Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri
ya Muugano wa Tanzania imeishauri Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya
Jinai ( ICC) kukaa meza moja na nchi wanachama wa Mkataba wa Roma
hususani zile za Afrika ili kutafuta suluhu ya changamoto na tofauti
zilizopo kati ya mahakama hiyo na wanachama wake.
Tanzania
imetoa wito huo siku ya jumatatu kupitia Mwakilishi wake wa Kudumu wa
Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipopokea na kujadili Taarifa ya Utendaji ya
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.
Taarifa
ICC imewasilishwa na Rais wa mahakama hiyo Jaji Slivia Fernandez de
Gumendi katika kupindi ambacho Jumuiya ya Kimataifa imekumbwa na
taharuki baada ya wanachama wawili wa Mkataba wa Roma, Afrika ya Kusini
na Burundi kuwasilisha rasmi katika Umoja wa Mataifa kusudio la
kujiondoa huku Gambia nayo ikitangaza kutaka kujitoa ingawa bado
haijawasilisha rasmi nia yake hiyo.
Mwakilishi
huyo wa Tanzania katika mchango wake amesema, uwepo au kuanzishwa kwa
ICC kulitokana kwa kiasi kikubwa na uungwaji mkono kutoka Afrika. Akasema
uungwaji mkono huo ulitokana hasa baada ya nchi hizo za Afrika
kukatishwa tamaa na kuvunjika moyo baada ya kutokea kwa mauaji ya
kimbari nchini Rwanda.
“Baada
ya kukatishwa tamaa na kuvunjwa moyo, Mahakama hii, ilikuja kuwa chombo
cha kutenda haki dhidi ya watu waliojihusisha na vitendo vya kikatili
vikiwamo vya ukatili dhidi ya binadamu, uhalifu kivita na ukiukwaji
mkubwa wa haki za binadamu. Madhira yasiyoelezeka yaliyotokea Barani
Afrika yakaifanya mahakama hii kuwa chombo cha matumaini dhidi ya wale
ambao hawakuweza kuguswa au walikuwa juu ya sheria”. Akasema Balozi
Manongi
Na
kuongeza. “ Kama nchi mwanachama wa Mkataba wa Roma wa Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai na Mwanachama wa Umoja wa Afrika. Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inatambua kwamba, uhusiano kati ya mahakama na
Afrika ni ule wa misuguano, na ni uhusiano ambao umeleta hofu ya Afrika
kujitoa”.
Balozi
Tuvako Manongi akaeleza zaidi kwamba, hofu hiyo ya kujitoa kwa Afrika
katika mahakama hiyo, haipaswi kuwepo kutokana na mambo kadhaa ambayo
Afrika imejipanga kuyatekeleza kwa manufaa ya bara hilo na watu wake. Baadhi
ya mipango hiyo ni utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo ya Umoja wa
Afrika maarufu kama agenda 2063 ambayo pamoja na mambo mengine
inachagiza katika utawala bora, demokrasia, usawa wa jinsia, kuheshimu
haki za binadamu, haki na utawala wa sheria..
“Viongozi
wa wakuu wa nchi na serikali wa Afrika wameutangaza mwaka 2016 kuwa
mwaka wa haki za binadamu huku mkazo ukielekezwa katika haki za
wanawake. Na katika kutambua kuwa Amani na Haki ni vitu ambavyo haviwezi
kutenganishwa, kwa sababu hizo, tunachotakiwa kuhimiza leo sana sana ni
majadiliano”.Akasisitiza Balozi. Tanzania
pia ikaeleza kwamba ni vema Mahakama hiyo katika utekelezaji wa
majukumu yake ikajenga mazingira ya kuaminiana kati yake na wanawachama
wake.
Tanzania
pia kupitia Mwakilishi wake, imezitaka nchi hususani zile za mataifa
yaliyoendelea kuacha kuzihubiria nchi zinazondelea kama vile zenyewe ni
adilifu sana. Na kusisitiza kwamba, kinachotakiwa wakati huu si
kunyosheana vidole au kulaumiana bali kufanya kazi kwa pamoja ili
kuifanya mahakama hiyo iendelee kutekeleza majukumu yake kwa uwazi ,
haki na kuaminiwa.
Akasisitiza
pia kuwa hata kama matatizo yaliyopo baina ya ICC na Africa yatapatiwa
ufumbuzi. Bado kuna haja na umuhimu kwa nchi za Afrika kuziimarisha na
kuzijengea uwezo Taasisi zake na vyombo vinavosimamia utoaji wa haki na
utawala wa sheria ili viweze kushughulikia makosa ya jinai yakiwamo ya
ukatili dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita badala ya kusubiri au
kutegemea mahakama za kimataifa kama ICC.
Akabinisha
kuwa nchi zinatakiwa kuwajibika kikamilifu siyo kwa kuhofia kuingiliwa
mambo yao ya ndani na ICC bali kwa sababu zinaowajibu wa kwanza wa
kuwalinda raia wao. “Kwa
Afrika matukio kama yale ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cote d’ Ivore,
Rwanda na Sierra-Leone ni kielelezo cha hatari ambayo tunatakiwa
kujikinga nayo.
Vile
vile Tanzania imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,
kutopeleka ICC rufaa zenye malengo wa kisiasa kwani kwa kufanya hivyo
kunachangia kuharibu sifa ya ICC na kuifanya isiaminiwe na kuonekana
inatumiwa na wakubwa kutimiza malengo yao. Pamoja
na kulitaka Baraza la Usalama kutoingiza siasa katika rufaa zake,
Tanzania pia imewashangaa baadhi ya wajumbe wa Baraza hilo na ambao si
wanachama wa Mkataba wa Roma kuwa mstari wa mbele katika kupeleka rufaa
kwenye Mahakama hiyo dhidi ya mataifa mengine.
Wazungumzaji
wote zaidi ya 50 walioomba kuchangia Taarifa hiyo ya ICC pamoja na
kuzungumzia utendaji kazi na changamoto zinazoikabili Mahakama hiyo,
walijielekeza zaidi katika kuelezea masikitiko yao juu ya uamuzi wa
Afrika ya Kusini na Burundi kujitoa. Wasemaji
hao kama ilivyokuwa kwa Tanzania walisisitiza sana umuhimu wapande
zinazopingana kukaa mezani na kuzungumza huku baadhi yao wakizitaka
Afrika ya Kusini na Burundi kufikiria upya uamuzi huo.
Mwakilishi
wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,Balozi Tuvako Manongi
akizungumza wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipopokea na
kujadili Ripoti ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC) hapo
jumatatu. Katika kuchangia Ripoti hiyo, Tanzania imesisitiza haja na
umuhimu kwa ICC kukaa na kuzungumza na Nchi za Afrika ili kutafuta
suluhu ya misuguano baina ya pande hizo mbili.
No comments:
Post a Comment