Uchumi : Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Atembelea kiwanda cha Uzalishaji Sukari Nchini Cuba - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Saturday, 26 August 2017

Uchumi : Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Atembelea kiwanda cha Uzalishaji Sukari Nchini Cuba


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Viwanda vya Sukari nchini Cuba, Bw. Francisco Lled, ambaye amekubali kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.


Shirika la Sukari la nchini Cuba linauwezo wa kuzalisha tani milioni nne za sukati kwa mwaka huku mahitaji ya ndani ni tani 700,000, ambapo kiasi kinachobaki huuzwa nje ya nchi. Kwa sasa shirika hilo linazalisha tani milioni mbili tu katika viwanda vyake 56.


Waziri Mkuu alikutana na Bw. Lled (Alhamisi, Agosti 24, 2017), wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha sukari cha UGB Central Azucarero 30 de Noviembre katika mji wa San Nicola’s de Bari ambacho ni kati ya viwanda 27 vya shirika hilo linalomilikiwa na Serikali ya Cuba kwa asilimia 100.


Katika mazungumzo yao Waziri Mkuu alimshawishi Bw. Lled kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha sukari. Alisema kwa sasa Tanzania kuna viwanda vikubwa vitano vya sukari ambavyo uzalishaji wake hautoshelezi mahitaji ya ndani.


Waziri Mkuu alivitaja viwanda hivyo ambavyo ni Mtibwa na Kilombero (Morogoro), Mahonda (Zanzibar), TPC (Kilimanjaro) na Kagera ambavyo vyote vinazalisha jumla ya tani 320,000 za sukari kwa mwaka huku mahitaji yakiwa ni zaidi ya tani 400,000.


Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inatarajia kujenga viwanda vitatu vya kuzalisha sukari, ambavyo vitazalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na ndani ya nchi na kiasi kitakachosalia kitauzwa nje.


Kwa upande wake Bw. Lled alisema sera za Cuba haziruhusu shirika kwenda kuwekeza nje ya nchi na badala yake wanaruhusiwa kuzisaidia nchi zinazohitaji kujenga viwanda hivyo kwa kutoa ushauri na usimamizi wa ujenzi wa miradi hiyo.


Alisema Shirika lake lipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika usimamizi na kutoa ushauri wa ujenzi wa miradi ya viwanda vya kuzalisha sukari na kwamba walishatoa huduma kama hiyo katika nchi mbalimbali zikiwemo Brazil na Bolivia.


Katika hatua nyingine, Bw. Lled alisema mbali na uzalishaji sukari pia shirika hilo kupitia viwanda vyake vya sukari wanazalisha vyakula vya mifugo, asali ambayo inatumika katika viwanda vya kutengeneza vinywaji vikali pamoja nishati ya umeme.


Alisema miwa ya kuzalishia sukari katika viwanda vyao wanaipata kutoka kwenye vikundi vya ushirika wa kulima wa miwa vilivyoko katika mikoa yote nchi nzima kasoro mkoa wa Havana na Pañar del Rio na kwa mkulima mmoja mmoja ambao kwa pamoja hukusanya miwa katika vituo ambavyo hupeleka kiwandani.


Hata hivyo alisema kuwa viwanda vyao vinanunua miwa kwa bei tofauti kulingana na ubora wa miwa na kwamba shirika lao linawasaidia wakulima kwa kuwaelimisha namna bora ya kulima pamoja na kuwaazima mashine za kuvunia wakati wa mavuno. Miwa yote nchini Cuba inavunwa kwa kutumia mashine.


IMETOLEWA NA:


OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 25, 2017.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo ya ukarabati wa kiwanda cha Sukari cha UGB kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari nchini Cuba Bwana Francisco Martin, August 24/2017 kiwanda hicho kipo katika Mji wa San Nicola's de Bari nchini Cuba
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia shehena ya sukari iliyozalishwa katika kiwanda cha UGB Central Azucarero 30 Noviembre wakati alipotembelea kiwanda hicho August 24/2017 kilichopo katika mji wa San Nicola's de Bari nchini Cuba

No comments:

Post a Comment