Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, ameiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na
Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA) kuwachukulia hatua wale wote wanaoitia
doa taaluma hiyo kwa kufanya ubadhilifu wa fedha za umma.
Maagizo
hayo yametolewa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Mpango, wakati wa Uzinduzi wa Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC)
uliokwenda sambamba na ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa wahasibu
unaojumuisha wadau kutoka nchi za Afrika Mashariki, katika eneo la
Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Amesema
kuwa Idadi ya Wahasibu wenye sifa inazidi kuongezeka na hivyo kuisaidia
Serikali, japo kuwa Serikali hairidhiki kuona wanataaluma wa Uhasibu na
Ukaguzi wa hesabu (CPA) wanaongezeka huku vitendo vya ubadhilifu wa
fedha za Umma na ufisadi vikiendelea kuripotiwa.
“Wapo
hata wahasibu wanaotumia taaluma yao vibaya, wanaowawezesha
wafanyabiashara kukwepa kodi, wanachakachua vitabu vya taarifa za fedha
na kufanya ufisadi kwa njia ya kalamu na kompyuta jambo ambalo
halikubaliki hata kidogo” Aliongeza Dkt. Mpango
Amesema
kuwa machozi ya masikini wa Tanzania yatawafuata mafisadi hadi kaburini
lakini serikali ya Awamu ya Tano haitasubiri hao mafisadi wafe,
itawatumbua na wala hakuna mzaha na kwamba tayari mahakama ya mafisadi
imeanza kazi na itawashughulikia.
Aidha,
Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewaasa
wanataaluma wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu kuitumia taaluma yao
kuisaidia Serikali katika hatua yake ya kuelekea katika uchumi wa kati
unaotegemea viwanda kwa kuwa taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na
Wakaguzi wa Hesabu, Bw. Pius Maneno amesema kuwa, Kituo hicho
kilichozinduliwa cha APC hadi kumalizika, kitagharimu Sh. Bilioni 35
ambapo mpaka sasa fedha zilizotumika ni takribani Sh. Bilioni 33
“Gharama
halisi za ujenzi wa kituo hicho zilikuwa Bilioni 14 lakini kutokana na
mzabuni wa ujenzi kuchelewesha ujenzi ndio maana kumekuwa na Ongezeko la
kiasi hicho cha fedha” aliongeza Bw. Maneno.
Ujenzi
wa kituo hicho ambao uko katika eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 14
umehusisha ujenzi wa Kumbi za mikutano zinazochukua zaidi ya watu 1600,
viwanja vya michezo na vyumba vya kisasa 108 vya kulala wageni.
Bw.
Maneno amesema kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutaifanya Bodi hiyo
kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kikitumika kukodi kumbi za
kufanyia na kusahisha mitihani ya Bodi (NBAA).
Amezitaja
faida zingine kuwa ni kuboreshwa kwa mazingira ya kitaaluma na
wanataaluma wa uhasibu pamoja na kuimarika kwa utawala bora na kuwa
chachu ya uchumi wa viwanda, kwa kuwa Kituo hicho, kinatoa elimu bora
itakayowawezesha wahitimu kuingia kwenye ushindani ndani ya nchi za
Afrika Mashariki na Duniani kwa ujumla.
Ujenzi
wa Kituo hicho umedhaminiwa na serikali kupitia mkopo kutoka Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii-NSSF, Bodi ya Uhasibu-NBAA na Mbia mwenza wa kituo
hicho, Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Serikali-GEPF.
Waziri
wa Fedha, Dk. Philip Mpango (kulia), akikata utepe kwa niaba ya Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa kuashiria kuzindua rasmi Kituo cha Taaluma ya
Uhasibu (APC), kilichopo Bunju jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA),
Profesa Isaya Jairo na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa GEPF, Joyce
Shaidi.
Mwonekano wa baadhi ya majengo ya kituo hicho.
Mwonekano wa ukumbi wa mikutano wa kituo hicho.