Matukio : Maandalizi ya Sherehe za Miaka 53 ya Muungano Yakamilika - Waziri Mhagama - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


22 Apr 2017

Matukio : Maandalizi ya Sherehe za Miaka 53 ya Muungano Yakamilika - Waziri Mhagama


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Jenista Mhagama ameeleza kukamilika kwa maandalizi ya kuadhimisha sherehe za miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitakazofanyika Viwanja vya Jamhuri Mjini Dodoma, siku ya jumatano Aprili 26, 2017.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Aprili 22, 2017 katika Ofisi yake Dodoma.
“Nipende kuwaeleza Watanzania wote kuwa hadi sasa maandalizi ya kuifikia siku ya Maadhimisho ya Sherehe za Muungano tayari yamekamilika kwa kuangalia mambo yote yaliyopangwa katika ratiba ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli.”Alisema Waziri Mhagama.
Amesema sherehe hizo zitakuwa na upekee wa aina yake ukizingatia kuwa ni mara ya kwanza tangu Serikali ilipotimiza adhma yake ya kuhamia Dodoma.
Akitaja upekee huo, Waziri Mhagama amesema sherehe hizo zitapambwa na Gwaride la heshima lililoandaliwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Maonesho ya Kikosi cha Makomando, Onesho la Mbwa na Farasi waliofunzwa, onesho la Ukakamavu la Uzalendo la Wanafunzi kutoka shule za Sekondari za Dodoma, burudani za vikundi vya ngoma kutoka Kaskazini Pemba pamoja na Bendi ya mziki wa kizazi kipya kutoka Dodoma, Yamoto Bend na Mwenge Jazz.
“Ikumbukwe hii itakuwa mara ya kwanza kuiadhimisha sherehe hii ya Miaka 53 ya Muungano wetu kwa kuzingatia Serikali sasa imeshahamia Dodoma na tayari Watendaji wake wapo huku hivyo tuitumie fursa hii kuwaalika Wananchi wote kuudhuria kwa wingi ili kuifanikisha na kuonesha Umoja wetu.”Alisistiza Waziri
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba ametoa wito kwa Watanzania wote wajitokeze kwa wingi kwenda kuangalia mafanikio yaliyotokana na uwepo wa Muungano huo.
“Muungano huu umetupa mafanikio mengi ikiwemo; kuijengea nchi heshima, kuwepo kwa Katiba, kuimarika kwa Taasisi za kimuungano, ongezeko la masuala ya kimuungano kutoka 11 hadi 22, ongezeko la usalama, Kuwepo Mfumo dhabiti wa kushughulikia changamoto za Muungano na ongezeko la ushirikiano kwa masuala yasiyo ya Kimuungano.”Alieleza waziri Makamba.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana alipongeza jitihada za Ofisi ya Waziri Mkuu hususan Kitengo cha Maadhimisho kwa kushirikiana na Ofisi yake kwa kuratibu na kuhakikisha maandalizi yote yamekalika kwa wakati uliopangwa.
“Niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jitihada zake kuiratibu siku hii muhimu kwa Taifa letu, na nitoe wito kwa Wakazi wa Dodoma na walioko nje ya Mji kuonesha mfano kuja kwa wingi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.”Alisisitiza Mhe.Rugimbana.


CHANGAMOTO ZA MUUNGANO ZATATULIWA KWA KIASI KIKUBWA : MAKAMBA
Na; Evelyn Mkokoi na Lulu Mussa - Dodoma
Waziri wa Nchi anayeshughulia masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba, amesema kuwa changamoto za Muungano wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar zimetatuliwa kwa kiasi kikubwa kutoka 15 mwaka 2006 hadi kufikia changamoto 3 kwaka huu 2017, Muungano unaotimiza miaka 53 wiki ijayo.
Waziri Makamba amezungumza hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na waratibu wa sherehe za kitaifa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Walemavu na kusimamiwa na Waziri Mwenye dhamana Mhe Jenista Mhagama.
Mhe. Makamba amezitaja changamoto zilizobakia kuwa ni pamoja na usajili wa vyombo vya moto unaorahisisha kusafirisha magari kutoka Zanzibar kwenda Bara na kutoka Bara kwenda Zanzibar na kusema kuwa swala hili linafanyiwa kazi kwa kumalizwa kwa taratibu za kisheria.
Alisema kuwa changamoto nyingine inahusu Hisa za Zanzibar kwa iliyokuwa bodi ya safari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Pamoja na Mapendekezo ya tume ya Pamoja ya fedha.
Awali akizungumzia Muungano huo unaotimiza miaka 53, Waziri Makamba Alisema kuwa umekuwepo kisheria na umerasimisha udugu na ushirikiano uliyokuwepo kati ya Bara na Visiwani.

Mkutano huo wa waandishi wa habari uliandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Walemavu umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Jordan Rugimbana, Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wa Ofisi hizo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi, Ajira na watu wenye Ulemavu Mhe,Jenista Mhagama akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusu Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika Mkoani Dodoma 26 Aprili 2017.Kulia kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Januari Makamba na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw.Jordan Rugimbana.

Waandishi wa Habari kutoka Vyombo mbalimbali wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi, Ajira na watu wenye Ulemavu Mhe,Jenista Mhagama wakati akizungumza nao kuhusu maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika Mkoani Dodoma 26 Aprili 2017.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Januari Makamba akizungumza na waandishi wa habari leo Mjini Dodoma kuhusu matukio mbalimbali yatakayokuwepo katika Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika Mkoani Dodoma 26 Aprili 2017.Kushoto kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi, Ajira na watu wenye Ulemavu Mhe,Jenista Mhagama na mwishoni ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw.Jordan Rugimbana.


Mkoa wa Dodoma Bw.Jordan Rugimbana akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) juu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika Mkoani Dodoma 26 Aprili 2017 na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi.Kulia kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi, Ajira na watu wenye Ulemavu Mhe,Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Januari Makamba.


Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO Dkt.Hassan Abbas akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari kuhusu Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika Mkoani Dodoma 26 Aprili 2017.KUlia kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi, Ajira na watu wenye Ulemavu Mhe,Jenista Mhagama ,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Januari Makamba na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw.Jordan Rugimbana.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera na Uratibu) Dkt.Hamis Mwinyimvua(kushoto) na Mkurugenzi Idara ya Uratibu na Maadhimisho ya Kitaifa Ofisi ya Waziri Bi.Flora Mazilengwe wakifurahia jambo katika Mkutano na waandishi wa Habari kuhusu juu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika Mkoani Dodoma 26 Aprili 2017.


Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof.Faustine Kamuzora akifuatilia taarifa ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Januari Makamba wakati wa mkutano na waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika Mkoani Dodoma 26 Aprili 2017. Picha zote na Daudi Manongi-MAELEZO, DODOMA.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad