Teknolojia : Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan akutana na rais wa shirika la DATANG kutoka China - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


2 Mar 2017

Teknolojia : Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan akutana na rais wa shirika la DATANG kutoka China


Shirika la Datang Telecom International Technology Company Limited la Serikali ya China lina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza vifaa vya mawasiliano nchini kwa ushirikiano na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).


Rais wa Shirika hilo Yuan Yong ametoa kauli hiyo 1-Mar-2017 baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam.


Yuan Yong amemweleza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Serikali ya China pia ina mpango wa kuikopesha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kiasi cha shilingi bilioni 600 ili kuipa uwezo wa kiteknolojia na kupanua mtandao wa mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini hasa vijijini.


Rais huyo amesema lengo la mkakati huo ni kuifanya TTCL kuwa Kampuni bora inayotoa huduma za mawasiliano kwa njia ya kisasa kuliko kampuni yeyote katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.


Amesema kuwa mahusiano mazuri kati ya Tanzania na China ndio yamepelekea shirika hilo kuweka mikakati ya kuja kuwekeza nchini katika sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma bora za mawasiliano mijini na vijijini kwa njia ya kisasa bila usumbufu wowote.


Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameonyesha kufurahishwa na mikakati hiyo na kusisitiza kuwa serikali ipo tayari kwa uwekezaji huo mkubwa kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande hizo Mbili.


Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema anaimani kubwa kuwa uwekezaji huo ukikamilika utaiwezesha (TTCL) kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.


Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kuelekea katika uchumi wa viwanda kwa kishindo hali ambayo itasaidia taifa kuongeza pato lake la taifa pamoja na kutoa ajira kwa mamia ya wananchi kupitia viwanda ambazo vitajengwa nchini.


Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia amepongeza mpango wa Shirika hilo la Mawasiliano la Serikali ya China wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wa TTCL ikiwemo ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Utafiti wa Mawasiliano nchini hatua ambayo itasaidia kuimarisha utendaji kazi kwa wafanyakazi wa TTCL ili waweze kuendana na teknolojia ya kisasa ya mawasiliano Duniani kupitia tafiti zitakazofanywa nchini.


Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Ikulu- Dar es Salaam.


1-Mar-2017.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akizungumza na Rais wa Shirika la Datang Telecom International Technology Company Limited la Serikali ya China Bw.Yuan Yong (kulia) pamoja na ujumbe wake, Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

10:Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa Shirika la Datang Telecom International Technology Company Limited la Serikali ya China Bw.Yuan Yong na ujumbe wake mara baada ya kupokea taarifa ya mpango wa serikali ya China wa kuikopesha TTCL ili kuipa uwezo wa kiteknolojia na kupanua mtandao wa mawasiliano vijijini na mijini pamoja na kujenga kiwanda cha kutengeneza vifaa vya mawasiliano hapa Tanzania. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad