Zanzibar /Sanaa : Balozi Seif Ali Iddi azungumza na uongozi wa chama cha Wasanii Ofisini kwake - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


2 Mar 2017

Zanzibar /Sanaa : Balozi Seif Ali Iddi azungumza na uongozi wa chama cha Wasanii Ofisini kwake



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Uongozi huo ulifika kumtaarifu rasmi azma yao ya kuandaa Tamasha la kuibua vipaji vya wasanii wanchanga Zanzibar linalotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu.

Balozi Seif akiwa katika picya ya pamoja na Uongozi wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya aliofanya nao mazungumzo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Msanii Jamila Abdulrahman { Babyjay } na Mohamed Abdulla Laki. Kushoto ya Balozi Seif ni Msanii Abdulkheir Chum na Msanii Rashid Mustapha ambae ni msemaji wa Chama hicho. Picha na – OMPR – ZNZ.



Uongozi wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kizazi Kipya Zanzibar (ZFU) unafikiria kuandaa mpango maalum wa kuwawekea Bima ya Afya wanachama wake kwa lengo la kuwakomboa wakati wanapokumbwa na matatizo ya Kiafya.


Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Chama hicho Mohamed Abdulla Laki akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa ZFU wakati wa mazungumzo yao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.


Mohamed Abdulla Laki alisema inakuwa aibu na masikitiko makubwa pale Msanii ambaye ni kioo cha jamii anapoonekana akidhalilika wakati akitafuta huduma za matibabu kipindi anaposumbuiliwa na matatizo ya kiafya bila ya kupata msaada wa uhakika.


Alisema wapo baadhi ya wasanii katika zama tofauti zilizopita waliowahi kukumbwa na kadhia hiyo na kuishia katika mazingira ya kusikitisha huku jamii ikijisahau kwamba wasanii hao walitumia nguvu, ujuzi na uzalendo wao katika kuielimisha jamii hiyo kupitia fani ya sanaa.


Akizungumzia Tamasha la kuibua Vipaji vya wasanii wapya linalotarajiwa kuandaliwa na Chama hicho Mwezi Septemba Mwaka huu Katibu wa Chama hicho Laki alisema wasanii watakaoonyesha uwezo mkubwa watatunukiwa zawadi maalum ili kuwapa motisha wa kuendeleza vipaji vyao.


Hata hivyo Laki alisema kutokana na uanagenzi wa masuala kama hayo Uongozi wa chama chake uko tayari kupokea msaada, ushauri na hata mawazo kutoka kwa wataalamu waliobobea ili kuona lengo la kuandaa Tamasha hilo linafanikiwa vizuri.


Alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Wasanii Vijana wa Kizazi Kipya hivi sasa wamebadilika kimaadili kiasi kwamba hata sanaa zao wameamuwa kuzielekea zaidi katika maadili yanayohitajika na kukubalika na Jamii.
Aliliomba Baraza la Sanaa Zanzibar kuendelea kukipa mashirikiano ya karibu zaidi Chama hicho ili kuona sheria, kanuni na Maadili ya kazi za Wasanii yanafuatwa na kuzingatiwa ipasavyo.


Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwaahidi Wasanii hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwasaidia Vijana waliojiweka kimalengo katika kuendesha maisha yao.


Balozi Seif alisema Sanaa ni miongoni mwa Sekta ambazo hutoa ajira hasa kwa vijana kutokana na umuhimu wake wa kuelimisha, kufurahisha sambamba na kufikisha ujumbe kwa Jamii.


Alisema ili kuimarisha Sanaa Nchini ni vyema nyimbo zinazotungwa zikaendelea kutoa mafunzo na burdani akiwasisitiza Wasanii umuhimu wa kupenda kufanyakazi kwa kushirikiana na Umoja mambo yanayoshinda majungu na fitina.


Katika mazungumzo hayo Uongozi huo wa Chama cha Wasanii wa Muziki wa Kikazi Kipya {ZFU} umemkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Albamu Mpya iliyozindauliwa na chama hicho.


Albamu hiyo isemayo Amani kwanza yenye nyimbo zote za Kitaifa inakusudiwa kuuzwa kwa lengo la kusaidia kuendesha shughuli zao za kila siku zinazohitaji gharama kubwa katika utengenezaji wake.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
1/3/2017.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad