Matukio : STAMICO Yaanza Uzalishaji Makaa ya Mawe Kabulo - Kiwira . - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


2 May 2017

Matukio : STAMICO Yaanza Uzalishaji Makaa ya Mawe Kabulo - Kiwira .



Wataalam wa STAMICO wakiendelea na kazi ya uchimbaji makaa ya mawe katika Mlima wa Kabulo uliopo Kiwira wilayani Ileje mkoa wa Songwe.

Shughuli za uchimbaji wa Makaa ya Mawe zinazofanywa na STAMICO, zikiendelea katika Mlima Kabulo-Kiwira.



Na Koleta Njelekela-STAMICO
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza uchimbaji wa makaa ya mawe katika mlima wa Kabulo uliopo Kiwira katika wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe.


Mratibu wa Mradi wa Uchimbaji Makaa ya Mawe-Kiwira, Mjiolojia Alex Rutagwelela ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji wa STAMICO amesema kazi ya uchimbaji iliyoanza tarehe 30/04/2017 inaendelea vizuri na tayari tani 100 zimechimbwa katika siku ya kwanza. Lengo la mradi ni kuchimba tani 200-300 kwa siku.


“Tumeanza uchimbaji na tani hizo, kama njia mojawapo ya kujaribu mitambo ya uchimbaji, kabla ya uzinduzi rasmi ambao unatarajiwa kufanyika hivi karibuni, baada ya Shirika na wadau wake, kukamilisha maandalizi ya uzinduzi.” Alifafanua Mjiolojia Rutagwelela.


Aidha Rutagwelela amesema matarajio ya STAMICO ni kuchimba kati ya tani 6000 hadi tani 9000 za makaa ya mawe kwa mwezi kwa kuanzia, kiwango ambacho kinatarajiwa kuongezeka kadiri kazi ya uchimbaji inavyoendelea.


Mratibu huyo amesema awamu ya kwanza ya Mradi wa uchimbaji makaa ya mawe inatekelezwa kupitia leseni zake mbili za uchimbaji mdogo wa madini Primary Mining Licences (PMLs) zilizopo ndani ya leseni ya utafiti ya Kabulo zenye ukubwa wa Hecta 16.52.


Leseni hizo mbili za Uchimbaji wa Awali wa Madini katika eneo hilo la Kabulo zina tani zipatazo 241,865 za mashapo ya makaa ya mawe yaliyoko karibu na uso wa ardhi ambayo yataruhusu Uchimbaji wa Mgodi wa Wazi (Open pit mining) kufanyika.


“Uchimbaji huu, ambao umeanzia kwenye mlima wa Kabulo na baadae mlima wa Ivogo, utaiwezesha STAMICO kuzalisha makaa ya mawe na hivyo kupunguza uhaba wa madini hayo nchini ambayo ni moja ya vyanzo vya nishati ya umeme. Makaa ya mawe hutumika kama moja ya vyanzo vya Nishati katika shughuli za uzalishaji viwandani vikiwemo viwanda vya Saruji nchini” alifafanua Rutagwelela.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad