Matukio :Kwa Simu Kutoka London - Safu Mpya - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Tuesday, 2 May 2017

Matukio :Kwa Simu Kutoka London - Safu Mpya


KWA SIMU TOKA LONDON- Safu Mpya Mtandaoni Ndogo Ndogo Mitaani, Ulaya Wazungumzaji , wanafunzi na wapenzi wa Kiswahili wana-arifiwa safu mpya ya mwandishi Freddy Macha. Baada ya miaka mingi akitathimini, kutafiti na kutangaza habari, fasihi na makala, ameanzisha kipindi kipya (cha Video) mtandaoni. https://www.youtube.com/channel/UCtVEe3zlUtuF6pTbn_OK8JQ Ndiyo nini? “Kwa Simu Toka London” siyo toleo la hali ya juu au kustaajabisha. Macha anatumia weledi na ujuzi wake kuelezea -kupitia simu ya mkononi- kadhia mitaani, maholi na majumbani, London, na kwingineko anakotembelea Ughaibuni. Teknolojia inakayotumika ni ya kawaida tu kwa chombo hiki tulichokizoea siku hizi.

Inakuwaje? Vipindi vimegawanyika sehemu tatu.
Ndogo Ndogo

Matukio ya hapa na pale, mafupi mafupi, mseto mseto, yenye mada moja inayogusa au kuchimba kadhia, tukio au weledi Majuu, haraka haraka.
Mahojiano

Na mzungumzaji maalum, yenye vipengele vya taaluma au ujumbe wa kielimu na kijamii.
Mada Maalum

Inayohusu matukio makubwa yeyote kimataifa kama michezo, muziki , sayansi, siasa nk. Wapiiii? You Tube. Idhaa, mlizamu au mlango maalum (“channel”) yaani- “Kwa Simu Toka London.” Watazamaji watakaofurahia kipindi na kubofya “Subscribers” watazawadiwa habari za matoleo mapya yanayotazamiwa kutoka kila juma au inapojiri. Watakaoshindwa vile vile watanufaika bila wasiwasi. Ila ukiwa “Subscriber” (mpenzi wa “Kwa Simu...”) utakuwa na mrabaha au mavuno ya kuweka maoni yako pale. Lugha Gani Kwa sasa itakuwa Kiswahili fasaha na hatimaye kujumuisha nyingine, hususan Kiingereza. Freddy Macha alianzaje? Macha (katikati) - Uhuru na Mzalendo- 1978. Picha ya Khatibu Ali Akiwa Shule ya Sekondari Ilboru na Mzumbe , Morogoro, aliandika na hatimaye kuajiriwa na gazeti mzazi la Kiswahili nchini (na Chama) - Uhuru na Mzalendo- mwaka 1976. Alijifunza na kujumuika na wanahabari wakongwe, leo marehemu mathalani mtangazaji redio mashuhuri miaka ya 70, Abdi Mushi, bwana michezo - Omari Bawaziri, wapiga picha Awadh Shebe na Khatibu Ali,Sengondo Mvungi, Yahya Buzaragi ...nk. Walio hai ni Ndimara Tegambwage, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri Mheshimiwa Harrison Mwakyembe, Salva Rweyemamu nk. Baadhi ya Safu zake Enzi hizo na Sasa Akiwa “Uhuru na Mzalendo” Macha aliandika safu kadhaa ikiwepo “Wachapa Kazi” iliyoangalia Watanzania waliostahili pongezi. Aliripoti habari za wasanii jambo lililomfanya ajifunze Kifaransa kuhoji wanamuziki wa Kikongo (Wazaire) waliofurika Tanzania. Miongoni mwao ni King Kiki na marehemu Remmy Ongala. Mwaka 1986 alichapisha kitabu cha maisha ya Ongala kilichomjenga sana na hatimaye kupata mkataba wa kimataifa na Real World Music- WOMAD , Uingereza. Macha alijiuzulu Uhuru ,1978 na kujaribu kuanzisha gazeti akishirikiana na wenzake wawili. Ila miaka hiyo haikuwa rahisi kama sasa. Aliandikia magazeti mengine mfano Nchi Yetu, Mfanyakazi, Kiongozi, Lengo, New Outlook na African Woman mjini London. Kuanzia 1981 hadi 1992 Macha alikuwa mwandishi maalum wa gazeti la kila Jumapili “The Sunday News”- chini ya mhariri Ulli Mwambulukutu. Safu yake ya Kiingereza “Cultural Images” (1981-84),ilizungumzia kadhia mseto hasa utamaduni. Baada ya kusafiri nchi lukuki, alitua Marekani ya Kusini kusomea muziki na masuala ya afya. Kati ya matukio makuu ni kukutana na kumhoji Mwalimu Nyerere, mjini Rio De Janeiro, Juni 1991 ...na kurusha baadhi ya matukio wakati wa Kombe la Soka la 1994 Idhaa ya Kiswahili BBC tokea Brazil. Salvador, Bahia , 1994. Mahojiano na Mutabaruka, Mshairi Rasta, asiyevaa viatu daima, toka Jamaica. Picha na Amita Macha.... Aliendelea na safu magazeti ya Mwananchi 2003 (Kalamu toka London) na Guardian (“Letter from London) , kisha Citizen (“Chat from London”), hadi sasa. Mahojiano na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Mhe Bernard Membe, London , 2010. Picha ya Urban Pulse Kawahi kupata tuzo gani? Mwaka 1981, Macha alishinda tuzo la uandishi wa mashairi ya Kiingereza yaliyochapishwa mkusanyiko wa Waafrika London, Summer Fires (Heinemann, 1983). Bahashishi ya hadithi fupi fupi ya Jumuiya Ya Madola, kwa kisa kuhusu kuua nyoka, lilitolewa 1996. Tajriba na Uzoefu wa Video, Redio na Filam Wakati wa michezo ya Olimpiki 2012, Macha alishirikiana na vijana wa Urban Pulse kutafiti , na kutangaza tukio hili muhimu. Vipindi bado vinaonekana You Tube. Novemba 2011 sauti yake ilisikika ikisoma kitabu cha mwandishi wa Kenya Binyavanga Wainaina , redio ya BBC4. Anaendelea kufanya kazi na vyombo mbalimbali vya redio, muziki, TV na mitandao, ikiwemo Africans in London TV chini ya nguli Joseph Adamson, Informer East Africa na Swahili Hub. Habari zaidi bofya www.freddymacha.com/

No comments:

Post a Comment