Matukio : NEC yakabidhi Tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa Waziri Mhagama - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


29 Oct 2016

Matukio : NEC yakabidhi Tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa Waziri Mhagama

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mst. Damian Lubuva (kushoto) akimkabidhi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama, Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015 kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mst. Damian Lubuva (kushoto) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama, wakionesha Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015 ambayo ilikabidhiwa kwa Mhe. Waziri na NEC kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma .
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama akihutubia kwenye mkutano wa kukabidhiwa Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015, kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma .Kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mst. Damian Lubuva na Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji Mst. wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mst. Damian Lubuva akitoa maelezo kuhusu Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015 ambayo aliikabidhi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani akitoa maelezo ya Utangulizi kuhusu Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015, ambayo Tume iliikabidhi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma.Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa NEC Jaji Mst. wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa makabidhiano ya Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015 wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mst. Damian Lubuva (aliyesimama mbele).Taarifa hiyo ilikabidhiwa kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama, kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bungeni mjini Dodoma. Picha zote na Hussein Makame-NEC, Dodoma.

Christina Njovu-NEC, Dodoma

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekabidhi Taarifa ya Tathmini baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015 kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu , Sera, Bunge, Kazi , Ajira, Vijana na Walemavu Mh. Jenista Mhagama mjini Dodoma leo.

Akikabidhi taarifa hiyo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damin Lubuva alisema kuwa Tathmini hiyo imeonesha kuwa Tume hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendesha na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 25 mwaka 2015.

Alisema kwa mujibu wa tathmni hiyo Tume imebaini kuwa sheria, kanuni na zilizotumika wakati wa Uchaguzi mkuu zilikuwa chachu ya kufanikisha Uchaguzi Mkuu, Watendaji wa Uchaguzi walionesha kuwa na uelewa wa kutosha wa Shriea na Kanuni za Uchaguzi.

Jaji Mst. Lubvuva alisema kuwa lengo la tathmini hiyo ni kupata taswira halisi ya Tume kutoka kwa Wadau kwa lengo la kujenga msingi bora wa utekelezaji wa chaguzi zijazo na kujua kwa nini baadhi ya maeneo yalikuwa na mwitikio mdogo katika kupiga kura wakati yalikuwa na mwitikio mkubwa kwenye kuandikisha wapiga kura kwenye Daftari la kudumu la Wapiga Kura.

Alisema kuwa Tathmini hiyo ni ya kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa Tume hiyo mwaka 1993 ambayo imeweza kuwapatia mrejesho juu ya utekelezaji wa Uchaguzi Mkuu kutoka kwa wadau wa Uchaguzi .

Alibainisha kuwa wakati wa tathmini hiyo wadau wengi walionesha kuridhishwa na utendaji wa Tume katika kusimamia Uchaguzi Mkuu na kutangaza matokeo kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo.

Akipokea Taarifa hiyo , Waziri wa Nchi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuweza kufanikisha Uchaguzi Mkuu ulikuwa na changamoto nyingi na ushindani mkubwa wa kisiasa na kufanikiwa kufanya tathmini ya Uchaguzi Mkuu ambayo imekabidhia kwake kwa niaba ya Serikali.

“Ni kweli kwamba wananchi wengi wamekuwa na mwamko wa kisiasa katika jamii yetu, hasa vijana , hivyo taarifa hii itasaidia sana wananchi kuifahamu vyema zaidi namna Tume inavyosimamia , kuendesha na kuratibu mchakato mzima wa Uchaguzi kuanzia uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hadi kutangaza matokeo.” Alisema Waziri Mhagama.

Alisema Tathmini hii itawawezesha wadau mbalimbali kuitumia kama nyenzo muhimu katika kushiriki na kufanya maandalizi ya chaguzi zijazo.

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Bw. Ramadhan Kailima katika maelezo ya utangulizi alieleza kuwa tathimini hiyo ilitumia njia ya mahojiano ya ana kwa ana na majadiliano na ilijumuisha makundi 192 ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na makundi 192 ya vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 35.

Alisema matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa kati ya watendaji 1,029 walihojiwa na watendaji wengi kati wao walisema taratibu mbalimbali za uchaguzi hadi kutangaza matokeo zilizingatiwa.

Bw. Kailima aliongeza kuwa kuhusu Elimu ya Mpiga Kura wadau wa Uchaguzi 1,915 waliohojiwa kuhusu uelewa wao juu ya Elimu ya Mpiga Kura kati yao Wadau 1,463 sawa na asilimia 76.4 walisema kuwa walikuwa na uelewa wa Elimu ya Mpiga Kura na Watu 452 sawa na asilimia 23.6 hawakuwa na uelewa.

Kutokana na tathmini hiyo Bw. Kailima alisema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imejipanga kutoa Elimu ya MpigaKura kwa lengo la kuwafikia wananchi na wadau moja kwa moja na imeweza kushiriki katika maonyesho mbalimbali yakiwemo ya Sabasaba, Nanenane , Mkutano wa Tawala za Mitaa Tanzania na Wiki ya Vijana iliyofanyika Mkoani Simiyu.

Sambamba na hilo, aliongeza kuwa Tume imepanga kuhudhuria na kutoa Elimu katika mikutano ya viongozi mbalimbali ikwemo viongozi wa Dini, Mabaraza ya Madiwani na mikutano mikuu ya vijiji na mitaa. Kutoa elimu ya Mpiga Kura kwa njia ya luninga, redio, mabango na mitandao ya kijamii, Kutoa vibali vya kutoa elimu ya Mpiga kura kwa Taasisi na Asasi.

Kufanyika kwa tathmini Baada ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015 ni mojawapo ya ukamilishaji wa mzunguko wa Uchaguzi huo ambao ulitanguliwa na zoezi kukabidhi ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kwa Mh. Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ikulu jiji Dar es Salaam na ni mwanzo wa kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi mwingine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad