie umri wa utu uzima ambapo anaweza kuwa na maamuzi sahihi katika maisha yake yenye kuwa na tija kwa familia.
“Kabla ya kuoa kijana alikuwa haruhusiwi kutumia tumbaku na kunywa pombe, bali kijana akioa na kuwa na watoto wawili kwa mujibu wa mila za makabila ya yaliyopo Mbulu aliruhusiwa kuingia katika kundi la watu wazima na kuruhusiwa kutumia vitu mbalimbali ikiwemo tumbaku na kinywaji cha pombe. Hapa kuna jambo la Watanzania kujifunza na kutunza ili kuondokana na mmomonyoko wa maadili” alisema Naibu Waziri Wambura.
Mila za jamii zilizo njema zinapaswa kutunzwa na kuendelezwa ili ziweze kusaidia vijana na jamii kwa ujumla kuweka mawazo yao katika shughuli za maendeleo pamoja na kupatia familia zao mahitaji ya kila siku.
Naibu Waziri Wambura alisisitiza kuwa mila hizo hazitakiwi kuachwa bali zainatakiwa kuenziwa, kutunzwa, kuendelezwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya sasa ziweze kuchangia katika kukuza utalii wa kiutamaduni ambao ni moja ya vyanzo vya mapato kwa wanajamii na taifa kwa ujumla.
Aidha, Naibu Waziri Wambura alisema kuwa wilaya ya Mbulu ni tajiri katika masuala ya utamaduni na kuongeza kuwa wilaya hiyo ni mdau muhimu katika sekta ya michezo na utamaduni ambazo zinapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay amesema kuwa wilaya hiyo imekuwa na utamaduni wa kufanya tamasha la utamaduni kila mwaka ambapo mwaka huu lilifanyika tarehe 21 hadi 23 mwezi Septemba na inaedelea kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo hatua inayopelekea makabila yote kuwa mstari wa mbele katika kudumisha amani ya nchi.
Mbunge huyo aliyataja makabila yanayotokana na makundi makuu manne yanayopatikana wilaya ya Mbulu kuwa ni pamoja na Wairaqw ambao ni jamii ya Wakushi, Wahadzabe jamii ya Khoisan, Wanyiramba na Wanyisanzu jamii ya wabantu na Wadatooga jamii ya Kiniloti.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mbulu Chelestino Mofuga amemhakikishia Naibu Waziri Wambura kuwa wilaya hiyo itaendelea kuenzi sekta ya utamaduni kwa kuwa na tamasha la utamaduni linalokutanisha makabila yote wilyani humo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uanuwai wa Utamaduni duniani ambayo hufanyika mwezi Mei tarehe 21 kila mwaka.
Hatua hiyo inatokana na Tanzania kusaini mkataba wa azimio la Umoja wa Mataifa (UN) kuenzi utamaduni na kuheshimu tamaduni za watu wengine chini unaosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Mwaka 2002 Umoja wa Mataifa uliamua kuanzisha maadhimisho ya siku ya Utamaduni Duniani kutokana na kuongezeka kwa migogoro, mapigano na kupotea kwa maisha ya watu na mali zao iliyokuwa inatokea sehemu mbalimbali duniani mwishoni mwa miaka ya 1990.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura (wa pili kushoto) akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Ulinzi na Usalama mara baada ya kuwasili Wilayani Mbulu kwa ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu Chelestino Mofuga akimkaribisha Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura kuongea na wananchi waliokuwa katika tamasha la utamaduni katika Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) Haydom mara baada ya kuwasili Wilayani humo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo.
Baadhi ya Washiriki wa tamasha la utamaduni katika Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) Haydom, wilaya ya Mbullu wakimsikiliza Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura (hayupo pichani) alipotembelea kituo hicho.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura akitoka ndani kujionea moja ya nyumba za asili ya Wabantu Wanyiramba na Wanyisanzu iliyopo Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) kilichopo Haydom.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura akicheza ngoma na washiriki wa tamasha la utamaduni alipotembelea Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) kilichopo Haydom.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura (wa pili kulia) akipata maelezo ya utamaduni wa kabila la Wadatoga katika Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) kilichopo Haydom.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wasichana wa kabila la Datoga na kusisitiza Watanzania kuenzi utamaduni wetu kwa kuurithisha kwa vijana wetu. Wa nne kushoto ni Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay.(Picha na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mbulu)
No comments:
Post a Comment