Matukio : Wananchi Wamekumbushwa kulipa kodi ya Majengo - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


23 May 2017

Matukio : Wananchi Wamekumbushwa kulipa kodi ya Majengo


NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA


KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amewahamasisha wananchi wenye majengo katika Jiji la Mwanza kuhakikisha wanalipa kodi ya majengo kwa wakati ili kuepuka kutozwa faini au kufikishwa mahakamani.


Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wadau wa kodi jijini Mwanza jana Kichere alisema kodi ya majengo ipo kwa mujibu wa sheria na italipwa mara moja kwa mwaka, hivyo ni muhimu wananchi wakailipa mwaka huu wa fedha kabla ya Juni 30 .


Alisema TRA haina sababu ya kufikishana mahakamani an wananchi lakini watakaoshindwa kulipa ndani ya muda wa kisheria watalazimika kulipa na tozo au kufikishwa mahakamani na kulingana na matakwa ya sheria za mamlaka hiyo watalipa sh. 70,000 badala ya viwango vya sh. 20,000 (Nyamagana) na sh. 15,000 (Ilemela) vya sasa.


“ TRA na Serikali ya Mkoa wa Mwanza inalenga kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kulipa kodi hii bila adhabu ifikapo Juni 30, mwaka huu ambayo ni mwisho.Wenye majengo kwenye Halmashauri ya Jiji na Manispaa ya Ilemela ambao hawajapokea Ankara zao za kodi wakazichuke ofisi za TRA au kwa viongozi wa serikali za mitaa yao ama wajisajili na kulipia benki yoyote ya biashara,”alisema Kichere.


Alisema TRA mkoa wa Mwanza inasimamia kodi ya majengo yaliyokamilika na kutumika kwa makazi na biashara yaliyothaminishwa au la,yaliyopimwa na yasiyopimwa katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na Manispaa ya Ilemela.


Alieleza kuwa nyumba zilizothaminiwa wamiliki watalipa kodi kwa asilimia ya thamani ya jengo na nyumba za maeneo yasiyopimwa na ambazo hazijathaminiwa kodi italipwa kwa viwango maalumu vilivyopitishwa na mabaraza ya madiwani na kutangazwa na TRA kwenye vyombo vya habari.


Kamishna mkuu huyo wa TRA alifafanua kuwa baadhi ya majengo ya serikali pamoja na ya ibada yamesamehewa, pia wastaafu au wazee wenye umri wa miaka 60,walemavu kwa nyumba moja wanazoishi lakini zisiwe zinatumika kwa biashara nao wamesamehewa.


Hata hivyo aliwaondoa hofu Wakuu wa Wilaya, Naibu Meya pamoja Wakurugenzi wa Jiji na Manispaa ya Ilemela kuwa kodi hiyo si mali ya TRA ni mali ya halmashauri za miji, majiji na serikali za mitaa na hivyo baada ya kukusanywa itarejesha kwenye halmashauri zikatekeleze shughuli za maendeleo.


Kichere alieleza zaidi kuwa ushirikiano wa serikali ya mkoa, serikali za mitaa, umewezesha kutoa makadirio sahihi ya tozo, viwango rafiki, kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji, kutoa elimu kwa jamii, kushughulikia pingamizi za kodi ya majengo kwa wakati pamoja na kuendelea kuimarisha uthamini wa majengo.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella alisema jukumu la kulipa kodi ya serikali ambayo inawezesha kujengwa kwa barabara na huduma zingine za jamii ni la wananchi ambapo TRA wanafanya kazi ya kuikusanya kwa dhamana waliyopewa na serikali.


“ Dar es Salaam wanatuzidi kwa historia tu.Kulipa na kukusanya kodi ya serikali za mitaa kwa uadilifu tukifanya hivyo nchi yetu itakwenda.Kwenye mkoa wangu nimeagiza hakuna mkurugenzi wa halmashauri kutoka nje hadi amekusanya kodi tuliyokubaliana kisha tupigiane hesabu na tuelewane,” alisema Mongella.


TRA inasimamia na kukusanya kodi ya Majengo kuanzia Julai 2016 kutokana na Sheria ya Fedha ya Serikali Mitaa Sura 290, Sheria ya Miji Sura ya 298 na Sheria za Mamlaka ya Mapato Tanzania sura 339.


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella akizungumzia umuhimu kodi ya majengo kwenye mkutano wa wadau wa kodi uliofanyika Ukumbi wa Ofisi yake.Kulia kwake ni Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Kamishna wa Polisi Cloudwing Mtweve na wa kwanza kulia ni Richard Kayombo Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi makao makuu TRA.Picha zote na BALTAZAR MASHAKA
Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella akielezea umuhimu wa wananchi kulipa kodi ya majengo kwenye mkutano wa wadau wa kodi uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi yake.Kulia kwake ni Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Kamishna wa Polisi Cloudwing Mtweve na wa kwanza kulia ni Richard Kayombo Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi makao makuu TRA.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles E. Kichere akizungumza na wadau wa kodi pamoja na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhamasisha ulipaji kodi ya majengo kwa wakati bila shuruti.Watatu kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, Katibu Tawala mkoa, CP Cloudwing Mtweve (wa pili kulia) naRichard Kayombo,Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi makao makuu TRA wa kwanza kulia , kushoto wa kwanza ni Ernest Dundee,Meneja wa mamlaka hiyo mkoani humu .

Post Top Ad