Matukio : Tanzania na Uganda Zakubaliana Kushirikiana - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 6 April 2017

Matukio : Tanzania na Uganda Zakubaliana Kushirikiana



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi ambaye alikuwa mwongozaji wa kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kwa ngazi ya Mawaziri kati ya Tanzania na Uganda akitoa neno la ukaribisho kwa wajumbe waliohudhuria kikao hicho.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakiweka saini Nyaraka yenye maelezo ya masuala yote yaliyokubaliwa katika kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda.

Waziri Mahiga na Mgeni wake, Mhe. Sam Kutesa wakionesha nakala za nyaraka za makubaliano mara baada ya kusaini.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa wakiweka saini Mkataba utakaotoa fursa kwa Tanzania na Uganda kushirikiana katika huduma za usafiri wa anga.

Prof. Mbarawa na Mhe. Kutesa wakionesha nakala za mikataba mara baada ya kuisaini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Mhe. Mhandisi Irene Muloni wakiweka saini Mkataba ambapo Tanzania na Uganda zitashirikiana kuendeleza mradi wa umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo.

Waziri Mahiga na Mhandisi Muloni wakibadilishana nakala za mikataba.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akisoma hotuba ya kufunga kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa akisoma hotuba kwa wajumbe walioshiriki kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda

Baadhi ya Viongozi waandamizi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioshiriki kikao cha JPC kati ya Tanzania na Uganda. Wa kwanza kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi na wa pili ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia hotuba za Waheshimiwa Mawaziri wa Mambo ya Nje

Viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali ya Uganda wakisikiliza hotuba za Mawaziri.

Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano

Bw. Gerald Mbwafu (kulia) kutoka Wizara ya Mambo ya Nje akisalimiana na Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Maji, Bw. Sylvester Matemu kutoka Wizara ya Maaji.

Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wakionesha nyuso za furaha kuashiria furaha yao baada ya kufanikisha mkutano wa JPC.






TANZANIA NA UGANDA ZAKUBALIANA KUSHIRIKIANA


Tanzania na Uganda zimefungua sura mpya ya ushirikiano baada ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo kusaini nyaraka inayoainisha maeneo mbalimbali ambayo nchi hizo zimekubali kushirikiana kwa pamoja ili kuinua uchumi wa mataifa yao.


Nyaraka hiyo iliyosainiwa leo jijini Arusha imetokana na Kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda kilichofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 03 Aprili 2017.


"Makubaliano haya yataongeza chachu ya uhusiano na ushirikiano wetu na Uganda, japokuwa tulichelewa kufanya kikao cha JPC tokea mkataba uliposainiwa mwaka 2007 nchini Uganda". Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga alisema alipokuwa akisoma hotuba ya kufunga.


Kikao cha JPC kilifanyika kwa kuzingatia makundi ya kisekta ambapo katika kila kundi, wajumbe waliainisha maeneo yenye maslahi kwa pande zote ambayo yanajumuisha pamoja na mambo mengine: uendelezaji wa miundombinu; kilimo; viwanda; biashara; uwekezaji; nishati; utalii; utunzaji wa mazingira; uvuvi; ufugaji; afya; elimu; utangazaji; madini na masuala ya kijamii.


Kikao hicho kilitarajiwa kuhitimishwa kwa kusainiwa mikataba sita lakini kutokana na mashauriano ya ndani ya baadhi ya mikataba kutokamilika, mikataba miwili ndio iliweza kusainiwa. Mikataba hiyo ni ushirikiano katika kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo na huduma za usafiri wa anga.


Mikataba minne iliyosalia ambayo inahusu ushirikiano katika usafiri wa reli, usafiri wa majini; utangazaji na ulinzi wa raia itasainiwa wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika hivi karibuni hapa nchini.


Waziri Mahiga alieleza kuwa kusainiwa kwa mikataba hiyo ni muhimu kwa kuwa itaimarisha zaidi misingi ya mahusiano yetu, hivyo alizihimiza pande zote kukamilisha mashauriano hayo ili mikataba hiyo iweze kusainiwa katika muda uliopangwa.


Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Uganda kufanya kazi kwa pamoja ili kuinua uchumi kwa madhumuni ya kuwaondolea umasikini wananchi.


Alisema mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania ni moja ya miradi itakayosaidia kuboresha maisha ya wananchi, hivyo alisisitiza umuhimu wa kukamilisha taratibu zote zilizosalia ili ujenzi huo uweze kuanza.


Alihitimisha hotuba yake kwa kuzipongeza Tanzania na Uganda kwa kufanikisha uwekaji saini wa mikataba miwili ukiwemo wa kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo ambao ulikuwa katika majadiliano kwa zaidi ya miaka minane.


Kikao hicho cha JPC kimefanyika kufuatia maelekezo ya Marais wa nchi hizo waliyoyatoa wakati wa ziara ya Rais wa Uganda nchini mwezi Februari 2017. Viongozi hao waliagiza kikao cha JPC kifanyike kabla ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao ulipangwa kufanyika jijini Dar Es Salaam tarehe 06 Aprili 2017.




Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, 05 Aprili, 2017

No comments:

Post a Comment