Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa fedha za Serikali ya
Baraza la Wawakilishi (PAC), Ofisini kwake Migombani.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ukaguzi wa fedha za Serikali ya Baraza la Wawakilishi
(PAC), Mhe. Omar Ali Shehe, akizungumza wakati kamati yake ilipokutana
na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
Ofisini kwake Migombani.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa
katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi wa fedha za
Serikali ya Baraza la Wawakilishi (PAC), pamoja na baadhi ya watendaji
wakuu wa ofisi yake, Ofisini kwake Migombani.
ZANZIBAR 15/07/2014.
Na: Hassan Hamad (OMKR).
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, Serikali
inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuongeza vyanzo vya mapato ikiwa ni
pamoja na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato hayo.
Akizungumza
na Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya ukaguzi wa fedha za Serikali
(PAC) Ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema ikiwa mianya ya
upotevu wa mapato ya serikali itadhibitiwa ipasavyo, serikali itaweza
kuongeza mapato yake na kuweza kukamilisha miradi ya maendeleo kwa
wakati.Aidha
amesema serikali inapaswa kutafakari zaidi kuona kuwa sehemu kubwa ya
matumizi kwa ajili ya kazi za maendeleo inatokana na mapato ya ndani,
badala ya kutegemea wafadhili na mikopo kutoka nje.
“Sasa
hivi mapato ya ndani yanatumika kwa kazi za kawaida wakati kazi za
maendeleo zinasubiri wafadhili na mikopo kutoka nje, ukweli serikali
tunapaswa tujifunze juu ya hali hii ili tumewe kuiepuka kwa mustakbali
mwema wa maendeleo ya nchi yetu”, Maalim Seif aliwaambia wajumbe wa
kamati hiyo. Amesema
Serikali inathamini juhudi zinazofanywa na kamati hiyo katika udhibiti
wa fedha za umma, na kuishauri iendelee kuwa wazi katika kueleza
matumizi ya fedha za Serikali.
Maalim
Seif amesema Ofisi yake imekuwa ikiyafanyia kazi mapendekezo
yanayotolewa na kamati hiyo, na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo kwa
lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo
na Serikali kwa ujumla.
Nae
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa fedha za Serikali ya Baraza la
Wawakilishi Mhe. Omar Ali Shehe amewapongeza watendaji wakuu wa Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kuweza kusimamia vyema matumizi ya fedha
za Ofisi hiyo.
Amebainisha
kuwa kamati yake ambayo ndiyo yenye jukumu la kufuatilia ripoti ya
mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, haikubaini kasoro yoyote
ya matumizi ya fedha, licha ya kuwepo mapato madogo tofauti na yale
yaliyoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi. Ameishauri Serikali kuyafanyia kazi mapendekezo ya Ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali ya mwaka 2011/2012 ili kuweza kukabiliana na changamoto zolizojitokeza.
Wakati huo huo,
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amekutana na balozi mpya wa
Tanzania nchini Urusi balozi Wynjones Kisamba na kusema kuwa Tanzania
ikiwa nchi isiyofungamana na upande wowote kisiasa, itaendelea
kushirikiana na pande zote katika kukuza na kuendeleza mahusiano ya
kimataifa.
Amesma Tanzania ni nchi iliyojijengea sifa kubwa katika medali ya Kimataifa, na itaendelea kuienzi sifa hiyo. Amemtaka
balozi Kisamba kuendelea kuitangaza Tanzania kwa kueleza fursa za
uwekezaji zilizopo nchini, huku Zanzibar ikitilia mkazo katika maendeleo
ya sekta ya utalii.
Maalim
Seif amesisiza kuwa mabalozi wa Tanzania nchi za nje wana jukumu kubwa
la kuendeleza diplomasia ya kiuchumi katika nchi wanazokwenda, ili
kusaidia kukuza uchumi wa nchi.Amempongeza
balozi huyo kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchi Urusi, na kumtakia
mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake.
Nae
balozi Kisamba amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa atafanya
kila awezalo kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Urusi
unaimarika kwa maslahi ya pande zote mbili. Amesema
nchi hizo zina uhusiano wa muda mrefu tokea wakati wa kupigania uhuru,
na kwamba uhusiano huo kamwe hauwezi kupuuzwa, na badala yake utazidi
kuimarishwa.
Akizungumzia
uzoefu wake kuhusu Urusi, balozi Kisamba amesema nchini hiyo ni
miongoni mwa nchi zinazotoa watalii wengi duniani hasa wakati wa msimu
wa baridi, na kuahidi kulishughulikia suala la kuendeleza utalii, ili
watalii wengi wa Urusi waweze kuja Tanzania.
No comments:
Post a Comment