Mkurugenzi wa Idara ya Habari Dkt. Hassan Abbass akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nuru Millao (hayupo pichani) wakati wa Kikao Kazi cha Maafisa Mawasiliano Serikalini mapema hii leo Mjini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nuru Millao akizungumza na Maafisa Mawasiliano wa Serikali (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi cha maafisa hao mapema hii leo mjini Dodoma, kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Dkt. Hassan Abbass .
Maafisa Mawasiliano wa Serikali wakiendelea na kikao kazi mapema hii leo mjini Dodoma.
Bw. Dotto Paul toka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari (IJMC) akitoa mada kwa Maafisa Mawasiliano wa Serikali wakati wa kikao kazi cha maafisa hao (hawapo pichani) mapema hii leo mjini Dodoma.
Maafisa Mawasiliano wa Serikali wakifuatilia mada wakati wa kikao kazi mapema hii leo mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw. Theophil Makunga akitoa mada kwa Maafisa Mawasiliano wa Serikali wakati wa kikao kazi cha maafisa hao (hawapo pichani) mapema hii leo mjini Dodoma.
Afisa Mawasiliano toka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bw. Innocent Mungy akichangia mada wakati wa kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali mapema hii leo mjini Dodoma.
Picha zote na Eliphace Marwa – Maelezo
………..
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao amewataka Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kuuza huduma zitolewazo na Wizara au Taasisi husika kwa lengo la kutekeleza shughuli za Serikali.
Bibi Nuru Millao ameyasema hayo leo mjini Dodoma katika Ukumbi wa Hazina ndogo wakati wa Kikoa Kazi cha Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kilicholenga kuwajengea uwezo Maafisa Mawasiliano Serikalini.
“Katika kikao hiki tutapata nafasi ya kujadiliana namna bora ya kuboresha mawasiliano katika maeneo yetu ya kazi, kuisemea Serikali, kuitendea haki Serikali katika kuwasilisha taarifa mbalimbali za Serikali” alisema Bibi. Millao.
Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Bw. Dotto Paul alisema kuwa wajibu mkuu wa Maafisa Mawasiliano Serikalini ni Kufuatilia kwa ukaribu nini kimeripotiwa kwenye vyombo vya habari kwa lengo la kuwa tayari kujibu au kufuatilia habari zinazohusu Serikali.
Bw. Paul aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu wajibu wa Maafisa Mawasiliano Serikalini katika kutoa taarifa za Serikali kwa Umma kupitia vyombo vya habari na Wajibu wa vyombo vya habari katika kutoa habari za Serikali kwa Umma.
Aidha alisema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali za maafisa Mawasiliano katika kutimiza wajibu wao ikiwemo upungufu wa mafunzo kuhusu tasnia na ujuzi wa kutosha ambapo kuna fursa chache za mafunzo na masomo katika kuongeza ujuzi kwa maafisa mawasiliano.
Akisisitiza zaidi Bw. Paul alisema kuwa mbali na hayo vyombo vya Habari vina Wajibu wa kutoa Habari za Serikali kwa Umma na kuutarifu umma kuhusu mipango, shughuli na vipaumbele vya serikali pamoja na utekelezaji wake.
“Vyombo vya Habari vinatakiwa kuwa daraja na sauti muhimu kati ya umma na serikali kwa kuzingatia maoni, mahitaji ya umma na kuyawasilisha kwa walengwa kama taasisi a uviongozi kwa kusikiliza upande wao, na kuyaripoti” Alisema Bw. Paul.
Nae Bw. Theofil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) akiwasilisha mada kuhusu mtazamo wa Wahariri kwa Maafisa Mawasiliano wa Serikali, amewataka Maafisa Mawasiliano kuhakikisha wanasimamia idara zao ipasavyo kwa kutoa taarifa sahihi kwani vyombo vya habari vinawategemea kwa kiwango kikubwa.
“Mawasiliano na mahusiano ya Wahariri na Maafisa Mawasiliano Serikalini yawe ya ukaribu na kuelewana ili kuweza kupata taarifa sahihi na kwa upana zaidi kuhusu tukio fulani kwa lengo la kuboresha shughuli za Serikali” alisema Bwa. Makunga.
No comments:
Post a Comment