Mbunge
wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo (wa tatu kutoka kulia) akizungumza jambo wakati wa makabidhiano
ya vitabu vya shule za Sekondari na Msingi. Wengine katika picha ni
baadhi ya wabunge wa Mkoa wa Mara kutoka vyama mbalimbali ambao walifika
kwa ajili ya kukabidhiwa vitabu.
Shehena
ya vitabu ambavyo vilikabidhiwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini
na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa Wabunge
wote wa Mkoa wa Mara.
Mbunge
wa jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo (kushoto) akimkabidhi vitabu Mbunge wa jimbo la Tarime,
Ester Matiko (Chadema) katikati. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt.
Vicent Naano ambaye alishuhudia makabidhiano hayo.
Mbunge
wa jimbo la Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) kulia akitoa shukrani
kwa Mbunge wa Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo (wa pili kushoto) mara baada ya kukabidhiwa vitabu vya
shule za Msingi na Sekondari kwa ajili ya shule za jimbo lake. Wengine
katika picha ni wabunge wa Mkoa huo.
Mbunge
wa jimbo la Bunda Vijijini, Boniface Mwita (CCM) katikati akipokea
vitabu vilivyokabidhiwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto). Kulia ni Mkuu
wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Vicent Naano.
Mbunge
wa jimbo la Serengeti na Katibu wa Umoja wa Wabunge wa Mkoa wa Mara,
Marwa Ryoba (Chadema) akizungumza wakati wa makabidhiano ya vitabu. Wa
pili kulia ni Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye alikabidhi vitabu hivyo kwa
wabunge wa Mkoa huo.
Mbunge
wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo amekabidhi vitabu vya sayansi na hesabu 25,000 vyenye
thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 kwa Wabunge wote wa Mkoa wa
Mara kwa ajili ya shule za msingi na sekondari mkoani humo.
Makabidhiano
hayo yamefanyika jana katika uwanja wa Mukendo uliopo Musoma Mjini
Mkoani Mara na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Vicent
Nnano na wananchi mbalimbali waliofika katika uwanja huo ili kushuhudia
tukio hilo la kihistoria.
Akizungumza
katika makabidhiano hayo, Profesa Muhongo alisema lengo la kukabidhi
vitabu hivyo kwa wabunge hao ni kuhakikisha elimu hususan katika masomo
ya sayansi inaboreka ili kuwa na wanayasansi wengi zaidi.
Alisema
vitabu hivyo ni kwa majimbo yote ya Mkoa wa Mara bila kujali itikadi za
kivyama. "Ndugu zangu vitabu hivi ni kwa ajili ya kuboresha elimu kwa
watoto wa Mkoa huu, ninakabidhi kwa wabunge wote bila kubaguana. Itikadi
za kivyama hazina nafasi katika suala la maendeleo," alisema Profesa
Muhongo.
Aliongeza
kuwa anatarajia kupokea shehena nyingine ya vitabu ambayo atakabidhi
kama zawadi ya Krismasi kwa shule zenye maktaba za Musoma Vijijini.
"Lengo
langu ni kuhakikisha Mkoa wetu wa Mara unarudisha hadhi yake ya ufaulu
mashuleni hasa katika masomo ya sayansi kama ilivyokuwa huko zamani,"
alisema.
Aliongeza
kwamba ajenda kuu ya wabunge wote wa Mkoa wa Mara ni maendeleo kwa
wananchi na kuahidi kuwa ataendelea kutoa misaada mbalimbali katika
majimbo yote ya mkoa huo.
"Huu
ni mwanzo na sio mwisho; ninaahidi kuendelea kushirikiana na wabunge
wote wa Mkoani hapa katika kuhakikisha kunakuwa na maendeleo endelevu,"
alisema Profesa Muhongo.
Alisema
Wabunge wa Mkoa wa Mara wameamua kuweka kando tofauti zao za kisiasa na
badala yake kushirikiana ili kuleta maendeleo kwa wananchi
waliowachagua.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano hayo, Katibu wa Umoja wa Wabunge wa Mkoa wa Mara
ambaye ni Mbunge wa jimbo la Serengeti (Chadema), Marwa Ryoba
alimpongeza Profesa Muhongo kwa upendo na uzalendo alionao kwa wananchi
wa Mara na kuahidi kuendelea kumuunga mkono kwa ajili ya maendeleo ya
Mkoa huo.
"Profesa
Muhongo ni Mwenyekiti wa Umoja wetu, tunafarijika na tunayo bahati sana
kuwa na Mwenyekiti wa aina hii maana yeye si mtu wa maneno zaidi hua ni
vitendo," alisema Ryoba.
Ryoba
aliahidi kuhakikisha vitabu vinatumika kama ilivyokusudiwa na aliwasihi
wananchi wa Mara kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Profesa Muhongo
za kuwaletea maendeleo.
Wabunge
wengine waliokuwepo kwenye makabidhiano hayo ni Ester Matiko (Tarime
Mjini, Chadema), John Heche (Tarime Vijijini, Chadema), Boniphace Mwita
(Bunda Vijijini, CCM), Kangi Lugora (Mwibara, CCM) na ambao hawakufika
walituma wawakilishi.
Wabunge hao kwa pamoja walimshukuru Profesa Muhongo na walimpongeza kwa uzalendo wake na kueleza kuwa ni mfano wa kuigwa.
No comments:
Post a Comment