Na.Aron Msigwa - NEC,Dar es salaam.
Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema
kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaendelea kutoa elimu ya Mpiga Kura kote
nchini ili kuwajengea wananchi uelewa sahihi juu majukumu ya Tume na
chaguzi zinazofanyika nchini.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam Jaji Lubuva amesema baadhi ya wananchi wamekuwa
wakishindwa kutimiza Haki yao ya Kikatiba ya kupiga Kura kuwachagua
viongozi wananowapenda kwa sababu ya kukosa uelewa juu ya Sheria, Kanuni
na taratibu zinazosimamia Uchaguzi.
Amesema
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 inaipa NEC jukumu la
kusimamia na kuendesha Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa upande
wa Tanzania Bara na kubainisha kuwa ili jukumu hilo lifanywe kwa
ufanisi wananchi waliotimiza vigezo vya kupiga kura na wale wanaotarajia
kupiga kura miaka ijayo lazima wapatiwe elimu sahihi ya Mpiga Kura.
Amefafanua
kuwa baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani
mwaka 2015, NEC ilianza kutekeleza programu mbalimbali ikiwemo kutoa
elimu ya Mpiga Kura kuwafikia wananchi moja kwa moja kupitia mikutano
mikubwa inayohusisha viongozi mbalimbali, maonesho ya Sabasaba na
Nane Nane , kutoa elimu ya Mpiga kura kwenye vyombo mbalimbali vya
habari pamoja na kuzitembelea baadhi ya shule za Sekondari za mkoa wa
Singida na Mara.
"
Moja ya shughuli za Tume ni kuendesha na kusimamia uchaguzi wa Rais,
Wabunge na Madiwani nchi nzima kwa upande wa Tanzania Bara, ili shughuli
hii tuifanye vizuri ni muhimu sana tuwapatie wananchi elimu sahihi juu
ya upigaji wa kura, tutafanya jambo hili tukishirikiana na wadau na
Asasi nyingine ambazo tutazipa kibali cha kutoa elimu hii" Amesisitiza
Jaji Lubuva.
Jaji
Lubuva amebainisha kwamba utoaji wa elimu hiyo utaongeza idadi ya
wapiga kura kwenye chaguzi zijazo akitoa mfano wa idadi pungufu ya
wapiga waliojitokeza kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na ule
uliofanyika Oktoba 25 , 2015 ambapo baadhi ya wananchi walioandikishwa
kwenye daftari la kudumu la Wapiga Kura na kupewa vitambulisho
hawakujitokeza kupiga kura.
"
Tunalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu ya Tume ya Taifa
ya Uchaguzi pia umuhimu wa wananchi kushiriki Kupiga Kura, baadhi ya
wananchi wamekuwa wakijitokeza ili wapate vitambulisho jambo ambalo sio
sahihi, mfano mwaka 2010 wananchi milioni 15 walijiandikisha kupiga
kura lakini waliojitokeza kupiga kura ni milioni 8.626 hii ni idadi ya
chini, pia mwaka 2015 wananchi waliojiandikisha walikuwa milioni
23,161,440 lakini waliojitokeza Kupiga Kura ni watu milioni 15,589,639
hapa kuna ongezeko, tunaamini tukiwapatia elimu wengi zaidi
watajitokeza kuwachagua viongozi wanaowapenda " Amesitiza Jaji Lubuva.
Amesema
katika kuendelea kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya Mpiga Kura kwa
wananchi wengi zaidi NEC itashiriki Kongamano na maonesho ya Wiki ya
Vijana yatakayoambatana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa na
Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2016 Oktoba 7 hadi 14, 2016 mkoani
Simiyu ambapo pamoja na Mambo mengine watendaji na Maafisa wa Tume
watatoa elimu ya Mpiga Kura kwa wananchi na kutembelea shule za
Sekondari za mkoa huo.
Aidha,
ili kuboresha chaguzi zijazo ametoa wito kwa wananchi waendelee
kushirikiana na Tume kwa kujitokeza kwa wingi kuuliza maswali na kupata
ufafanuzi wa hoja mbalimbali katika maeneo ambayo watendaji wa NEC
watafika kutoa elimu ya Mpiga Kura.
No comments:
Post a Comment