Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga akimkabidhi msaada wa vifaa vya maabara, stuli za kukaliwa wanafunzi wakati wa mazoezi kwa vitendo kwa aliyekuwa mkuu wa shule ya sekondari Kishapu ambaye sasa ni mratibu elimu kata ya Sekebugora, mwalimu Hosea Somi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga akikagua mojawapo ya vyoo va nyumba za walimu katika shule ya sekondari Kiloleli kata ya Kiloleli wilayani humo.
Sehemu ya nyumba za walimu katika shule ya sekondari Kililoli kata ya Kiloleli wilayani humo ambazo ni mojawapo ya mpango wa halmashauri kuboresha sekta hiyo muhimu.
Na Robert Hokororo, Kishapu DC
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga inaendelea na mkakati wake wa kuboresha mazingira ya sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu katika shule zake mbalimbali. Inafanya hivyo kupitia programu mbalimbali zikwemo Mpango wa kuboresha Miundombinu katika shule za sekondari (SEDP) ili kumpa mwanafunzi mazingira mazuri ya kujifunza.
Pia halmashauri hiyo kupitia Idara ya Elimu Sekondari ina jukumu kubwa la kuhakikisha shule zake zinafanya vizuri katika mitihani ya kitaifa na hatimaye kuitoa kimasomaso wilaya kitaaluma. Imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ikiwa na lengo la kupanua wigo wa elimu katika shule mbalimbali za sekondari na hivyo wanafunzi kuwa na mazingira mazuri ya kujifunza.
Wanafunzi wanapokuwa na mazingira mazuri ya elimu ikiwemo miundombinu rafiki kwao wanakuwa na ari ya kujifunza na hatimaye kufaulu. Vile vile walimu nao wanapokuwa na wamewekewa mazingira mazuri ya kufundishia huweza kufanya kazi kwa nguvu moja na kwa moyo wote. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo endapo vikiwa katika ubora vinakuwa motisha kubwa kwa walimu na wanafunzi.
Hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga alikabidhiwa miradi ya miundombinu ya shule za sekondari iliyokamilika ujenzi wake. Katika shule ya sekondari Bubiki tayari vyumba vinne vya madarasa pamoja na matunda ya vyoo 18 yamejengwa kwa ajili ya wanafunzi na walimu, hali itakayosaidia kuboresha maisha yao.
Akibainisha hayo katika makala haya, Magoiga anasema mradi huo ambao umegharimu jumla ya sh. milioni 147.8, umetekelezwa katika kata ya Bubiki na hivyo kupunguza au kutatua kabisa changamoto ya uhaba wa vyoo na vyumba vya kwa wanafunzi.
Si hivyo tu bali pia halmashauri imeendeleza miradi hiyo katika kata zingine zikiwemo Mwakipoya, Mwamalasa na Masanga ambapo imeborsha miundombinu katika shule zake. Magoiga anafafanua kuwa shule ya sekondari Mwakipoya yamejengwa matundu 18, Mwamamalasa matundu 18 na Bulekela iliyoko kata ya Masanga jumla ya matundu 18 pia.
Mkurugenzi mtendaji huyo anaweka wazi kwa kusema gharama za mradi huo ni sh. milioni 115.9 ambapo tayari umekabidhiwa katika shule hizo tayari kwa matumizi.
Hata hivyo ili wanafunzi wafanye vizuri shuleni ni muhimu walimu kuwa na mazingira mazuri ya kufundishia na hata makazi yao.
Kwa kuliona hilo halmashauri imekuwa ikijitihadi kuwawekea mazingira mazuri walimu katika shule mbalimbali kama ambavyo mkurugenzi amekuwa akisisitiza. Kama inavyofahamika mwalimu ni mtu muhimu katika ustawi wa wanafunzi na ni mzazi kwa kuwa hutumia muda mrefu na wanafunzi kuliko alivyo mzazi.
Pia kazi ya ualimu ni wito kama walivyo wafanyakazi wa sekta ya afya hivyo mwalimu anapaswa kujengewa uwezo na mazingira mazuri ya kazi yake.
Ikumbukwe hivi karibuni Mkurugenzi Mtendaji Magoiga aliwataka wakuu wa shule wilayani Kishapu kutoa motisha kwa walimu wanaofanya vizuri katika ufundishaji. Ni dhahiri kuwa motisha hiyo ni pamoja na kuwajengea miundombinu ya makazi kwa maana ya nyumba bora karibu na maeneo yao kazi kwenye shule.
Katika kata ya Kiloleli wilayani humo, jumla ya nyumba sita za walimu zimejengwa kwa sanjari na tangi la kuvunia maji ya mvua lenye ujazo wa lita 30,000. Magoiga anasema kuwa mradi wa nyumba hizo zenye kila aina ya huduma umegharimu jumla ya sh. milioni 149.1 na tayari umeanza kutumika.
Kutokana na kukamilika kwa mradi huo sasa walimu wameondokana na adha ya kupanga mbali na shuleni hali iliyowasababishia kuchelewa kufika vituo vyao vya kazi. Kutokana na kupata makazi karibu na shuleni walimu hao wataweza kufanya kazi zao za kufundisha kwa ufanisi mkubwa kwa kuwahi. Miongoni mwa vitu muhimu kwa ufundishaji ni mafunzo kwa njia ya vitendo (practical) hususan katika masomo ya Sayansi ambapo kupitia hivi mwanafunzi anakuwa na uwanja mpana wa kujifunza.
Tayari mkurugenzi mtendaji ametoa vifaa vya maabara vikiwemo stuli 135 kwa ajili ya shule tano za sekondari zilizopo kata mbalimbali wilayani humo.
Mradi huo wenye thamani ya sh. milioni 6.75 umefadhiliwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) chini ya mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (P4R).
Magoiga anabainisha kuwa nchi ya viwanda kama ambavyo ilivyo sera ya Serikali ya Awamu ya tano inatokana na masomo ya sayansi na hivyo mojawapo ya vipaumbele vyake ni kuboresha sekta ya elimu.
Mradi mwingine ni vitanda kwa mabweni ya Shule ya Sekondari Kishapu ambapo Magoiga alikabidhi jumla ya vitanda 31 vyenye thamani ya Sh. 4,650,000 ikiwa ni kutokana na fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Mkurugenzi alitoa ahadi ya vitanda hiyo Septemba 2016 alipofanya ziara shuleni hapo na kukuta changamoto ya uhaba wa vitanda ambavyo vilikuwa ni 10 tofauti na mahitaji ya wanafunzi wake. Shule hiyo ambayo katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2016 ilishika nafasi ya pili kimkoa kati ya shule nane sasa imeondokana na changamoto ya idadi kubwa ya wanafunzi kukosa vitanda.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Wilaya, Paul Kasanda akizungumza na makala haya anasema halmashauri inaendelea kutekeleza miradi katika sekta hiyo. Anasema mradi wa vifaa vya maabara ni miongoni mwa miradi mitatu kwa shule za sekondari zilizopo wilayani humo ikiwa ni njia ya kuboresha sekta ya elimu.
Anataja baadhi ya miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Mangu iliyopo kata ya Shagihilu.
Kasanda anasema kuwa kutokana na misaada hiyo inayotolewa kutoka Serikali Kuu, sekta ya elimu katika halmashauri hiyo itasonga mbele na hivyo ufaulu kwa wanafunzi utapanda.
No comments:
Post a Comment