Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
JUMLA
ya ajira 16,671 zimetengenezwa na viwanda vya uzalishaji nchini ambapo
viwanda vya wawekezaji kutoka nje ya nchi vikiongoza kwa utoaji wa ajira
hizo.
Takwimu
hizo zimetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda, Biashara
na Uwekezaji, Charles Mwijage wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa
habari kuhusu ongezeko la wawekezaji nchini kipindi cha mwaka mmoja wa
uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Waziri
Mwijage amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inafanya juhudi za
kuwahamasisha wawekezaji ili waweze kushiriki katika kuchochea mageuzi
ya kiuchumi hivyo imeanza kupunguza uuzaji wa malighafi nje ya nchi
ikiwa ni njia mojawapo ya kuwavutia wawekezaji kuwekeza nchini.
”Katika
kujenga uchumi wa viwanda, tunalenga kujenga uchumi shirikishi na ulio
endelevu ambao utahusisha watu wengi hivyo utaratibu wa aina hiyo
utawasaidia kuwainua wananchi kiuchumi pamoja na kukuza pato la taifa,”
alisema Mwijage.
Kwa
mujibu wa Mwijage ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja cha
Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, takwimu zinaonyesha kuwa kuna
ongezeko la uwekezaji katika sekta za ujenzi wa majengo, maliasili,
rasilimali watu, viwanda vya uchakataji bidhaa, sekta ya nishati,
kilimo, huduma, usafiri pamoja na mawasiliano.
Aidha,
amezitaja sekta zingine za uwekezaji ambazo zinaongoza kwa uzalishaji
wa ajira kwa wingi kuwa ni majengo ya biashara ambayo yanazalisha ajira
5537, sekta ya utalii ajira 2011 pamoja na sekta ya huduma inayozalisha
jumla ya ajira 680.
Akizungumzia
kuhusu ubora wa makaa ya mawe, Kaimu Kamishna wa Madini kutoka Wizara
ya Nishati na Madini, John Shija amesema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa
na makaa ya mawe ya kutosha ya kuweza kuchimbwa na kutumiwa kwa zaidi ya
miaka 200.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Uhandisi wa Shirika la Utafiti na Maendeleo
ya Viwanda, Mhandisi Lugano Wilson amesisitiza kuwa kati ya nchi
zinazozalisha makaa ya mawe zikiwemo za India, China na Afrika ya
Kusini, nchi ya Tanzania ndiyo inayoongoza kwa kuwa na makaa ya mawe
yenye ubora unaokubalika.
Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akiongea na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu ongezeko la
wawekezaji nchini katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali
ya Awamu ya Tano.