Maisha : Ufugaji na Kilimo Yawaongezea Kipato walengwa wa TASAF, Shinyanga - Wazalendo 25 Blog

Breaking

Glory to Story.


Post Top Ad


9 Feb 2017

Maisha : Ufugaji na Kilimo Yawaongezea Kipato walengwa wa TASAF, Shinyanga


NA ESTOM SANGA- SHINYANGA


Walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF mkoani Shinyanga wameeleza kunufaika na fedha zinazotolewa na mfuko huo kama ruzuku kwa kuanzisha miradi midogo midogo na hivyo kujiongezea kipato na kupunguza tatizo la umaskini lililokuwa linawakabili kabla ya kuanza kwa Mpango huo.


Wakizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea baadhi ya kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Shinyanga baadhi ya walengwa hao wameeleza kuwa wameweza kuanzisha miradi ya ufugaji wa nguruwe, mbuzi, ng’ombe na kuku kwa kutumia ruzuku ya fedha walizozipata kupitia utaratibu wa uhawilishaji fedha unaofanywa na TASAF.


Walengwa hao wamesema kabla ya kuingizwa kwenye utaratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini,walikuwa wakihangaika na kushindwa kupata fedha za kuanzisha miradi midogo midogo kutokana na kutokuwa na fursa ya kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha na hivyo kutopea katika dimbwi la umaskini.


“Ninaishukuru sana serikali kwa kutuletea TASAF kwani imetufungua macho na kuwa chachu ya maendeleo kwani sasa naishi kwenye nyumba yangu niliyoijengwa baada ya kudunduliza fedha kutoka TASAF” amesisitiza Bi.Christina Ndimila (70) mkazi wa Ndala A katika manispaa ya Shjinyanga.


Walipoulizwa wanawezaji kuanzisha miradi hiyo ilhali baadhi ya watu wanadai kuwa ruzuku ya fedha inayotolewa na TASAF ni ndogo, walengwa hao wamesema kuwa matumizi sahihi na kuzingatia masharti ya Mpango ndiyo kumewawezesha kujiwekea akiba kidogo kidogo ya fedha hizo kila wanapozipata.


“ Ukizipata fedha za TASAF na kuzila zote utaziona kuwa ni ndogo ,lakini ukipata na kuziwekeza kwenye mradi wowote mdogo fedha hizo huongezeka baada ya muda mfupi na hivyo kukupa uwezo wa kujiendeleza” alisisitiza Bi. Joyce Jindai Lubunga(59) mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini anayeishi katika mtaa wa Banduka nje kidogo ya manispaa ya Shinyanga.


Waandishi wa habari waliotembelea Baadhi ya walengwa katika manispaa ya Shinyanga wameshuhudia baadhi yao wakitumia sehemu ya fedha za ruzuku kutoka TASAF kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba, kuanzisha bustani za mboga mboga hususani nyanya, ufugaji wa nguruwe, mbuzi, kuku na ng’ombe shughuli ambazo zimeendelea kuwaongezea kipato.


Hata hivyo mbali ya mafanikio hayo walengwa hao wameeleza kuwa wanakabiliwa na tatizo la utaalamu wa mifugo hususani uwezo mdogo wa kukabiliana na magonjwa yanayokumba mifugo yao na hivyo kuomba wataalamu wa mifugo kuwatembelea kwenye maeneo yao na kuwapa ushauri wa namna ya kuboresha shughuli zao ili waweze kupata mafanikio zaidi.


Zifuatazo hapo chini ni baadhi ya picha za walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini katika manispaa ya Shinyanga wakionyesha mafanikio na miradi wanayoitekeleza baada ya kupata ruzuku kutoka TASAF.

Mmoja wa walengwa wa TASAF katika manispaa ya Shinyanga akiwa nje ya nyumba yake aliyoijenga kwa fedha za ruzuku kutoka TASAF ikiwa ni jitihada za kuboresha makazi yake na picha ya chini mlengwa huyo akiwaonyesha Waandishi wa habari baadhi ya mbuzi aliowanunua kutokana na ruzuku hiyo.


Mmoja wa walengwa wa TASAF bi. Maria Gabriel Picha ya juu akiwa karibu na nyumba yake ya zamani na chini ni nyumba yake mpya aliyoijenga baada ya kupata fedha za ruzuku kutoka TASAF.Picha inayofuatia ni bomba la maji alilovuta kutokana na fedha za ruzuku hiyo.

Mmoja wa walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini Bi.Perpetua Tungu picha ya chini akiwa katika bustani yake ya mboga aliyoianzisha kutokana na fedha za ruzuku kutoka TASAF kama sehemu ya kujiongezea kipato. Picha ya chini inaonyesha nyumba anayoendelea kuijenga kwa kutumia fedha hizo ikiwa ni jitihada za kuboresha makazi yake.

Mmoja wa walengwa wa TASAF BI. Rehema Naligigwa katika manispaa ya Shinyanga akionyesha banda analolitumia kufuga nguruwe baada ya kupata fedha za ruzuku kutoka TASAF.

Post Top Ad