Matukio : Tanzania Yashiriki Kikao cha 71 cha Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (UNBOA) - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


26 Jul 2017

Matukio : Tanzania Yashiriki Kikao cha 71 cha Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (UNBOA)Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG )wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Prof Mussa J Assad wa pili kutoka kushoto akiwa na wajumbe wa Bodi ya Umoja wa Mataifa baada kikao cha 71 kinachoendelea mjini New York Marekani, kikao hicho kinafanyika kwa muda wa siku mbili.


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG) za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Mussa Assad ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa (UNBoA), jana tarehe 25 Julai, 2017 ameshiriki kuidhinisha ripoti za kaguzi za shughuli za Umoja wa Mataifa kwa mwaka ulioishia tarehe 31 Desemba 2016, kwenye kikao cha 71 cha Bodi ya Ukaguzi ya wanachama wa Umoja wa Mataifa kinachoendelea Mjini New York, nchini Marekani.


Katika kikao hicho, wajumbe wa bodi hiyo walipitia na kusaini ripoti ishirini na nane (28) za ukaguzi wa shughuli za Umoja wa Mataifa. Kati ya ripoti zilizoidhinishwa na wajumbe wa Bodi hiyo, ripoti kumi na moja (11) zilitokana na kaguzi zilizofanywa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (NAOT) na kuwasilishwa na CAG, Prof. Mussa Assad kwenye kikao hicho cha Bodi. Aidha, ripoti kumi na saba (17) zilizosalia zilitokana na ukaguzi uliofanywa na Ofisi za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali za India na Ujerumani.

Katibu Mkuu umoja wa Mataifa Bwana Antonic Guterres akizunguza na wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi wa Umoja wa Taifa katika kikao cha Bodi kilichofanyika mjini New York Marekani hivi karibuni.


Ripoti kumi na moja zilizowasilishwa na Prof. Assad ni kaguzi za Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Idadi ya Watu Duniani la Umoja wa Mataifa (UNFPA), Shirika la Ujenzi na Misaada la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wakimbizi wa Palestina na Mashariki (UNRWA), Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa UNRWA Wakazi (UNRWA – SPF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake (UN – Women), Mfuko wa Ukuzaji Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN Habitat), Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Mahakama ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na Mauaji yaliyotokea Rwanda (ICTR), Mahakama ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na Mauaji yaliyotokea Yugoslavia ya zamani (ICTY), Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kupunguza shughuli za mahakama za kimataifa (IRMCT).


Matukio mengine yaliyofanywa na Bodi hiyo ni pamoja na wajumbe wa Bodi kushiriki katika haflailiyowakutanisha na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. António Guterres. Katika hafla hiyo Mhe. Guterres aliwajulisha wajumbe wa UNBoA kuwa Umoja wa Mataifa unafanya marekebisho makubwa ya kimuundo na kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kugatua na kukasimu madaraka kwenda ngazi za chini ikiwemo ofisi zilizopo kwenye kanda, kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi bila ya kudhoofisha udhibiti.


‘UN inaendelea kufanya maboresho yanayolenga kuimarisha Umoja wa Mataifa katika nguzo zake zakitendaji ikiwemo kuimarisha amani na usalama, haki za binadamu, na maendeleo duniani’, alisema Mhe. Guterres. Aidha alisisitiza kuwa, UN itaendelea kuimarisha usawa na kupinga unyanyasaji ya kijinsia. ‘hatua kadhaa zimeendelea kuchukuliwa ikiwemo kuimarisha uwazi na uwajibikaji na pia kuwalinda watoa taarifa za maovu. Ninafahamu umuhimu wa wakaguzi katika kusaidia kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa na ni kiungo muhimu cha kutoa taarifa kwa nchi wanachama juu ya matumizi ya rasilimali za Umoja wa Mataifa’, alihitimisha, Mhe. Guterres.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyekaa katikati Bwana Antonic Guterres akibadilishana mawazo na wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa katika kikao cha 71 cha bodi hiyo, kilichofanyika mjini New York Marekani.


Wajumbe wa Bodi pia walifanya kikao na Mkuu wa Ofisi ya Sekretariati ya Umoja wa Mataifa (Chef de Cabinet) Bibi. Maria Luiza Ribeiro Viotti kilichogusia maboresho yanafanywa katika Umoja wa Mataifa ambapo Prof. Assad akiwakilisha wajumbe wenzake wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa alimfahamisha Bibi. Ribeiro kuwa wataendelea kutoa mchango chanya kwenye maboresho yanayofanywa na Umoja wa Mataifa. Aidha, aliomba Umoja wa Mataifa kuendelea kutoa elimu ya kutosha na kuboresha mawasiliano kati yake na wafanyakazi wake na wadau ili kufikia mafanikio yanayotarajiwa.


Prof. Assad na ujumbe wake kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, ulifanya mazungumzo na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Mhe. Balozi Modest J. Mero, kwenye Ubalozi wa Tanzania uliopo mjini New York, Marekani ambapo alimshukuru Mhe. Balozi Modest J. Mero na Ofisi ya Uwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kutoa msaada mkubwa kurahisisha shughuli za maafisa wa Ofisi ya Ukaguzi. ‘Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa mchango wenu ambao kwa kweli umekuwa kiungo muhimu katika kufanikisha shughuli hizi za Ukaguzi wa Umoja wa Mataifa’, alisema Prof. Assad.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano waTanzania Prof Mussa J Assad akisalimiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mr Antonic Guterres wakati wa kikao cha 71 cha bodi ya wakaguzi kilichofanyika nchini Marekani.


Aidha alifafanua kuwa, Ofisi imefanikiwa kutoa ripoti kwa wakati kwa miaka mitano mfululizo tangu ijiunge na Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa mwaka 2012. Mhe. Balozi Modest J. Mero alimshukuru CAG kwa taarifa na kutoa rai kwa watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuendelea kuangalia fursa za ukaguzi katika medani za kimataifa ili kuimarisha na kuendeleza ujuzi na uzoefu uliokwishajengeka kwa miaka yote hiyo. ‘Kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri, kwa kweli mnaipa nchi heshima kubwa, hata hivyo niwashauri kuwa ni vyema mkaendelea kutafuta kazi kwenye mashirika mengine ya kimataifa ili kuendeleza ujuzi huo’, alisema Mhe. Balozi Mero.


Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa inaundwa na wajumbe watatu, wanaopaswa kuwa wakaguzi wakuu wa serikali kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Kikao cha mwaka huu kimehudhuriwa na wajumbe wote ambao ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali ya India na mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw. Shashi Kant Sharma, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Ujerumani, Bw. Kay Scheller, na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Mussa J. Assad.


Tanzania ni nchi ya tatu ya Afrika kuwahi kuwa mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa iliyoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1946. Nchi zingine za Kiafrika ni Ghana na Afrika ya Kusini.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonic Guterres akisalimiana na Rais wa Wakaguzi nchini Ujerumani Bwana Amys C.E Morse katika kikao cha 71 cha bodi ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kilichofanyka nchini Marekani.

Post Top Ad