Matukio : Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Songwe awatolea Uvivu Madiwani, Mbunge - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


15 Mar 2017

Matukio : Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Songwe awatolea Uvivu Madiwani, Mbunge





Elias Nawera.



Na Brandy Nelson

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mkoani hapa,Elias Nawera ambaye ameingia mgogoro na madiwani wake, ameibuka na kutoa msimamo wake kwamba atafanya kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma na si kwa matakwa ya wanasiasa.



Hivi karibuni Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Songwe, Phillipo Mulugo walidai kutoridhishwa na hawana imani na utendaji kazi wa mkurugenzi huyo kwenye kikao chao kilichoitishwa kwa dharula kwa lengo la kumjadili na kumuazimia kumfuka kazi.

Akizungumza juzi , Nawera alisema kuwa amepelekwa kwenye halmashauri hiyo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na siyo kumtumikia mtu mmoja mmoja kwani kufanya hivyo ni kukiuka misingi ya utawala bora.



"Unajua baraza la madiwani ni wawakilishi wa wananchi na ni siasa, na siasa mara nyingi ilivyo ni nani kapata nini wakati gani vipi, kimsingi ndiyo siasa, wilaya yetu ni mpya na kuna watu wanataka kufanya kazi kwa namna walivyokuwa wamezoea kufanya mambo yao, kitu ambacho siwezi kukubaliana nacho hata siku moja,"alisema.


Alisema tangu alipofika katika halmashauri hiyo Septemba mwaka jana, alikuta mazoea ya watu kama wana ufalme kana kwamba Serikali haipo, hivyo yupo Songwe kufanya kazi kimfumo wa kiserikali na siyo kumtumikia mtu mmoja mmoja ambapo jambo hilo limekuwa likikwaza watu.


"Mfano kwenye kikao cha halmashauri nililazimishwa kumpa mtu kazi kwa jina,kufanya biashara na mtumishi wa halmashauri ,nikiuke sheria ya manunuzi kwa kusema sheria nini,vitu ambavyo sikubaliani navyo kwani kufanya hivyo nikukiuka sheria,taratibu na misingi ya utawala bora ".alisema


Mkurugenzi huyo alisema amekuwa akienda vijijini kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero za wananchi lakini amekuwa akizuiwa kufanya hivyo na kuambiwa abaki ofisini.

"Nimewahi kukatazwa nisiende vijijini,mimi ninajua rais amenileta huku nitumikie watu na Ilani yenyewe ya chama cha mapinduzi inasema lazima twende chini tufanye kazi na watu, kwa hiyo ukiniambia kitu tofauti na hicho miongozo, sheria kanuni na taratibu mimi sitokusikiliza kwa sababu nitataka kutumikia wananchi na kumsikiliza yule aliyenileta.'alisema

Alisema hata Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa mara nyingi amekuwa akiwaagiza watendaji kutoka ofisini na kwenda vijijini kwa wananchi, kwani pia kuna watumishi ambao wapo huko na wanahitaji huduma lakini hawana uwezo wa kufika wilayani hivyo hutumia fursa hiyo kuwasikiliza mahitaji yao.


Aidha alisema ameshangazwa na utaratibu wa Mkurugenzi kutakiwa kutoa taarifa katika ofisi ya mbunge au kwa katibu wa mbunge anapotaka kwenda vijijini kufanya kazi.


"Ukisimamia kwenye msimamo wa kufuata misingi ya sheria kanuni na taratibu za utumishi wa umma hapo ndipo unaonekana haufai,unakiburi au huna adabu"alisema


Akizungumzia mgogoro huo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Galawa alisema ni kitu cha kawaida katika utendaji kazi kwani hata katika familia hali hiyo hutokea na kwamba amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa utulivu na kusahau yaliyopita.


Chanzo Gazeti la Mwananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad