Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) Alvaro Rodriguez amesema vijana ndio chachu kubwa ya maendeleo endelevu kama watatumika ipasavyo.
Alisema kwa nchi kama ya Tanzania, yenye idadi yake ya vijana ipatayo milioni 30 ni vyema ikajielekeza katika namna ya kuiitumia vyema nguvu hiyo.
Akizungumza katika mafunzo ya kuwezesha vijana kutambua malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), alisema ni vyema watu wakatambua umuhimu wa kuungana pamoja kukabiliana changamoto zilizopo.
Alvaro ambaye alikuwa akitoa mafunzo kwa vijana na kujibu baadhi ya maswali yao mwishoni mwa wiki alisema kwamba maendeleo yanahitaji kufanyiwa kazi na kwamba kuwapo kwa mifumo ya kupasha habari ya kisasa sio sababu ya kuwezesha au kukwamisha maendeleo.
Alisema mifumo ya kupashana habari ya kisasa kama mitandao ya kijamii ambayo inaonekana kama ndio njia pekee ya kufikia taarifa haikuwapo wakati mataifa ya magharibi yanaendelea, hivyo suala la mifumo hiyo si kitu cha ziada zaidi ya juhudi binafsi ya kukabiliana umaskini kabla ya kujiunga kwa pamoja .
Alisema nadharia ya uwingi ndio ya msingi katika utekelezaji wa malengo endelevu kwa kuwa inatafsiri malengo hayo katika utekelezaji kuanzia ngazi za serikali na mipango yake.
Alisema vita ya sasa ya kukabiliana na umaskini wa uliokithiri inaweza isifanikiwe lakini kuondoa umaskini wa aina hiyo inawezekana kama ilivyo katika mataifa ya China, India, Korea na hata Chile.
Maendeleo endelevu yenye malengo 17 yamedhamiria katika miaka 15 ijayo kuleta uwiano wa maendeleo katika nchi moja moja na kwa ujumla ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na umaskini ambayo ndio malengo ya haraka.
Maendeleo endelevu (SDGs) yamejipanga kutekelezwa kuanzia yaliposhia malengo ya milenia ikiwa ni msukumo mpya wa kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii duniani kote.
Kwa mujibu wa Alvaro malengo hayo ambayo yamejikita zaidi kukabili umaskini uliokithiri lakini pia kuleta mizania katika maeneo matatu ya maendeleo endelevu kwenye uchumi, jamii na mazingira amewataka vijana hao kuhakikisha kwamba wanajitolea kwa kuwa misaada haijawahi kuamsha maendeleo.
Alisema ruzuku na misaada si kichocheo cha maendeleo na kwamba maendeleo yanaweza kuangaliwa kwa kuangalia pia dhima ya kisiasa, kidini au nyinginezo ambayo inatoa majibu ya namna ya kuenenda katika kukamata ustawi wa jamii.
Alisisitiza katika maelezo yake kwamba serikali nyingi zimekuwa zikikabiliana na rushwa kwa lengo la kukabiliana na umaskini uliokithiri huku akiipongeza serikali ya Tanzania kuona kwamba vita yake kubwa ni kukabili umaskini lakini pia kwa kukabili rushwa.
Alisema kuishi pamoja na kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu kutasaidia kuleta maisha yanayotakiwa ya hali ya juu yenye kujali mazingira ambatana.
Pia Alvaro alikumbusha maelezo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba hata mataifa hohehahe yanaweza kubadilisha maisha ya watu wake na kitaifa kama ilivyofanya China, India na Chile na kwamba mataifa hayo ambayo miaka 50 iliyopita zilikuwa sawa na Tanzania sasa zina mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo.
Alisema ni wajibu wa dunia kukabili umaskini uliokithiri kwa kumshirikisha kila mtu katika malengo hayo 17 bila kumwacha mtu nyuma.
Akijibu maswali mbalimbali ya vijana kuhusu hatima yao alisema kwamba vijana ni nguvu kubwa kama itaamua kuwa chanya itawezesha maendeleo na kama ikiamua kuwa hasi itasababisha mitafaruku mikubwa huku akitolea mfano kuwa hata Al Shabab walipoamua kukabili serikali kuleta maendeleo walikubaliana katika mazingira hasi na kuleta vurugu kubwa.
Alisema Shabab maana yake ni vijana lakini hatua waliyochukua kukabiliana na umaskini haikubaliki kwa kuwa imekuwa ikichochea ghasia.
lisema majadiliano yanayoshirikisha vijana ili kuongeza uelewa katika malengo ya SDGs yatakuwa ni heri kubwa kama yatazingatiwa kwani yatawezesha kwa namna moja kuona mbele na kushirikiana katika utekelezaji.
Alisema ni vyema kama utawala bora ulivyoingizwa kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa malengo mengine kama mazingira na maendeleo ya kijamii katika elimu bila ubaguzi.
Alisema kwa sasa suala si kutambua bali namna ya kushirikisha malengo hayo na mipango ya maendeleo ili kufanya malengo kuonwa kwa wazi na kutafsiriwa katika maendeleo endelevu.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjfrPXfor0V6f_X96D-13xMbLiRZ9WYUsoF9miAPmZv2dtwBZShJWI9dEIXLkjrHeuj2ZFpKzCQ3pkMICmMfoaz-nAfFkhf9nGEWJB9XfTsoOyCaCHzOoyG0etw_-_QWjWDZ0rHcNUuN5QY/s640/nikki+2.jpg)
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) Alvaro Rodriguez (kulia) akimkabidhi cheti Msanii wa muziki wa Hip Hop nchini, Nikki wa Pili, mhitimu wa Mafunzo ya siku moja ya Vijana wahamasishaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na kufanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment