Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Maswa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa MODECO wakati wa ziara yake wilayani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa (kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka (wa pili kulia) alipotembelea Shule ya Msingi Maswa kukagua ujenzi wa Vyumba vya madarasa wakati wa ziara yake wilayani humo.
Kiongozi wa kikundi cha Simiyu Umoja Arts Group cha Wilayani Maswa, Ally Kazembe (kulia) akitoa maelezo juu ya utengenezaji wa sabuni kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (wa tatu kulia) alipotembelea kikundi hicho wakati wa ziara yake wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa,Mhe.Dkt. Seif Shekalaghe akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa MODECO wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Mhe. Lucas Mwaniyuki akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa MODECO wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka.
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Maswa wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani)katika Mkutano wa hadhara uliofanyika uliofanyika katika Uwanja wa MODECO wakati wa ziara yake wilayani humo.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Serikali Mkoani Simiyu imeagiza Shule zote za Serikali Mkoani humo kuhakikisha kuwa ifikapo Januari 09 mwaka 2017 zinatumia Chaki zinazotengenezwa Wilayani Maswa.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka wakati wa ziara yake aliyoifanya wilayani Maswa kwa lengo la kukagua ujenzi wa Miundombinu ya shule ikiwa ni pamoja na vyumba vya madarasa.
“Kuanzia Januari 09 mwakani shule zitakapofunguliwa Wakuu wa Shule, Walimu wakuu na Wazabuni wanaofanya kazi na shule za Serikali wahakikishe wananunua chaki zinazotengenezwa na Vijana wa Wilaya ya Maswa. Haya ni maelekezo na hayajadiliki”, alisema Mtaka.
Mtaka amewataka Wananchi Mkoani Simiyu kujenga utamaduni wa kupenda na kuthamini vitu au bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa Maono ya Serikali ya Mkoa ni kuzalisha bidhaa zote ambazo malighafi yake yanapatikana hapa nchini na kubadili mtazamo na fikra za Watanzania walio wengi wanaoamini kuwa bidhaa bora ni zile zinazotengenezwa nje ya nchi.
Mtaka amewataka Viongozi wa Kisiasa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Watendaji wa Serikali katika ngazi zote, ili waweze kufikia azma ya Mkoa wa Simiyu kuwa Mkoa kiongozi kwa kutekeleza kwa Vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi , ikiwa ni pamoja na kuifikia Tanzania ya Viwanda kwa kuanzisha viwanda vidogo hususani vya kuyaongezea thamani mazao yanayozaliswa mkoani humo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi cha Vijana wanaozalisha Chaki cha Maswa Family, Kelvin Steven amesema kikundi hicho kimeongeza uzalishaji ambapo kimekuwa kikizalisha katoni 200 kwa siku, wakati mahitaji halisi ya Mkoa wa Simiyu ni katoni 700 kwa mwezi, hivyo kutokana na uzalishaji kuongezeka wanaendelea kutafuta soko nje ya Mkoa.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.Dkt.Fredrick Sagamiko amewataka Wakuu wa Shule na Walimu wakuu wote wilayani humo kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa la kununua chaki zinazotengenezwa na Kikundi cha Vijana (Maswa Family) shule zitakapofunguliwa Januari 09,2016.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa amewataka wazazi wote wenye watoto wanaotakiwa kwenda shule mwakani wahakikishe wanawapeleka na watakaokaidi watakuwa vibarua wa Serikali ambao watafanya usafi katika taasisi za umma ikiwa ni pamoja na shule,hospitali,vituo vya afya, zahanati, vituo vya polisi, masoko na vituo vya mabasi.
Mtaka ameongeza kuwa wazazi wawe waaangalifu na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika kipindi hiki cha sikukuu ili waweze kuwaandalia watoto wao mahitaji yote muhimu ya shule.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu amefanya ziara ya siku moja Wilayani Maswa ambapo ametoa jumla ya mifuko 200 ya saruji ikiwa ni kutimiza ahadi yake aliyoitoa kuunga mkono juhudi za Serikali na wananchi wa Maswa katika ujenzi wa miundombinu ya shule hususani vyumba vya madarasa