Waziri
wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo akisalimiana na viongozi wa
Chama na Serikali alipowasili Chaani Masingini kukagua kituo cha Afya
cha kijiji hicho kufuatia mwaliko wa Mwakilishi wa Jimbo hilo Nadir
Abdul- latif.
Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya
Kaskazi ‘A’ Hassan Ali Kombo na Daktari dhamana wa Wilaya hiyo Rahma
Abdalla Maisra wakati akikitembelea kituo cha Afya cha Chaani Masingini.
Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akifuatana na viongozi wa Jimbo la Chaani
wakiangalia tanuri la kuchomea taka za kituo cha Afya cha Chaani
Masingini alipotembelea kituo hicho.
Mwakilishi
wa Jimbo la Chaani Nadir Abdul-latif akimkaribisha Waziri wa Afya
Mahmoud Thabit Kombo kuzungumza na wananchi waliofika kituo cha Afya cha
Chaani Masingi ambacho kinahitaji matengenezo makubwa.
Waziri
Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na wafanyakazi wa kituo cha afya cha
Donge na Kamati Kiongozi ya Jimbo hilo katika Kituo cha Afya cha Donge
Wilaya Kaskazini B.
Mkuu
wa kituo cha Afya Donge vijibweni Miza Ali Ussi akitoa maelezo kwa
Waziri wa Afya (hayupo pichani) alipotembelea kituo hicho kujua
changamoto zinazowakabili.
Mwakilishi
wa Jimbo la Donge Dkt. Khalid Salum Mohammed akizungumza katika
mkutano huo (kulia kwake) ni Mkuu wa kituo cha Afya Donge Miza Ali
Ussi. Picha zote na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.
Na RAMADHANI ALI/MAELEZO ZANZIBAR
Waziri
wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo amezitaka Kamati Kiongozi za
Majibo kusimamia kikamilifu vituo vyao vya Afya na kuhakikisha majukumu
waliyopangiwa wanayatekeleza kikamilifu ili kuimarisha huduma katika
vituo hivyo.
Alisema
Serikali imebadili mfumo katika kusimamia vituo vya afya kwa kuvipeleka
moja kwa moja kwa jamii kusaidia huduma ndogo ndogo huku Serikali kuu
ikibakia na jukumu lake la msingi la kuvipatia vifaa vya matibabu,
dawa na mishahara ya wafanyakazi.
Waziri
Mahmoud Thabit Kombo alieleza hayo alipofanya ziara ya kutembelea vituo
vya Afya vya Mkoa wa Kaskazini Unguja kujua changamoto zinazowakabili
wafanyakazi wa vituo hivyo katika kutoa huduma bora.
Alisema
huduma ya matengenezo madogo madogo, kulipia umeme na maji, kuviwekea
uzio na ulinzi sasa vipo chini ya Kamati Kiongozi za Majimbo ambazo
zinaundwa na Wabunge, Wawakilishi, Madiwani, Masheha na Mkuu wa kituo
cha Afya husika.
Aliongeza
kuwa hivi sasa Serikali haitoa kipaumbele kujenga vituo vipya vya Afya
bali inaelekeza nguvu zake kuviimarisha vituo viliopo kwa kushirikiana
na mradi wa ORIO na Milele pamoja na Kamati Kiongozi za Majimbo.
Aliwahakikishia
wananchi wa Jimbo la Chaani kwamba kituo chao cha Afya cha Chaani
Masingini, ambacho kimesitisha kutoa huduma kwa miaka mitano kutokana na
kuwa kibovu, kitaanza kufanyiwa matengenezo makubwa hivi karibuni
kupitia Mradi wa ORIO.
Waziri
wa Afya aliwataka viongozi na wafanyakazi wa sekta ya Afya kuwapa
ushirikiano wa karibu wakunga wa jadi ambao wanatoa mchango mkubwa
katika kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga wakati wa
kujifungua.
Alisema
wakunga wa jadi bado wanaendelea kuaminiwa na wanachi wengi, hasa
sehemu za vijijini, kutokana na huduma nzuri wanazotoa kwa wateja wao na
ameshauri wapatiwe vitambulisho maalum ili waweze kutambulika.
Aidha
alisema Zanzibar imepata sifa kubwa mbele ya Jamii ya Kimataifa katika
kupambana na Malaria na maradhi mengine yaliyokuwa yakiwasumbua
wananchi, lakini hali sio nzuri katika kupunguza vifo vya wajawazito na
watoto wachanga hivyo ametaka juhudi zaidi ifanywe kukabiliana na tatizo
hilo.
Akinamama
wa Jimbo la Chaani walimueleza Waziri wa Afya kuwa wanapendelea zaidi
kujifungua kwa wakunga wa jadi kutokana na kauli zisizoridhisha kutoka
kwa wakunga wa vituo vya Afya wanapokwenda kujifungua.
Walishauri
kutolewa elimu ya ukarimu na upole kwa wakunga wa vituo vya afya ili
kuwajengea imani wajawazito kwenda kujifungulia kwa wingi katika vituo
hivyo.
Mwakilishi
wa Jimbo la Chaani Nadir Abdul-latif alimuhakikishia Waziri wa Afya
kwamba yupo tayari kutoa kila msaada unaotakiwa ili kuona huduma za Afya
katika Jimbo hilo zinaimarika.
Waziri wa Afya alitembelea vituo vya Afya vya Chaani Masingini, Chaani Kikobweni na Kituo cha Afya Donge.
No comments:
Post a Comment